.

MAZOEZI YA KIJESHI YA IRAN YANA UJUMBE WA AMANI

Feb 26, 2017

Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema lengo la mazoezi ya majini ya Wilayat 95 ni kutuma ujumbe wa amani na urafiki kwa nchi za eneo sambamba na kuinua kiwango cha kujihami Iran.
Admeri Habibullah Sayyari Kamanda wa Jeshi la Majini la Iran aliyasema hayo Jumamosi usiku katika mahojiano na Kanali ya Pili ya Televisheni ya Iran. Amesema awamu ya mwisho ya mazoezi ya kijeshi yaliyopewa jina la "Wilayat 95" yanaanza leo Jumapili na kuongeza kuwa, upana wa eneo la mazoezi ni karibu kilomita mraba milioni mbili kuanzia Lango Bahari la Hormoz kuelekea  Bahari ya Oman hadi Kaskazini mwa Bahari ya Hindi yapata daraja 10 kutoka mstari wa ikweta.
Admeri Sayyari amesema, kati ya malengo ya mazoezi hayo ni kuwapa wanajeshi vijana uzoefu wa kikazi na kufanyia majaribio silaha mbali mbali. Aidha ametaja lengo jingine la luteka hiyo kuwa ni kudumisha amani katika eneo na kukabiliana na ugaidi pamoja na uharamia na kuongeza kuwa: "Hadi sasa misafara ya meli za kivita za Iran imezisaidia meli za nchi 25 duniani zikiwemo za Ufaransa, Uingereza na Marekani katika kukabiliana na maharamia.
Manowari ya Iran katika mazoezi ya kivita
Admeri Sayyari amesema tokea mwaka 2008 hadi sasa, manowari za Iran zimesindikiza meli za mafuta na za kibiashara zipatazo 3,850  katika eneo la Bahari ya Hindi na Babul Mandab.
Admeri Sayyari amesema Iran ina uhusiano mzuri na nchi zote zenye mipaka katika Bahari ya Hindi na Bahari ya Kaspi na kuongeza kuwa, mwaka 2018 Iran itakuwa mwenyeji wa makamanda wa majeshi ya majini ya nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช