.

UN YATAKA UCHAGUZI UFANYIKE KUHUSU MAUAJI KASAI, DRC

Feb 26, 2017

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa taarifa likilaani vikali matukio ya utumiaji mabavu yaliyotokea katika miezi ya hivi karibuni huko Kasai, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na kuihimiza serikali ya nchi hiyo kuchunguza mara moja matukio hayo.
Katika taarifa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa  limeashiria ghasia katika miezi ya hivi karibuni huko  Kasai na kutokana na hali hiyo, wajumbe wa Baraza hilo wamesema wana hofu kutokana na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kibinadamu za kimataifa kukiwemo wanamgambo kutumikisha watoto vitani na jeshi la serikali kuua raia.
Wamesema vitendo vyote hivyo vinaweza kuwa uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa hivyo wametaka serikali iwajibike kulinda raia na ijizuie kutumia nguvu za kijeshi kupita kiasi.
Wameitaka serikali kufanya uchunguzi usioegemea upande wowote na wahusika wafikishwe mbele ya sheria huku wakisema kuwa ujumbe wa umoja huo DRC, MONUSCO utakuwa tayari kusaidia iwapo utaombwa kufanya hivyo.
Kuhusu uchaguzi, wajumbe hao wamesisitiza umuhimu wa serikali ya DRC na wadau wa kitaifa kuchukua hatua zote muhimu za kuandaa uchaguzi huo bila kuchelewa na kuhakikisha mazingira ni salama kwa uchaguzi huru na wa haki.
Waasi nchini DRC
Wametoa wito kwa wadau wa maendeleo wa DRC kusaidia ili kufanikisha uchaguzi huku wakisema wako tayari kufanikisha utekelezaji wa makubaliano ya tarehe 31 mwezi Disemba mwaka jana yanayohusisha pia uchaguzi.
Siku chache zilizopita, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein aliitaka serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuchukua hatua za haraka kusitisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya raia yanayofanywa na jeshi la nchi hiyo. Alisema kuna habari za kuaminika na madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika eneo la Kasai  ya Kati na Mashariki na jimbo la lomami, huku kukiwa na kuzorota kwa kasi hali ya usalama na watu wakilengwa na askari kwa madai ya kuwa na uhusiano na wanamgambo wa ndani.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช