Breaking News

Your Ad Spot

Mar 25, 2017

MBUNGE RIDHIWANI NA MADIWANI WA CHALINZE WAIKALIA KOONI CHALIWASA

Mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete akizungumza na madiwani wa halmashauri hiyo katika baraza la madiwani. (picha na Mwamvua Mwinyi)


Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete pamoja na madiwani wa halmashauri ya Chalinze ,wameujia juu uongozi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Chalinze CHALIWASA kwa kushindwa kusambaza maji ili kuondoa kero hiyo .
Amesema mradi huo ulitakiwa kukabidhiwa mwezi huu jimboni hapo lakini unasuasua.
Ridhiwani aliyasema hayo kwenye baraza la Madiwani lililofanyika Lugoba.
Alisema tatizo la ukosefu wa maji, bado ni kubwa hivyo inaonekana uongozi wa Mamlaka hiyo umeshindwa kutatua.
Ridhiwani alifafanua kwamba hadi sasa hakuna matenki yaliyojengwa na mabomba hayajafukiwa hivyo ni ndoto za alinacha mradi huo kukamilika mwezi huu.
Kwa mujibu wake, waziri wa maji anapaswa kulieleza bunge na wananchi wa Chalinze fedha za maji zilizopelekwa kwa ajili ya mradi huo na mwezi wa kuumaliza .
"Kama mradi huu utaendelea kusuasua wananchi na wawekezaji wanaokimbilia kuwekeza Chalinze watashindwa kutimiza malengo yao na kuendelea kuishi kwenye adha hii inayowapa wakati mgumu "alisema Ridhiwani.
Nao madiwani walisema, kama uongozi wa mamlaka hiyo umeshindwa kazi basi wawapishe .
Diwani wa Lugoba, Rehema Mwene,aliiomba serikali imsimamie mjenzi wa mabomba na matenki amalize kazi hiyo.
Nae Hassan Mwinyikondo, alieleza hatari kubwa kwa wananchi wa maeneo ya Bwilingu na Chalinze ambao wanatumia maji yasiyo safi wala salama.
Alisema mradi wa maji wa CHALIWASA hauna faida, kutokana na wananchi kukosa maji kwa kipindi kirefu.
Hussein Hading'oka aliweka hofu katika kipindi kinachokuja kuwa cha mvua za masika na kuongeza kwamba mara kadhaa viongozi wa CHALIWASA wamekuwa wakisema kipindi cha mvua mitambo yao huwa inasumbuliwa na tope.
hivyo kushindwa kufanyakazi za kusukuma maji.
Alimshangaa Meneja wa Mamlaka hiyo Mhandisi Christer Mchomba kushindwa kuhudhuria kikao hicho kama alivyotakiwa na Mkurugenzi Edes Lukoa .
Meneja huyo alitakiwa kwa ajili ya kuwapatia Madiwani hao maelezo ya kina kuhusiana na tatizo sugu la maji linalowakabili wananchi wa Halmashauri hiyo kwa miaka mingi sasa.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Edes Lukoa alisema Halmashauri imetenga bajeti iwa ajili ya maeneo ambayo hayafikiwi na CHALIWASA hivyo mamlaka hiyo lazima iwe na mpango wake.
Hivi karibuni Waziri wa Mazingira Januari Makamba alipofanya ziara ndani ya Halmashauri hiyo alifika eneo la chanzo cha maji Wami na kutoa maagizo kwa wilaya na mkoa.
Aliagiza Mkuu wa wilaya Alhaj Hemed Mwanga kuhakikisha na Mkoa wanakutana na wenzao wa Morogoro kuzungumzia suala la wafugaji wanaotokea Morogoro kuvamia kando ya mto WAMI na kuhakikisha wakulima wanaolima kando ya mto wondolewe mara moja.
Mwisho

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages