Breaking News

Your Ad Spot

Mar 11, 2017

SIKU YA MTUMIAJI MWAKA HUU KUADHIMISHWA MKOANI DODOMA

DODOMA, TANZANIA
Jukwaa la Watumiaji Tanzania limeandaa maadhimisho ya Tisa ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Mtumiaji yatakayofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Chuo cha Mipango, Mkoani Dodoma kuanzia Machi 13 hadi 15, 2017.

Jukwaa la Watumiaji ni chombo kinachounganisha Juhudi za kumuelimisha na kumtetea Mtumiaji kupitia Taasisi za Serikali zinazojishughulisha na utetezi wa Mtumiaji ambazo ni Mabaraza ya Ushauri kwa Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na: Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA-CCC), Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA-CCC), Mamlaka ya Udhibiti wa Sekta ya Mawasiliano (TCRA-CCC), Mamlaka ya Udhibiti wa Sekta za Nishati na Maji (EWURA-CCC) na Tume ya Ushindani (FCC).

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo inasema ‘Haki ya Mtumiaji katika Ulimwengu wa Kidigitali. Kaulimbiu hii imetoholewa kutoka Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mlaji Kimataifa kwa mwaka 2017 iliyotolewa na Asasi Huru ya Utetezi wa Mlaji ‘’Consumers International’’ ambayo inasema "Consumer Rights in the Digital Age’’.

Maadhimisho hayo yatapambwa na shughuli mbalimbali zikiwemo vipindi mahsusi katika redio za kijamii (Community Radios) mjini Dodoma, semina kwa makundi ya wadau mbalimbali ambayo ni wanafunzi wa shule za Sekondari, Wadau kutoka Asasi za Kiraia, Serikali za Mitaa, Madiwani wa Dodoma Mjini na Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu.

Maadhimisho hayo yatafunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Jordan Rugimbana tarehe 13 Machi, 2017 na yatafungwa na Mwakilishi wa Waziri Mkuu, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Mhe. Jenista Mhagama (MB) tarehe 15 Machi, 2017 katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere, Chuo cha Mipango, Dodoma.

Kaulimbiu hii inayotaka haki za mtumiaji katika ulimwengu huu wa kidigitali kuboreshwa imekuja wakati muafaka ambapo inakadiriwa kuwa kwa sasa watu wapatao bilioni 3 ulimwenguni (sawa na asilimia 40 ya idadi ya watu ulimwenguni) kwa sasa wanatumia huduma mbalimbali kupitia mitandao ya mawasiliano ya tovuti ikilinganishwa na asilimia moja tu ya idadi ya watu ulimwenguni waliokuwa wakitumia huduma hizo mwaka 1995.

Kufikia Mwaka 2016, Watanzania wapatao milioni 45 walikuwa wamesajiliwa katika huduma za fedha kupitia mitandao ya simu za mkononi. Miamala inayohusisha huduma za fedha katika simu ni mingi na ya thamani kubwa, na hivyo wateja wanatakiwa kulindwa ili waziamini huduma hizo na kuendelea kuzitumia.

Aidha, Kumekuwa na matatizo ya watumiaji wa huduma hizi kutapeliwa na watoa huduma na wauza bidhaa mitandaoni wasio waaminifu. Wapo watoa huduma ambao pia wamekuwa wakitoza gharama kubwa kwa wateja wanaonunua bidhaa mitandaoni lakini wakaambulia bidhaa zilizo bandia, au chini ya kiwango. Aidha, watumiaji wengine wamelalamikia kutapeliwa na kuibiwa kupitia huduma za fedha katika simu za mikononi.

Kwa kuwa idadi hii inaongezeka kwa kasi, changamoto ya uwepo wa uhakika wa usalama na ulinzi wa mtumiaji wa mitandao hiyo ni jambo muhimu kwa ajili ya maendeleo endelevu ya huduma za manunuzi pamoja na utumaji na upokeaji pesa kwa njia ya mitandao ya wavuti na simu za mikononi.

Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Namba 70/186 Kuhusu Utetezi wa Mlaji la tarehe 22 Desemba, 2015, pamoja na mambo mengine, limebainisha miamala ya manunuzi kwa njia za kielektroniki, pamoja na huduma za fedha kuwa ni maeneo ambayo watumiaji wanatakiwa kulindwa wanapotaka kupata huduma hizo.

Tanzania imekwishaanza kuchukua hatua katika eneo hili kwa kutunga ‘’Sheria ya Mifumo ya Malipo’’ ya mwaka 2015 na kanuni zake za mwaka 2015 pamoja na Sheria ya Kudhibiti Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2015. Aidha, Benki Kuu ya Tanzania, imeanzisha Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo inayodhibiti miamala ya fedha kupitia simu za mikononi.

Kwa upande wa huduma za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa huduma za kifedha na utetezi wa mlaji wakiwemo FCC, TCRA, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Bima (TIRA), Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Asasi ya Kiraia ya Financial Sector Deeping Trust (FSDT) wamekwishaanza juhudi za kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kuelimisha Watumiaji wa Huduma za Kifedha ili waweze kuelewe haki na wajibu wao na kuchukua hatua pale wanapoonewa. Sambamba na hilo wamekwishaanza mikakati ya kuanzisha mfumo wa utetezi wa mtumiaji wa huduma za kifedha.

Baadhi ya Taasisi za Kumtetea Mtumiaji zimeanzisha vilabu vya Utetezi wa Mtumiaji katika shule kadhaa za msingi na sekondari pote nchini. Taasisi hizo ni pamoja na Tume ya Ushindani FCC,  SUMATRA-CCC, EWURA-CCC na TCRA-CCC. Vilabu hivyo vimekuwa ni chachu ya mabadiliko makubwa katika uelimishaji watumiaji kwa jamii ya kitanzania. Madhumuni ya kuanzisha vilabu mashuleni ni kuwajengea uwezo watoto kuhusiana na masuala muhimu ya utetezi wa mtumiaji ili wakue wakiwa na ueledi wa masuala hayo na hivyo kuweza kuteta haki zao na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa soko. 
  
Imetolewa na:
MHANDISI THOMAS MNUNGULI

KAIMU MWENYEKITI -JUKWAA LA WATUMIAJI TANZANIA

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages