Breaking News

Your Ad Spot

Mar 27, 2017

WAZIRI MWIGULU AHIMIZA UADILIFU POLISI

Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba amewataka maofisa na askari Polisi kote nchini kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu ili kujenga taswira nzuri kwa wananchi wanaowahudumia jambo ambalo litaongeza imani na ushirikiano katika kukomesha vitendo vya uhalifu nchini.

Waziri Nchemba ameyasema hayo wakati alipokuwa akifungua kikao kazi cha Maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi kutoka makao makuu, Makamanda wa Polisi wa Mikoa na vikosi kutoka bara na Zanzibar kinachoendelea mkoani Dodoma.

Alisema Pamoja na Jeshi hilo kufanya kazi nzuri bado linakabiliwa na changamoto ya baadhi ya askari na maofisa wasio waadilifu wanaofanya vitendo vya  kuwabambikia wananchi kesi na wakati mwingine kuwabadilishia kesi ili kujenga mazingira ya kupatiwa rushwa jambo ambalo ni kinyume na maadili ya askari Polisi.

“Fanyeni kazi kwa weledi hasa kwa kuwasimamia waliopo chini yenu kwa kuwa wapo baadhi yao bado hawataki kubadilika na katika awamu hii lengo letu ni kutoa haki kwa maskini hivyo ninyi kama wasimamizi wa sheria mnapaswa kutenda haki mnapofanya kazi zenu na wale wasiotaka kubadilika hamna budi kuchukua hatua ” Alisema Nchemba.

Aidha alilitaka Jeshi hilo kuwachukulia hatua bodaboda wanaofanya makosa na wale wasiokuwa na makosa waachwe waendelee na majukumu yao ya kujipatia kipato na kuachana na dhana ya kuwa kila bodaboda ni mhalifu.
Kwa upande wake Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP Ernest Mangu alisema kikao hicho kinafanyika kwa siku tatu kwa lengo la kufanya tathmini ya utendaji kazi kwa mwaka uliopita na kuweka mikakati kwa mwaka huu ili kuendeleza juhudi za kukabiliana na vitendo vya uhalifu hapa nchini.

Mangu alisema Jeshi hilo litaendelea na Oparesheni zake za kupambana na uhalifu zikiwemo za dawa za kulevya, uhalifu wa kutumia silaha na wizi wa mtandao kwa mikakati mipya ambayo itaibuliwa katika kikao kazi hicho ili kuhakikisha hakuna mhalifu anayetamba hapa nchini.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge mambo ya nje na usalama Balozi Adadi Rajabu alisema kamati hiyo itaendelea kuishawishi Serikali kuboresha maslahi na vitendea kazi vya Jeshi la Polisi ili Jeshi hilo liweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Ufunguzi wa Kikao kazi hicho ulihudhriwa pia na Waziri Mkuu mstaafu Samweli Malechela, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana pamoja na baadhi ya wabunge na Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba (kulia) pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Ernest Mangu wakiongozwa na askari wa kikosi cha bendera kuingia ukumbini kwa ajili ya ufunguzi wa kikao kazi cha mwaka kinachowahusisha maafisa wakuu wa jeshi la Polisi na makamanda wa mikoa na vikosi kinachofanyika mkoani Dodoma. Picha na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba (kulia) akitoa hotuba ufunguzi wa kikao kazi cha mwaka kinachowahusisha maafisa wakuu wa jeshi la Polisi na makamanda wa mikoa na vikosi kinachofanyika mkoani Dodoma. Picha na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba (kulia) akiongea na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Ernest Mangu wakati wa hafla ya ufunguzi wa kikao kazi cha maafisa wakuu wa jeshi la Polisi na makamanda wa mikoa na vikosi kinachofanyika mkoani Dodoma. Picha na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi.
Baadhi ya maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi wakiimba wimbo wa maadili ya afisa wa polisi wakati wa hafla ya ufunguzi wa kikao kazi cha maafisa hao na  makamanda wa mikoa na vikosi kinachofanyika mkoani Dodoma. Picha na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi. Picha Na Hassan Mndeme.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages