Kuja
kwa mtandao wa intaneti kumepelekea huduma nyingi kuhamia mtandaoni na
hivyo kupunguza idadi ya watu kutembelea ofisi. Kupitia tovuti za
makampuni wateja wamepewa fursa kubwa ya kuperuzi huduma mbalimbali na
kupata taarifa za kutosha ndani ya muda mfupi.
Sekta mojawapo
iliyoyapokea mabadiliko hayo kwa kasi kubwa ni ya utalii na usafiri.
Kama unatembelea mitandao mara kwa mara nadhani utakuwa umegundua kuwa
kuna kampuni nyingi zinatoa huduma hizo kama vile Jumia Travel na
Expedia.
Lakini
haimaanishi kuwa kuja kwa intaneti kutaondoa kuhitajika kwa mawakala.
Kwa asilimia fulani idadi ya wateja kwenda au kuwasiliana na mawakala
imepungua. Lakini Jumia Travel ingependa kusisitiza kuwa mawakala wana
nafasi kubwa kwa wateja hususani katika masuala yafuatayo:
Kupata ushauri wa
kitaalamu. Zoezi la kupanga mchakato mzima wa kusafiri huwa linachosha
sana kama hauna utaalamu mkubwa. Mara nyingi mawakala wa usafiri
wanakuwa na uzoefu mkubwa katika sekta hiyo. Na hii ni kutokana na
kufanya kazi kwa muda mrefu, kujuana na watoa huduma pamoja na mchakato
mzima mpaka safari inakamilika. Mbali na hapo haikugharimu pesa kupata
huduma zao kwani mara nyingi wao hulipwa kwa kamisheni.
Kuokoa fedha.
Mawakala wanaweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha za mteja kwani wanaweza
kumpatia huduma ambazo kwa njia ya kawaida hawezi kuzipata. Na hii ni
kutokana na mahusiano mazuri na ya muda mrefu kwenye biashara waliyonayo
na watoa huduma. Pia kuna bei na ofa zingine huwafikia mawakala kwanza
kabla ya wateja. Kwa hiyo ukiwatumia wao utafaidika nazo tofauti na
ukienda kwa watoa huduma hao moja kwa moja kama mteja.
Kuokoa muda. Zoezi
zima la kupanga kusafiri iwe ndani au nje ya nchi linachosha kutokana na
mlolongo mrefu ndani yake. Lakini unaweza kuutua mzigo wote huo kwa
mawakala wa usafiri. Kwa sababu wao wanakuwa wamekwishafanya utafiti wa
kutosha na kujua wateja wanapendelea vitu gani na ni wapi kwa kuvipata.
Kwa hiyo badala ya kupoteza muda mtandaoni jaribu kuwasiliana na wakala
aliye karibu nawe akusaidie huku wewe ukistarehe kwa kuweka miguu juu
ukisubiria simu kujulishwa kuwa kila kitu kipo tayari.
Ni njia salama
zaidi kwa mteja. Mtu anaweza kujiuliza ni salama kivipi wakati huduma
wanazotoa wao ni sawa na za makampuni husika? Jibu ni rahisi, kuna
wakati matatizo hujitokeza wakati wa kusafiri, kwa mfano, kuchelewa
ndege au safari kufutwa kabisa, au kutopatiwa chumba cha hoteli
ulichokihitaji. Zikitokea changamoto kama hizo na wewe ulitumia wakala
basi hautakiwi kuwa na wasiwasi au kugombana na mtu. Cha kufanya ni
kuwasiliana na wakala wako na yeye atasuluhisha kila kitu.
Wanajua kipi ni
bora kwa wateja wao. Kutokana na kuwepo kwenye sekta ya uwakala kwa muda
mrefu, kwa mfano, miaka 10, 20 au 30, ni dhahiri kwamba watakuwa
wanajua maswali ambayo wateja huuliza na majibu wanayoyatarajia. Hivyo
inakuwa ni rahisi kwao kuwapatia wateja wao kilicho bora zaidi kutokana
na uzoefu walionao. Na kwa kuongezea mawakala hupokea ofa mbalimbali
kutoka kwa mahoteli na kampuni za usafiri kwanza kabla ya wateja. Pia
wao huwa na ofa zao ili kuwavutia zaidi wateja kutumia huduma zao, kama
vile kipindi cha sikukuu na mapumziko mbalimbali.
Unapatiwa
machaguo sahihi kulingana na mahitaji yako. Faida mojawapo ya kuwatumia
mawakala ni kwamba wao hawatoi au kunadi huduma za kampuni moja tu
pekee. Kikubwa wao wanachokizingatia ni kutoa huduma nyingi kadri
wawezavyo na washirika wao wa kibiashara. Hivyo basi ni rahisi kwao
kusikiliza wateja wanataka nini na kuwatimizia kulingana na huduma
walizonazo. Lakini ukienda moja kwa moja hotelini au shirika la ndege ni
wazi kwamba utapata huduma zao tu pekee na si vinginevyo.
Kwa ufupi ukiwa
kama msafiri ni vema kutambua ni aina gani ya safari unayotaka kufanya
kabla ya kutumia wakala. Kama ni safari ya kawaida na haihitaji mambo
mengi unaweza kujipati huduma mwenyewe kwa kuingia mtandaoni. Wapo
mawakala wengi ambao wanatoa huduma mtandaoni na pia wana ofisi, kama
vile Jumia Travel wanavyoendesha shughuli zao nchini Tanzania na
kwingineko ndani na nje ya Afrika.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269