Breaking News

Your Ad Spot

May 1, 2017

SERIKALI YAAHIDI NEEMA KWA WAFANYAKAZI.

Na Nuru Juma, Husna Saidi - MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameahidi nyongeza ya kawaida kwa mishahara na kuwapandisha madaraja wafanyakazi wanaostahili.

Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo leo alipokuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Chuo Cha Ushirika, Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Dkt. Magufuli alisema Serikali ilisitisha upandishaji wa vyeo na mishahara kutokana na kuwepo na watumishi hewa na walioghushi vyeti lakini baada ya kuondolewa Serikali itahakikisha inashughulikia maslahi ya wafanyakazi.

“Watumishi 9932 walikuwa na vyeti feki,watumishi hewa walikuwa 19706 hivyo kama Serikali ingeongeza mishahara inamaana watumishi hawa pia wangefaidika na pesa ambazo hawakustahili kuzipata”, alisema Dkt. Magufuli.

Aidha aliwataka waajiri kuheshimu na kutoa mikataba ya kazi na kutowanyanyasa wafanya kazi wao na wafanyakazi kuomba kazi kulingana na elimu zao na waache tabia ya kughushi vyeti.

Aliongeza kuwa Serikali itashughulikia mfumuko wa bei za bidhaa na kuhakikisha viwanda vingi vitajengwa sehemu mbalimbali nchini ili kuongeza ajira kwa vijana wa kitanzania.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TUCTA Dkt. Yahya Msigwa ameipongeza Serikali kwa kutekeleza ahadi zake na kuopngeza kuwa hiyo ni ishara tosha kuwa Serikali inayodhamira ya dhati ya kuwajali wananchi wake wakiwemo wafanyakazi.

Ameongeza kuwa wanayo imani kubwa kwa Serikali kuwa itatekeleza ahadi yake ya kufanyia maboresho ya maslahi ya umma kama ambavyo umeonyesha nia njema ya kutekeleza ahadi zake.

Alizitaja baadhi ya ahadi zilizotekelezwa kuwa ni pamoja, kupiga vita rushwa na ufisadi, kuondoa watumishi hewa, Serikali kuhamia Dodoma, ujenzi wa miundombinu ya reli, vita dhidi ya dawa za kulevya pamoja na ununuzi wa ndege.

“Ni imani yetu kuwa ahadi hii ya kuboresha maslahi kwa Watumishi wa Umma itatekelezwa kwa wakati kwani tayari umekwisha ondoa mambo yaliyokuwa yanakwamisha zoezi hilo,” alisema Dkt. Msigwa.

Wakati huohuo Katibu Mkuu huyo ameiomba Serikali kuharakisha kubuni namna ambavyo wafanyakazi watanufaika na Mifuko ya Jamii na wanaodai mapato yao kusikilizwa kesi zao kwa wakati.

Maadhimisho hayo yameuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa akiwemo Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai,Naibu Spika Tulia Ackson, Mawaziri Jenister Mhagama na Angella Kairuki, Profesa Jumanne Maghembe na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi pamoja na baadhi ya Wabunge. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Uchumi wa Viwanda Vizingatie Haki, Maslahi na Heshima ya Mfanyakazi”.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages