Breaking News

Your Ad Spot

May 15, 2017

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA ALBINO KITAIFA

Na Husna Said & Nuru Juma- MAELEZO

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uelewa juu ya ualbino yatakayofanyika Juni 13 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. 

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chama cha watu wenye Ualbino Tanzania Nemes Colman Temba alipokutana na waandishi wa habari. 

Temba alisema maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kuibua mijadala na tafakuri kwa wadau juu ya ukusanyaji endelevu wa takwimu,uchambuzi na upatikanaji wa watu wenye Ualbino kwa wakati ili Serikali iweze kuwasajili, kuwahudumia na kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wa ngozi wanakuwa salama.

“Bila ya utaratibu mzuri wa upatikanaji wa Takwimu Serikali haitaweza kupanga vyema juu ya ustawi wa watu wenye ualbino, hivyo maadhimisho ya mwaka huu yataibua mjadala wa umuhimu wa upatikanaji wa takwimu sahihi kutoka ofisi ya Taifa ya takwimu kwaajili ya kusaidia katika mipango ya maendeleo ya watu wenye ualbino”,alisema Temba.

Aidha alisema Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 iliyojumuisha takwimu za watu wenye ualbino ilisaidia kubaini idadi ya watu hao ambapo walikuwa 16,376 wakiwemo Wanaume 7,620 na Wanawake 8,756.

Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Mh.Dkt. John Pombe Magufuli kwa kusikiliza na kutekeleza ombi la masuala ya watu wenye ulemavu kuhamishiwa ofisi ya Waziri Mkuu kwani lilikuwa ombi la muda mrefu kwaajili ya ustawi wa watu wenye ualbino na wenye ulemavu kwa ujumla. 

Kwa upande wake afisa habari na uhusiano wa wa chama hicho, Josephat Torner alisema kuwa, mauaji dhidi ya watu wenye ualbino yamepungua kwa kiasi kikbwa kulingana na hapo awali na mapambano dhidi ya vitendo hivyo bado yanaendelea licha ya ukimya uliokuwepo kwa sasa.

Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu Takwimu na Tafiti kwa Ustawi wa Watu Wenye Ualbino yatahudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo wadau toka Sweden, Uholanzi, Marekani, Canada, Uingereza, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Mataifa mengine.

Siku hiyo ya kimataifa ya uelewa juu ya Ualbino itatanguliwa na shughuli mbalimbali ikiwemo hamasa kupitia vyombo vya habari,uendeshaji wa kliniki za ngozi kwa maalbino pamoja na utoaji wa msaada wa kisheria,midahalo na makongamano na ukusanyaji wa takwimu za watu wenye ualbino.
Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) Bw. Nemes Temba (katikati) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akielezea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uelewa juu ya ualbino mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam Bw.Gabriel Aluga na kushoto ni Afisa Mawasiliano na Habari wa chama hicho Bw. Josephat Torner.
Afisa Mawasiliano na Habari wa Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) Bw. Josephat Torner (katikati) akifafanua jambokwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akielezea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uelewa juu ya ualbino mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Bw. Nemes Temba na kushoto Mwekahazina wa chama hicho Bw. Abdulah Omar.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) Bw. Nemes Temba (mwenye koto jeusi) wakati akielezea maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu wa ngozi mapema hii leo jijini Dar es Salaam. Picha zote na Eliphace Marwa

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages