Breaking News

Your Ad Spot

Sep 18, 2017

SIKU YA MTINDIO WA UBONGO KITAIFA KUFANYIKA DAR ES SALAAM.

Mweka Hazina wa Chama cha Wazazi wa Watoto Wenye Ulemavu wa Mtindio wa Ubongo, Akili na Viungo Tanzania (CHAMAUMAVITA), Bi. Jane Kim akielezea maadhimisho ya Watoto wenye Mtindio wa Ubongo yatakayofanyika tarehe 6, Oktoba mwaka huu mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani, Kushoto ni Mwenyekiti wa CHAMAUMAVITA Bw. Hilali Said. Picha zote na Thobias Robert, MAELEZO
............................

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO.
Chama cha Wazazi na Watoto wenye Ulemavu wa Mtindio wa Ubongo,Akili na Viungo Tanzania (CHAWAUMAVITA) kitafanya maadhimisho ya siku ya mtindio wa ubongo duniani kwa lengo la kuipa jamii uelewa juu ya changamoto wanazozipata watoto wenye matatizo hayo na kuwaleta pamoja familia zinazolea watoto hao ili wabadilishane uzoefu.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na mwenyekiti wa chama hicho, Hilali Said alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo.

“Kwa kawaida Siku ya Mtindio wa Ubongo duniani huadhimishwa kila Jumatano ya kwanza ya mwezi Oktoba lakini kwa mwaka huu itaadhimishwa tarehe 6, ambapo yanategemewa kufanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mjimwema vilivyopo wilaya ya Kigamboni na tunategemea mgeni rasmi wa maadhimisho hayo  atakuwa Mkuu wa Wilaya hiyo”, alisema Said.

Said ameongeza kuwa nchi mbalimbali Duniani huadhimisha siku hiyo kwa  kutoa elimu ya ulemavu wa aina hiyo kwa wananchi ili kupunguza athari zinazojitokeza kwa wazazi na watoto wenyewe pamoja na kuwasaidia wanachama kutetea na kupata haki zao kwa mujibu wa sheria.

Ameelezea mambo sita ambayo yamegundulika kuwa ni changamoto zitokanazo na matatizo hayo duniani kuwa ni fursa za matibabu kwa watoto hao, ukosefu wa dawa, ufahamu mdogo kwa jamii, ukosefu wa elimu, hali halisi ya kimaisha pamoja na mchango wao katika nchi  kama binadamu wengine.

Aidha, Said amefafanua kuwa chama hicho kwa sasa kinafanya kazi Jijini Dar es Salaam pekee ambapo kuna jumla ya vituo kumi vinavyowasaidia watoto wenye matatizo hayo kupata huduma ya mazoezi ya viungo vilivyoathirika mara moja kwa wiki.

Alivitaja vituo hivyo kuwa vipo katika manispaa za Ilala, Kinondoni, Kigamboni, Ubungo na Temeke jijini Dar es salaam.

Kwa upande wake mweka hazina wa chama hicho, Jane Kim ameiomba Serikali kuwasaidia watoto hao kwa kuwapatia mazingira mazuri ya kusomea pamoja na walimu wa kutosha wenye elimu stahiki ikiwa ni pamoja na kuwapatia ulinzi wa kutosha wanapokuwa shuleni ili nao waweze kupata elimu na kutimiza ndoto zao kama watoto wengine.

“Watoto wenye mtindio wa ubongo wana haki sawa na watoto wengine hivyo wanatakiwa kupata haki zote wanazopatiwa watoto wasio na tatizo hilo zikiwemo za mazingira mazuri ya kusomea pamoja na viwanja vya michezo vinavyolingana na hali zao”,alisema Jane.

Chama hicho cha kilisajiliwa  mwezi Machi, 2013 kupitia Msajili wa Vyama vya Kiraia, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kinawahusisha na wazazi wenye watoto walio na mtindio wa ubongo ambao wanafanya mazoezi tiba katika vituo vilivyopo Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages