Breaking News

Your Ad Spot

Oct 25, 2017

RC PWANI ATOA SIKU TATU DC KIBAHA KUONDOA MIFUGO SOGA/KONGOWE, NI KUFUATIA MFUGAJI KUUAWA KWA RISASI BAADA YA KUINGIZA MIFUGO KIHOLELA

NA MWAVUA MWINYI, KIBAHA
Mfugaji aliyetambulika kwa jina la Kidau Kibaderu (35) amefariki dunia kwa kupigwa risasi ya paja ,baada ya kuingiza mifugo kiholela, katika shamba la Mohammed Enterprises huko Soga , Mfuluni tarafa ya Kongowe, Kibaha.

Kufuatia tukio hilo, mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, ametoa siku tatu kwa mkuu wa wilaya ya kibaha pamoja na kamati yake ya ulinzi na usalama wilaya, kuondoa mifugo zaidi ya 5,000 inayodaiwa kuingia kiholela eneo la Soga /Kongowe.

Amesema ni lazima hatua ichukuliwe kwani tayari mtu mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi na wengine watano wanadaiwa kujeruhiwa.

Aidha mhandisi Ndikilo,amewataka wataalamu wa mifugo kuhakikisha wanakwenda kutoa elimu kwa wafugaji ambao hawazingatii sheria na taratibu .

Akizungumzia suala hilo kwa watumishi na watendaji wa halmashauri ya mji wa Kibaha na wilaya ,alieleza kuwa mifugo holela ni ishu na tatizo kubwa .

Mhandisi Ndikilo,alisema ,wafugaji hao waondolewe bila kujali wametokea wapi ili wananchi hasa wakulima wanaovamiwa maeneo yao waishi kwa amani.

“Hali sio shwari,kamati ya ulinzi na usalama na mkuu wa wilaya mfuatilie hili,nimepata taarifa hiyo,mmoja kapigwa risasi na wengine watano wamejeruhiwa ,kesho mtasikia wameuawa zaidi ,”Ni jukumu letu kwenda kuwaondoa wafugaji hao.”

Mhandisi Ndikilo alisema,kwa hilo wategemee kutakuwa na uvunjifu wa amani kama hatua stahiki hazitachukuliwa.

Aliwaasa wafugaji kuacha tabia ya kuingilia maeneo ya wakulima pasipo kufuata taratibu ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.

Akitolea taarifa juu ya tukio la risasi,kaimu kamanda wa polisi mkoani Pwani,mrakibu mwandamizi Blasilus Chatanda  ,alisema Kidau Kibaderu(35)mfugaji mkazi wa Bagamoyo,alifariki  dunia akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya Tumbi baada ya kupoteza damu nyingi kufuatia kupigwa risasi.

Alisema marehemu alipigwa risasi ya pajani katika mguu wa kulia na askari mgambo MG.5285 Iddi Daudi mkazi wa Soga kitongoji cha Bomu.

Chatanda alieleza,kabla ya kukutwa na umauti marehemu anadaiwa kuingiza mifugo katika shamba la Mohammed Enterprises Ltd na wakati walinzi hao wakiondoa mifugo katika shamba hilo,”Marehemu alichomoa sime alilokuwa nalo kwa lengo la kuwadhuru ndipo mtuhumiwa alimfyatulia risasi iliyomjeruhi kwenye eneo la paja na kufariki akiwa anapatiwa matibabu.

Jeshi la polisi mkoani hapo linamshikilia mlinzi huyo na kwa sasa wanaendelea na uchunguzi ambapo atafikishwa mahakamani baada ya kukamilisha taratibu zingine za kisheria.

Nae katibu tawala wa wilaya Kibaha (DAS),Sozi Ngate alisema mifugo hiyo imetoka hifadhi ya Ruvu Kaskazini baada ya kamati ya ulinzi na usalama wilaya kufanya zoezi la kuwaondoa wavamizi katika hifadhi hiyo.

Alisema licha hayo ,lakini wanaahidi kutekeleza agizo la mkuu wa mkoa na watahakikisha watakwenda kuwaondoa na kuzungumza na wafugaji na wananchi katika maeneo hayo .

Sozi alisema wao walipata  taarifa lakini hawakujua idadi ya mifugo iliyoingia kwenye maeneo ya Soga na Kongowe na watafanyia kazi zaidi suala hilo.

Kwa upande wake,mkuu wa polisi wa wilaya ya Kibaha (OCD),Innocent Feksi alisema ,ni kweli kuna tatizo hilo limejitokeza na wameshaongea na pande zote mbili za wamiliki wa mashamba na wafugaji .

Feksi alisema, wamejipanga kwenda kufanya oparesheni kuwaondoa wafugaji walioingia kinyemela.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages