Breaking News

Your Ad Spot

Oct 25, 2017

WALENGWA TABORA WAPOKEA BILIONI 20 ZA TASAF KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MIWILI

NA TIGANYA VINCENT, RS-TABORA
JUMLA ya sh. bilioni 20 zimetolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika Halmashhauri zote za Tabora kwa ajili kunusuru kaya maskini katika eneo hilo.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Tabora na Mratibu wa TASAF Mkoa huo Ngoko Buka wakati  wa kikao cha kutathmini utekelezaji wa TASAF Awamu ya Tatu sehemu ya kwanza kilichowashirikisha Wafadhili ,viongozi kutoka makao Makuu TASAF na wale wa Mkoa na Wilaya ya Uyui.

Alisema kuwa fedha hizo zilitolewa katika kipindi cha kuanzia Julai 2015 hadi Agosti mwaka huu ambapo jumla ya walengwa 45,928 waliwezwa  kunufaika na fedha hizo na hatimaye kubadilisha maisha yao.

Buka alisema kuwa fedha zimesaidia baadhi ya walengwa kuanzisha miradi mbalimbali kama ufugaji wa kuku,bata,mbuzi ,ng’ombe ,ujenzi wa nyumba bora, kusomesha watoto, kuwapa huduma ya kliniki na kuimarisha kilimo.

Alisema kuwa mambo mengine ambayo walengwa wamenufaika nayo ni pamoja na uanzishaji wa biashara mbalimbali ambayo kwa kiasi kikubwa imebadilisha maisha ya walengwa.

Naye Mkuu wa Msafara wa TASAF kutoka Makao Makuu Dkt. Jasson Bagonza alisema kuwa wako mkoani Tabora kuangalia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoratibiwa na Mfuko huo na kujadiliana na wadau mbalimbali ili kuona kama inakwenda malengo ya uanzishaji wake.

Alisema kuwa baada ya tathmini hiyo watakuja na TASAF awamu ya Tatu sehemu ya pili iliyoboreshwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi na wananchi wake.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages