.

WATUMISHI WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII WAMUAGA ALIYEKUWA MKURUGENZI MSAIDIZI WA IDARA YA UTALII, BI.UZEELI KIANGI BAADA YA KUSTAAFU KWA MUJIBU WA SHERIA YA UTUMISHI WA UMMA

Nov 13, 2017

DAR ES SALAAM
Watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii katika Idara ya Utalii wameombwa kumpa ushirikiano Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii Deograsius Mdamu, ili aweze kutimiza majukumu yake kwa ufanisi

Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki katika ofisi ndogo ya Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dar es Salaam  na aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi   Sehemu ya Maendeleo  ya Utalii katika Wizara hiyo , Bi. Uzeeli Kiangi  katika hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya kumuaga baada ya kustaafu mwanzoni mwa mwezi Julai kwa mujibu wa Sheria ya utumishi wa Umma akiwa ameitumikia Wizara kwa kushika nafasi mbalimbali kwa muda wa miaka 33.

Akizungumza katika hafla hiyo alisema  ‘’ Watumishi ni kiungo muhimu katika kumsaidia Mkurugenzi wa Idara ya Utalii kutekeleza majukumu yake, ni matumaini yangu kuwa mtampa ushirikiano katika hili’’

Amesema kupitia  ushirikiano huo  utasaidia kupelekea Wizara kutimiza azma ya kufikia watalii milioni 8 na fedha za kigeni dola bilioni 20 kila mwaka kufikia mwaka 2025

Aidha, Bi.Kiangi aliwataka watumishi kuzingatia miiko ya kazi zao kwa kutojihusisha na vitendo vya kupokea rushwa wanapotimiza majukumu yao, la sivyo serikali hii ya awamu ya tano haitawaacha salama.

‘’Wakati wa utumishi wangu nilijitahidi kukwepa kupokea rushwa kwa kuwa sikujua huyu anayetaka kunihonga katumwa na nani na kwanini anipe rushwa wakati natimiza majukumu yangu jihadharini na watoa rushwa’’ alisisitiza

Katika hatua nyingine,  Bi. Kiangi aliwataka  watumishi wenye tabia ya kujituma kufanya kazi pale tu wanapohisi kazi hiyo ina malipo wajirekebishe mara moja kwa kuanza kufanya kazi zote zenye malipo na zisizo na malipo kwani zina umuhimu katika kuwajenga kitaaluma.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Deograsius Mdamu alisema Idara yake imejipanga kufanya kazi kwa kasi zaidi na kuendeleza yale ambayo Mkurugenzi Msaidizi, Bi. Kiangi aliyokuwa akiyapigania kwa ajili ya maendeleo ya utalii.

‘’Wizara inatambua mchango wako tangu ulipoajiriwa mwaka 1984, tunakuahidi tutakutumia pale tunapohitaji utaalamu wako ili kuhakikisha Wizara inafikia malengo iliyojiwekea’’ alisisitiza

Kwa upande wake, Afisa Utalii Mwandamizi, Josephat Msimbano  wakati  amesema Bi. Uzeeli Kiangi wakati wa utumishi wake alikuwa ni kiongozi aliyeichukia rushwa na yeyote aliyethubutu kutaka kumhonga ili ahudumiwe kwa minajili ya kupindishwa kwa sheria  aligonga mwamba.

Naye Afisa Utalii, Domina Moshi  amesema kwa upande wake, Bi Uzeeli Kiangi alikuwa ni mshauri mzuri, alikua zaidi ya mama na alipenda watumishi wajiendeleze kielimu na ndiye aliyemfanya aende masomoni nchini kujiendeleza kielimu.

Bi. Uzeeli Kiangi kastaafu kwa Mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma akiwa ameihudumia Idara ya Utalii katika nafasi mbalimbali kwa muda wa miaka 33 ambapo aliajiriwa mwaka 1984 kama Afisa Utalii Daraja la tatu ambapo alipandishwa madaraja hadi kufikia Afisa Utalii Mwandamizi daraja la kwanza mwaka 2007.


Mwaka huo huo alipandishwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi kusimamia Sehemu ya Leseni na Uthibiti kwa kipindi cha miaka mitano. Pia, mwaka 2013 hadi julai 2017 alikuwa Mkurugenzi Msaidizi kusimamia Sehemu ya Maendeleo ya Utalii
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Bw. Deograsius Mdamu (kushoto)  akimpongezana na  aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa kusimamia Sehemu ya  Maendeleo ya Utalii katika Idara ya Utalii, Bi. Uzeeli Kiangi wakati wa hafla fupi  ya kustaafu kwake mapema mwezi Julai mwaka huu kwa mujibu wa Sheria ya utumishi wa Umma
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Bw. Deograsius Mdamu (kushoto)  akilishwa keki na  aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa kusimamia Sehemu ya  Maendeleo ya Utalii katika Idara ya Utalii, Bi. Uzeeli Kiangi wakati wa hafla fupi ya kumuaga  baada ya kustaafu mapema mwezi Julai mwaka huu kwa mujibu wa Sheria ya utumishi wa Umma. Wakishuhudiwa na   Afisa Utalii, Marygoreth Mushi (kwanza  kulia)  na Mary Msekela (wa pili kulia)
Aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa kusimamia Sehemu ya  Maendeleo ya Utalii katika Idara ya Utalii, Bi. Uzeeli Kiangi (kulia) akiwa na Afisa Utalii Mwandamizi, Martin Mrema (katikati) wakiwa wanatabasamu huku  wameshika kwa pamoja moja ya zawadi ya saa ya mezani yenye picha ya Bi. Kiangi aliyokabidhiwa katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki  baada ya kustaafu mapema mwezi Julai mwaka huu kwa mujibu wa Sheria ya utumishi wa Umma. Kushoto  ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Bw. Deograsius Mdamu
Aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa kusimamia Sehemu ya  Maendeleo ya Utalii katika Idara ya Utalii, Bi. Uzeeli Kiangi (Kulia)  akiwa na Afisa Utalii Domina Moshi, wakiwa wanatabasamu huku  Bi. Kiangi akiwa ameshika kwa moja ya zawadi ya saa ya mezani yenye picha yake  aliyokabidhiwa katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki  baada ya kustaafu mapema mwezi Julai mwaka huu kwa mujibu wa Sheria ya utumishi wa Umma. Kushoto  ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Bw. Deograsius Mdamu

Aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa kusimamia Sehemu ya  Maendeleo ya Utalii katika Idara ya Utalii, Bi. Uzeeli Kiangi akizungumza katika hafla ya kustaafu kwake

Baadhi ya Watumishi wa Idara ya Utalii wakimsikiliza aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa kusimamia Sehemu ya  Maendeleo ya Utalii katika Idara ya Utalii, Bi. Uzeeli Kiangi akizungumza katika hafla ya kustaafu kwake
1.  Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakiwa kwenye picha ya pamoja mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam  na aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa kusimamia Sehemu ya  Maendeleo ya Utalii katika Idara ya Utalii, Bi. Uzeeli Kiangi (katikati)  katika hafla fupi ya kumuaga baada ya kustaafu mapema mwezi Julai mwaka huu kwa mujibu wa Sheria ya utumishi wa Umma. Kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara Utalii, Bw. Deograsius Mdamu na Afisa Utalii Domina Moshi (kushoto) ( Picha zote na Lusungu Helela- MNRT)

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช