IKULU, DAR ES SALAAM
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza
kuchukuliwa hatua dhidi ya viongozi na watendaji ambao shule za msingi na sekondari
zilizopo katika maeneo yao zinawatoza wanafunzi michango mbalimbali kinyume na
muongozo uliotolewa na Serikali wa utoaji wa elimu bila malipo.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo asubuhi tarehe 17 Januari, 2018 Ikulu
Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.
Joyce Lazaro Ndalichako na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe.
Selemani Said Jafo.
Mhe.
Rais Magufuli amesema Serikali inatoa Shilingi Bilioni 23.875 kila mwezi kwa
ajili ya kuwezesha utoaji wa elimu bila malipo lakini inashangaza kuona bado
kuna walimu wanaendelea kuwatoza michango ama kuwarudisha nyumbani wanafunzi
ambao wanashindwa kutoa michango hiyo.
“Nawaagiza
Mawaziri, sitaki kusikia mwanafunzi anarudishwa nyumbani kwa kushindwa kutoa
michango, na fikisheni maagizo haya kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya,
Wakurugenzi na wote wanaohusika, nikisikia tena mahali jambo hili linaendelea
hawa niliowateua mimi wataondoka.
“Haiwezekani
tumefuta ada, halafu walimu wanaamua kuanzisha michango tena mikubwa ambayo
watu masikini wanashindwa kusomesha watoto wao, na kama wazazi wanataka
kuchangia kitu shuleni wapeleke michango yao kwa Mkurugenzi, lakini sitaki
kusikia mwanafunzi anapewa sharti la kutoa mchango ndipo apokelewe shule”
amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo baada ya kupata taarifa kuwa zipo baadhi ya
shule ambazo wanafunzi wanadaiwa michango mbalimbali tena kwa kiwango kikubwa
ikiwemo chakula, maabara, madawati na ziara za kujifunza, hali iliyosababisha
wazazi kushindwa kumudu.
Waziri
Prof. Joyce Lazaro Ndalichako ameagiza walimu na viongozi wa halmashauri
kuwarudisha shule mara moja wanafunzi wote waliorudishwa nyumbani kwa kutotoa
michango na pia kurejesha mara moja michango iliyokusanywa kinyume na mwongozo
wa Serikali.
Waziri
Mhe. Selemani Said Jafo amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya
kuwasilisha taarifa ya shule ambazo zimetoza michango kinyume na mwongozo wa
Serikali ifikapo Ijumaa wiki hii (tarehe
19 Januari, 2018) ili hatua zichuliwe dhidi ya walimu na maafisa elimu
ambao kwa makusudi wamekiuka mwongozo huo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269