Breaking News

Your Ad Spot

Jan 27, 2018

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUIKARABATI NYUMBA YA BABA WA TAIFA ILIYOPO MAGOMENI

DAR ES SALAAM
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk.Hamisi Kigwangalla leo amefanya ziara katika Makumbusho ya nyumba aliyoishi Baba wa Taifa Mwalimu  Nyerere iliyopo Mtaa wa Ifunda namba 62, Magomeni Jijini Dar es Salaam, na kuahidi kuwa serikali itaifanyia ukarabati ili kuiboresha.

Baada ya kuona mambo mbalimbali ndani ya nyumba hiyo ambayo sasa ni makumbusho Dk. Kigwangalla amekea maoni ya namna ya kufanyiwa maboresho ya nyumba hiyo ikiwemo kuboesha eneo la ofisi na maegesho ya wageni wanaotembelea Kituo hicho cha makumbusho ya nyumba hiyo ya baba wa taifa.

"Nimefika hapa leo kujionea Kituo hichi ambacho ni kielelezo kikubwa cha Mwasisi wa Taifa letu. Hapa pana hazina kubwa na kituo hiki kina mambo mengi sana ya kumuenzi Baba wa Taifa. Kwa hali tuliookuta kwa kweli tutakaa na timu yangu kuona tunafanya maboresho makubwa kabisa ili kiwe kama maeneo mengine yenye Wahasisi wa Mataifa yao, tumeona kama eneo alilozaliwa Mzee Mandela kule Afrika Kusini, nyumba yake imehifadhiwa vizuri na imekuwa na wageni wengi.

Kwa hapa kwetu na sisi tutakaa na wenzetu kutatua changamoto hizi. Hapa tutajenga Maktaba ambapo watu watakuja kusoma vitabu vya Mwasisi wetu na kuona mambo aliyokuwa akifanya. Lakini pia tutaonana na Viongozi wa Halmashauri ya Kinondoni kuona namna ya kupaboresha mahala hapa ikiwemo miundombinu ya Barabara ya kuingia na kutoka eneo ili" alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema, kituo hicho kipo katika hali mbaya kikikabiriwa na changamoto  licha ya kuwa ni kituo muhimu sana hapa nchini.  hivyo amewahakikishia wahifadhi wa Makumbusho hayo mipango iliyopo ni pamoja na kukifanyia marekebisho kutengeneza choo, kupaka rangi pamoja na kufanyia ukarabati mkubwa vionyeshi vya kumbukumbu nzima ya Baba wa Taifa.

Aidha, amesema kuwa, lengo kwa sasa ni kuifanya nyumba hiyo iwe kama nyumba halisi ailivyokuwa akiishi mwenyewe Baba wa Taifa kwani ndani bado kuna vitu halisi alivyokuwa akivitumia Mwasisi mwenyewe huku pia mikakati ikiwa ni pamoja na kununua hata nyumba za jirani ili kuongeza eneo na kuongezwa baadhi ya ofisi na pawe na hadhi kama Mwasisi mwenyewe.

"Kiukweli nimefika hapa kushuhudia makumbusho haya ambayo kiuhalisia hapa ni hazina kubwa sana ya kumbukumbu ya Taifa letu hasa katika harakati za kupigania Uhuru pia zilianzia hapa katika nyumba hii na tutaboresha zaidi kwa kuweka studio maalumu kuboresha CD zote za Baba wa Taifa ambazo zitakuwa zikionyeshwa humu ikiwemo zile za hotuba.

Awali Muhifadhi Mkuu wa Makumbusho hayo,  Neema Mbwana alieleza changamoto zinazoikabili kituo hicho pamoja na kuomba kuboreshwa kwa vitu muhimu ikiwemo ukarabati wa nyumba nzima, ikiwemo, paa na kupaka rangi.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages