.

GAUDENTIA KABAKA: WANAWAKE MSIONE FAHARI KUITWA 'DUME JIKE', BALI KUWENI WENYE MSIMAMO IMARA NA JASIRI KATIKA KUPIGANIA MAENDELEO

Apr 6, 2018

Mwenyekiti ya Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania (UWT) Gaudentia Kabaka akizungumza na Waandishi wa habari leo Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, Suwata Kariakoo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa UWT Bara Eva Kihwelo (Picha na Bashir Nkoromo).

NA BASHIR NKOROMO
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Gaudentia Kabaka amewataka Wanawake kote nchini  wasione fahari kuitwa 'Dume-Jike' bali wawe wanawake wenye msimamo imara na jasiri kwa maendeleo yao na ya nchi kwa jumla.

Gaudentia ameto mwito huo, wakati akiwasilisha salaam maalum za pole kwa ndugu jamaa, marafiki na hasa wanawake wote hapa nchini na duniani kote kufuatia kifo cha Winnie Mandela aliyemwelezea kuwa alikuwa amwanamke shupavu katika kupigania haki na vita dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

"Tazama Winnie Mandela alikuwa mpambanaji hata kabla ya kuwa mke wa Rais Nelson Mandela, kwa hiyo tukiangalia historia yake tunabaini kuwa hakuhitaji msukumo wa nguvu za mwanaume katika kuonyesha ushupavu wake", alisema.

Alisema Winnie Mandela aliyefariki dunia Aprili 2, mwaka huu, aliendelea kuonyesha ushupavu wake katika kupambana na udhalimu na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini hata wakati Mandela akiwa gerezani

"Winnie atakumbukwa na Watanzania na dunia nzima kwa ujasiri wake pia atakumbukuwa kwa umaarufu alioupata hata akiwa bado mwanafunzi, msichana kabla ya kuolewa. Alichukia kuona Mwafrika anabaguliwa, anatengwa asifike kwenye maeneo walipokuwa weupe. Kwa hiyo umaarufu wa Winnie haukutokana tu kwa kuwa ni mke wa Rais yaani “First lady “ lakini umarufu wake ulikuwa wa kwake mwenyewe. Alijitambua, akajiamini, akatimiza wajibu wake kama Binadamu, kama Mwafrika, baadaye kama Mke, Mama, Mwanasiasa na Kiongozi" alisema Gaundetia 

"Wanawake wa Tanzania hasa wanasiasa tuna mengi ya kujivunia na kujifunza kutoka kwa mwana mama huyu mtoto wa Afrika. Tumejifunza kuishi sisi wenyewe na sio kutegemea tufanyiwe, tupendelewe ndipo tuonekane tunaweza. 

Tunatambua uwezo tulionao wanawake lakini pia tuwe wastahimilivu tunapokumbana na magumu tupambane hadi mwisho. Kama Winnie Madikizela Mandela aliweza kutetea Waafrika wenzake hata baada ya mume wake kufungwa; kwa sababu hiyo kwa nini sisi wengine tusiweze kujitokeza waziwazi na kuiunga Serikali na Rais wetu Dk. John Magufuli katika juhudi zake za kupiga vita ufisadi, wizi wa mali ya umma, kutowajibika", Alisema Gaudentia. 

"Wanawake wa Tanzania na wa Afrika nzima tunapomlilia Winnie Mandela kwa nini tusiige ujasiri wake kwa kukemea bila woga tabia mbaya kama mahusiano ya jinsia moja, ubakaji na utumiaji dawa ya kulevya, katika jamii yetu. Wanawake wa Tanzania tumapomlilia Winnie Mandela kwanini tusijitokeze waziwazi kupinga mfumo dume unaoendelea kwenye baadhi ya maeneo hapa nchini kwetu na kusababisha kina mama kutojiamini", alisema.

Alisema, kama Winnie Mandela alivyotimiza wajibu wake katika harakati za Waafrika kuing’oa Serikali dhalimu ya kibaguzi nchini Afrika kwa nafasi yake kama mwanamama, na wanawake wa Tanzania  kila mmoja kwa nafasi yake wanaweza kuwa chachu ya kuleta mabadiliko ya kweli hapa nchini.

"Tunafahamu kuna wanawake wa nchi yetu ambao wameonyesha ujasiri  kama huo wa Winnie Mandela wakiiwakilisha nchi yetu Kimataifa. Sisi UWT tunajiandaa kuwatambua hivi karibuni, nia yetu ni kutambua michango yao wakiwa wanafanya kazi nje ya nchi yetu na hivyo wametuleta sifa wanawake wa Tanzania, lakini pia kuwatia moyo wengine watimize wajibu wao, Alisema Gaudentia.", alisema Gaudentia.

Akizungumzia mrejesho wa ziara aliyoifanya hivi karibuni aliwapongeza wanawake wanaowajibika ipasavyo Mijini na Vijijini hapa nchini akisema yeye na timu yake walitembelea Mikoa na Wilaya zote za Kanda ya Nyanda ya Juu Kusini na kubaini kuwa wanawake ni wajasiriamali wazuri, ni wakopaji na walipaji wazuri na kuzitaka Halmashauri kuwapa mikopo wanawake hao ili wapanue shughuli zao za ujasiriamali na kwamba hicho ndicho kilio chao kikubwa, akihimiza halmashauri hizo kutenga asilimia kumi ya mapato ya ndani.

"Tunapenda ifahamike kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Mwelekeo wa Sera zake kwa Mwaka 2010 - 2020 na Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015-2020 kwa pamoja zimeweka msisitizo wa kuyawezesha makundi Maalum ikiwemo Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu na katika kutekeleza maelekezo CCM, Serikali imeshatoa Maelekezo kwa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Wilaya na Miji Midogo kutenga asilimia kumi za makusanyo yao ya ndani kwa ajili ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu Alisema Gaudentia na kungeza;

"Tunapenda kuwakumbusha wale wote wenye dhamana katika Mamlaka hizi kwamba ni Maelekezo ya CCM kutoa bila kukosa fedha hizi ili kuwawezesha wananchi katika makundi haya muhimu. Kuanzia sasa UWT itafuatilia kwa ukaribu suala hili na hatutasita kupendekeza kwa Mamlaka za uteuzi kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa wale wote wanaosuasua au kutenga kutoa fedha hizi ili kujihakikishia kuwa wanawake hawa wachapakazi wapate mahali pa kupata mikopo kwa bei nafuu kwa maana ya riba nafuu".

"Tunawaomba Maafisa Maendeleo ya Jamii watimize wajibu wao wa kutembelea vikundi vya wakina mama ili kuwapatia elimu ya kujisajili, Kuendesha shughuli zao, Kupata mikopo ya Halmashauri,  Kupata mikopo kutoka benki kwa wale watakaoweza. Tunawapongeza Wakurugenzi na Maafisa wa Maendeleo ya Jamii ambao tulikuta wanatimiza wajibu wao kikamilifu, kwa mfano, Mkurugenzi wa Maendeleo Halmashauri ya Chunya ambayo inaongozwa na Wanawake (Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri, Afisa Maendeleo ya Jamii) ndiyo Halmashauri ya mfano kwa kutenga asilimia kwa wanawake, pia Halmashauri ya Njombe (V) inaongozwa na Mwanamke na ina fanya vizuri ikifuatiwa na Halmashauri ya Mufindi", alisema Daudentia.

Kuhusu Maadili, Gadentia alisema UWT wataendelea kukemea maadili yaliyoporomoka kwa vijana wa kike na wa kiume jambo ambalo ni hatari kwa kizazi kijacho na kuhumiza wazazi na walimu kukemea uvunjaji wa Maadili na hasa mimba za utotoni.

"UWT inashauri kwenye maeneo tunakoishi ambako kuna Kamati mbalimbali kama vile polisi jamii na nyingine, Jamii iongeze Kamati ya za Maadili zitakazosimamia maadili kwa vijana wa kike na wa kiume kwa kila Kata, ambazo zitakuwa na wajumbe wafuatao, Viongozi wa Dini zote, Madiwani wa Kata na Viti Maalum, Wazee na watu wazima wanaoishi ndani ya Kata hizo, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata. Kamati hizo zisimamie kikamilifu zoezi hilo na viongozi waliotajwa hapo juu na ikibidi watakaokiuka wachukuliwe hatua za kinidhamu kama wahalifu wengine", alisema Gaudentia 

Alisema, baada ya kukamilisha ziara hiyo UWT iliandaa Mafunzo ya kuwajengea uwezo na uelewa wa pamoja Viongozi na Watendaji wa UWT wa ngazi ya Wilaya na Mikoa hiyo ya Nyanda za Juu Kusini. Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 26 – 27/03/2018 katika Mkoa wa Mbeya na kwamba ziara na mafunzo haya yataendelea kufanyika katika Mikoa yote.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช