.

UWT WATOA TUZO ZA MWANAMKE WA MFANO 2018, DAR NA KUZINDUA KWA KISHINDO SIKU YA MWANAMKE WA MFANO TANZANIA AMBAYO ITAKUA IKIFANYIKA KILA MWAKA

Apr 29, 2018

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akimpongeza Mke wa Rais Mstaafu Mama Salma Kikwete, wakati akimkabidhi tuzo ya 'Mwanamke wa Mfano Tanzania 2018', katika hafla ya Uzinduzi wa 'Siku ya Mwanamke wa Mfano Tanzania', katika Ukumbi wa PTA, Temeke Dar es Salaam, jana. Kushoto ni katibu Mkuu wa UWT Amina Makilagi.
Na Bashir Nkoromo
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema Wanawake walikuwa na mchango mkubwa katika harakati za kufanikisha kupatikana kwa Uhuru wa Tanzania.

Makamu wa Rais ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa Siku ya Mwanamke wa Mfano Tanzania iliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ikiambatana na Jumuiya hiyo kutoa Tuzo ya Mwanamke wa Mfano 2018, ambapo jumla ya Wanawake 26 walipewa tuzo hizo.

Makamu wa Rais alisema ni dhahiri kuwa wanawake walikuwa na mchango mkubwa sana. Walifanya kazi kubwa katika uhamasishaji, malezi ya watoto na vijana na kusimama bega kwa bega na kuunga mkono wanaume waliokuwa mstari wa mbele katika mapambano hayo ya kuleta Uhuru.

Alisema, walifanya mengi nyuma ya pazia ambayo yalikuwa na mchango mkubwa katika Taifa, na kwamba walisukumwa na mapenzi yao, subira mbali na mchango wao wa hali na mali ndio uliowapa nafasi wanaume kufanikisha harakati za uhuru kwa kuwa wanawake waliwapa wepesi kwa kuwapunguzia mzigo mzito uliokuwa mabegani mwao na kuwa haiyumkini, katika ngao ya Taifa la Tanzania, ikatambua nafasi ya mwanamke kwa kuwekwa sambamba na mwanaume. 

Makamu wa Rais alisema kutokana na kazi kubwa ya wanawake jasiri na mashujaa waliotangulia, hadi sasa wanawake wameendelea kutoa mchango mkubwa katika uongozi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. 

Makamu wa Rais alitoa mwito kwa Wanawake na kuwa Tuzo za “Mwanamke wa Mfano Tanzania” ziwe chachu yetu Wanawake katika kuchapa kazi, kuungana, kushikamana katika kuleta maendeleo miongoni ya nchi na jamii nzima ya Watanzania. 

"Sisi wanawake ni nusu ya watu wote nchini, tukijiongeza tukaendelea, kaya zetu zinaendelea na hatimaye nchi inaendelea" alisema Makamu wa Rais. 

Makamu wa Rais aliwataka Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) kuchukua jukumu la kuwasemea, kuwatetea na kuwaunganisha wanawake wote wa Tanzania wana CCM, wasio wana CCM na wasio na vyama akisema ndiyo wajibu wa UWT iliopewa na Katiba ya CCM. " Katika nchi yetu, hamna chombo chochote kikubwa cha kuwaunganisha wanawake isipokuwa ninyi. Nawakumbusha kuwa nanyi mnatazamwa na wanawake wa nchi yetu", alisema Makamu wa Rais.

Katika uzinduzi huo ulioongozwa na viongozi na baadhi ya waasisikaribu wote wa UWT chini ya Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudentia Kabaka na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Amina Makilagi walihudhuria viongozi mbalimbali wakiwemo wake wa Marais wastaafu wa Tanzania na Zanzibar.
 Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, akizungumza na Katibu Mkuu wa UWT Amina Makilagi baada ya kuwasili ukumbini, katika hafla ya uzinduzi wa Siku ya Mwanamke wa Mfano Tanzania, katika Ukumbi wa PTA, Temeke Dar es Salaam, jana. Kwa matukio mbalimbali ya tukio hili la kihistoria endelea kuangalia picha zifuatazo:-

Viongozi wa UWT na waalikwa mbalimbali wakishangilia mwishoni mwa hafla hiyo ya uzinduzi wa Siku ya Mwanamke wa Mfano Tanzania, jana katika Ukumbi wa PTA, Temeke Dar es Salaam. Kushoto ni katibu Mkuu wa UWT Amina Makilagi. PICHA ZOTE NA BASHIR NKOROMO

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช