Breaking News

Your Ad Spot

Apr 11, 2018

WAZIRi MPINA AWABANA WANAOTOROSHA PUNDA NJE YA NCHI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina  akiangalia zizi la Punda na Mkurugenzi wa Kiwanda  cha kuchinjia Punda  Fang Hua, Lifang Yu aliye kushoto kwake. Picha  na John Mapepele.
Na John Mapepele, Shinyanga
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amewahakikishia wenye viwanda nchini kuwa hakuna mali ya mifugo ya Tanzania itakayotoroshwa  tena kwenda nje ya nchi kimagendo kwani Tanzania haiwezi kukubali kugeuzwa kuwa machungio ya mifugo hiyo.

Waziri Mpina ametoa kauli hiyo jana mjini Shinyanga baada ya kutembelea Kiwanda cha Fang Hua kinachojishughulisha na uchinjaji wa Punda ambapo alielezea kuridhishwa kwake na juhudi kubwa zilizofanywa na mwekezaji huyo kuwezesha kuwepo soko la uhakika la mifugo hiyo.

Mkurugenzi wa Kiwanda  cha Fang Hua, Lifang Yu alimweleza Waziri Mpina kwamba  kiwanda chake  kimeshaingia  ubia na  wafugaji wadogo wapatao 27  ili kuongeza uzalishaji ambapo kinatarajia kuwashilikisha wafugaji wengi zaidi katika mikoa mbalimbali nchini

Waziri Mpina aliwahakikishia wawekezaji wenye viwanda katika sekta ya mifugo kuwa malighafi hiyo itakuwepo ya kutosha kwani Serikali ya awamu ya tano chini ya Dk. John Pombe Magufuli haitakubali tena mifugo hiyo kuendelea kutoroshwa nje ya nchi na kunufaisha viwanda vya nchi hizo.

Hivyo Waziri Mpina alisema uwekezaji wa aina hiyo wa kuongeza thamani ya mazao ya mifugo ni moja ya vipaumbele vya wizara yake kwa sasa ili kuchochea kwa kasi kufanikisha azma ya Tanzania ya viwanda.
Alisema kiwanda hicho mbali na kuongeza soko la punda pia kimechangia kuchochea uchumi wa Mkoa wa Shinyanga pamoja na kutatua changamoto ya ajira ambapo hadi sasa kimeajiri wafanyakazi 100 hivyo alimhakikishia mwekezaji huyo kuwa changamoto ya punda wengi kutoroshwa nchini Kenya haitakuwepo tena.

Alisema kwa sasa  kuna viwanda  viwili vya kuchakata nyama ya punda na kuuza nchini China, ambapo wastani wa mauzo ya nyama hiyo nje ya nchi yalifikia tani 2000 mwaka 216/17.

Mpina aliwahimiza wawekezaji hao kuhakikisha wanawasaidia  wafugaji katika kuongeza uzalishaji, kupambana  na maradhi, upatikanaji wa maji na malisho kwa mifugo.
Aliwataka kuanzisha ranchi ya mifugo na maeneo yakupumzishia  mifugo hiyo kabla ya kuchinjwa.

 Alisema idadi ya punda waliopo nchini ni 520,000 tu hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kuongeza uzalishaji.

Kaimu Mkurugenzi wa  Uzalishaji Mifugo na Masoko wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Lovince Assimwe  aliwataka  wafugaji kuongeza soko la uhakika.

Alipongeza  uongozi wa kiwanda hicho kwa kubuni mbinu za kuwasaidia  wafugaji kwa kuwapatia  shilingi  elfu tano kila  mwezi kwa ajili ya  matibabu ya punda.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages