.

RAIS DK. MAGUFULI AAGIZA UCHUNGUZI UFANYIKE MRADI WA UJENZI WA UKUMBI WA MIHADHARA MUCE

May 3, 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameviagiza vyombo vya dola, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuchunguza mradi wa ujenzi wa jengo la ukumbi wa mihadhara na ofisi za Wahadhiri katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kilichopo katika Manispaa ya Iringa.

Mhe. Rais Magufuli ambaye alisoma chuoni hapo wakati ikiwa shule ya sekondari ya Mkwawa, ametoa agizo hilo leo tarehe 02 Mei, 2018 alipotembelea chuo hicho na kuzungumza na wanafunzi na Wahadhiri katika uwanja wa michezo.

Ujenzi wa jengo la ukumbi wa mihadhara na ofisi za Wahadhiri ulianza mwaka 2010 na tayari Serikali imeshatoa Shilingi Bilioni 8 na Milioni 804, lakini ujenzi wake bado haujakamilika.

Mhe. Rais Magufuli pia ameagiza vyombo vinavyohusika vifuatilie kesi iliyofunguliwa dhidi ya Mkandarasi aliyekuwa akijenga majengo hayo.

Katika Mkutano wake na wanafunzi wa MUCE Rais Magufuli amesikiliza kero zao mbalimbali zikiwemo zinazohusumikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na mazingira ya kusomea, ambapo amewaeleza kuwa Serikali imekuwa ikiongeza fedha za mikopo na kuwakopesha wanafunzi wengi zaidi lakini akasisitiza kuwa sasa haitaweza kutoa mikopo kwa wanafunzi wote wa vyuo vikuu.

“Nataka niwahakikishie Serikali ya Awamu ya Tano inawapenda wanafunzi wa vyuo vikuu, lakini lazima niwaambie ukweli Serikali haiwezi kutoa mikopo kwa wanafunzi wote” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha Mhe. Rais Magufuli ameagiza Wakala wa Barabara Mkoani Iringa (TANROADS) kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara ya kuingia chuoni hapo ili ijengwe kwa kiwango cha lami.
Akisoma taarifa kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho kinakisimamia Chuo Kikuu cha MUCE, Prof. Bonaventure Rutibwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutembelea UDSM na kukijengea mabweni yanayochukua wanafunzi 4,000 katika kampasi ya Mwl. J.K Nyerere Mlimani Jijini Dar es Salaam ambayo yamepewa jina la “Hosteli za Dkt. John Pombe Magufuli”

Naye Rasi wa MUCE Prof. Esther Dungumaro ameseam chuo hicho kilichoanza mwaka 2005 kimezalisha walimu 7,090 wenye shahada ya kwanza na shahada ya uzamili na kwamba katika mwaka huu kitazalisha walimu 1,365 wakiwemo 641 wa masomo ya sayansi.

Katika ziara hiyo Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Charles Mwijage.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช