ALIYEKUWA Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Haji Manara akiwa achini ya ulinzi wa Polisi alipofikishwa katika mahakama ya Kinondoni, jana kwa tuhuma za utapeli. (Picha na Emmanuel Ndege).
Stori Kamili
ALIYEKUWA Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Haji Manara (35), jana alipandishwa kizimbani kujibu mashitaka ya wizi wa magari na kujipatia mamilioni ya fedha kwa njia ya udanganyifu.
Manara alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, ambapo umati wa watu ulifurika, wakiwemo ndugu zake ambao walionekana kulengwa na machozi, baada ya mshitakiwa huyo kurudishwa rumande.Mtuhumiwa huyo, ambaye aliamua kujiuzulu wadhifa huo, kutokana na tuhuma hizo za utapeli wa magari, alisomewa mashitaka sita na kurudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Alisomewa mashitaka hayo na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Batseba Kasanga, mbele ya Hakimu Benadicta Beda. Batseba alidai Novemba 27 mwaka jana, eneo la Magomeni, wilaya ya Kinondoni, aliiba gari aina ya Toyota OPA, lenye namba za usajili T 527 AVB, alilolichukua kutoka kwa Abdul Ngalawa kwa madai kwamba angeenda kuliuza kwa sh. milioni 10 na kumrudishia fedha hizo, lakini alitumia kwa matumizi yake binafsi.
Pia anadaiwa Desemba 19 mwaka jana, eneo hilo la Magomeni, kwa njia ya udanganyifu alijipatia magari mawili yenye namba T 866 BEB aina ya Toyota IPSAM lenye thamani ya sh. milioni 14 na T 746 AVU aina ya Toyota NADIA lenye thamani ya sh. milioni 12 mali ya Asma Miraji, baada ya kujifanya kwamba atamrudishia magari hayo baada ya siku 10, jambo ambalo siyo la kweli.
Januari 5 mwaka huu, eneo la Kinondoni, Manara anadaiwa kwa nia ya udanganyifu alijipatia sh. milioni 5 mali ya Jacob Manyanga, kwa madai ya kwamba atamuuzia gari huku akijua si kweli.
Katika shitaka lingine, Manara anadaiwa Desemba 20 mwaka jana, eneo la Magomeni kwa nia ya udanganyifu alijipatia sh. milioni tatu mali ya Wilson Matimba, kwa madai kwamba atamuuzia gari huku akijua si kweli.
Manara pia anadaiwa Januari 29 mwaka huu, saa 11.00 jioni, eneo la Magomeni, wilaya ya Kinondoni, kwa nia udanganyifu alijipatia sh. milioni 1.9 kutoka kwa Dotto Hussein, baada ya kujitambulisha kuwa ni mfanyabiashara na kwamba atamrudishia fedha hizo baada ya siku tano.
Shitaka lingine, Manara anadaiwa Januari 13 mwaka huu, saa 2.00 usiku, eneo la Magomeni, kwa nia ya udanganyifu alijipatia sh. milioni 3.6 kutoka kwa Fadhil Kassim baada ya kujifanya ni mfanyabiashara na kwamba atamrudishia fedha hizo baada ya siku tano.
Manara alikana mashitaka. Upande wa Mashitaka ulidai upelelezi haujakamilika na kwamba hauna kipingamizi kuhusu dhamana. Hakimu Benadicta alitaja masharti ya dhamana kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria ambao wanapaswa kuweka hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya sh. milioni 35 au kutoa fedha taslim sh. milioni 17.
Hata hivyo, Manara alishindwa kutimiza masharti hayo, ambapo alirudishwa rumande hadi Machi 4, mwaka huu, kesi itakapotajwa.
Manara alipandishwa kizimbani saa 7.30 mchana, na kusomewa mashitaka katika chumba cha mahakama ‘chemba’, hali iliyofanya polisi kuwatoa baadhi ya watu baada ya chumba hicho kujaa.
Hata hivyo, ndugu na jamaa wa Manara aliyeonekana kujiamini, walikuwa wakiwazuia wapigapicha kumpiga picha, jambo ambalo mshitakiwa huyo alitaka kuwaacha watekeleze jukumu lao.
Mahakamani hapo, jana watu wanaodai kutapeliwa na Manara magari yao na kutoingizwa katika hati ya mashitaka, walidai wataenda kituoni kufungua mashitaka.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269