Kijana Alex
BAADA ya washiriki wa shindano la ‘Maisha Plus Season II’ kuishi kijijini kwa siku 56, hatimaye juzi usiku mshiriki Alex Lubinza kutoka Mbeya ametangazwa kuwa mshindi wa shindano hilo..
Hatua imemfanya mshiriki huyo kuondoka na kitita cha sh. Milioni 15 kama zawadi yake kutokana na ushindi huo alioupaya baada ya kupata kura nyingi kuliko washiriki wenzake 10 walioingia fainali ya shindani hilo.
Shamrashamra za fainali hiyo zilianza saa 10 jioni hadi saa sita usiku pale mshindi alipotangazwa ambapo mandhari ya kijiji nayo pia yalionekana kuwa tofauti na siku nyinginezo ambapo washiriki Mwinshehe, Alex, Neema wa Shinyanga, Leonald walionekana wakifanya vituko ambavyo walikuwa wanaviita vya mara ya mwisho kufanywa.
Ilipofika usiku, washiriki nane waliobakia kijijini baada ya washiriki wawili Jackline na Taiba kutolewa kijijini kutokana na utovu wa nidhamu walionekana kuwa na wasiwasi hasa pale ya kutojua nani atatoka, ingawa burudani nazo zilikuwa zinaendelea kwa kasi kijijini.
Hali ambayo ilimfanya Msemaji wa kijiji, Masoud Kipanya kuwakaribisha kikundi cha ngoma cha Frolida kuja uwanjani kutoa burudani ya ngoma za kiasili. Jambo ambalo lilionekana kumpa ‘mzuka’ Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga kuingia uwanjani na kuanza kutibwirika pamoja na wasanii wa kikundi hicho.
Kutibwirika huko kuliwafanya wageni wengine waliowasili kijijini, Mbunge wa Viti Maalumu, Janeth Massaburi na Mbunge wa Kinondoni, Idd Azan kuingia kati nao na kuanza kucheza ngoma hizo za asili zilizoanza kuchezwa na washiriki, wasanii wa kikundi hicho tangu mchana.
Baada ya burudani ya ngoma kumalizika, pia kulikuwepo na burudani ya muziki wa Bongo Fleva kutoka kwa mwanamuziki Diamond huku Afande Selle na Madee nao kuingia kijijini na kutamka bayana kuwa ni marafiki na hawana ugomvi kabla ya kuanza ‘kushusha’ mistari.
Kabla ya mshindi hajatangazwa, washiriki walisoma risala kwa kwa Mgeni Rasmi ambapo waliweza kutanabainisha vitu vingi wanavyotaka kuvifanya baadae ikiwemo uanzishwaji wa ‘Foundation’ ya Maisha Plus, Upataji wa Ofisi pamoja na kazi watakazofanya za kusaidia jamii ikiwemo kufanya usafi kwenye mahospitali na kutoa misaada kwa jamii.
Risala hiyo ilionekana kumkuna mgeni rasmi ambaye aliwaahidi kuwapatia ofisi pamoja na kukubali kuwa Bibi na Mwanachama wa shindano lijalo hasa pale Babu alipompa kibuyu cha kuthamini mchango wake juu ya shindano hilo na yeye kutamka hakuna shaka.
Baada ya muda ulifika, Babu aliitwa kwa ajili ya kuwatoa washiriki saba kabla ya kuja tena kumtoa mshiriki mmoja, Luhende na kuwafanya kubakia washiriki wawili Neema wa Shinyanga na Alex na kumpa bahasha yenye jina mmoja mgeni rasmi ambaye muda mwingi alionekana yupo kwenye tabasamu nzito na baadae kutamka rasmi kuwa mshindi wa shindano hilo kwa mwaka huu ni ALEX na kupewa ‘cheque’ yake ya sh. Milioni 15 kutoka Infinity.
Kutamkwa kwa jina hilo kulimfanya Alex kukimbia na kuanguka chini huku akiwa amini kilichotokea kuwa ni yeye ndiye ni mshindi wa shindano kwa mwaka huu kabla ya kuwashukuru watu wote waliofanikiwa kumsaidia kushinda na kuahidi kutoa sh. Laki mbili kwa washiriki wenzake walioingia fainali.
Hata hivyo, haijaweza kujulikana kuwa kiasi hicho cha pesa atakigawa pia kwa washiriki wenzake wawili, Jackline na Taiba waliotimuliwa kijijini, hivyo kuchukua kwa Alex kumefanya tangu kuanzishwa kwa shindano hilo washiriki wa kiume wameonekana kung’ara baada ya Maisha Plus ya kwanza kuchukuliwa na Abdul kutoka Zanzibar ambaye alichukua kitita cha sh. Milioni 10.
Wanaenda Ngorongoro
BAADA ya kumalizika kwa shindano la ‘Maisha Plus Season II’, washiriki nane leo wanaenda kwenye hifadhi za wanyama za Ngorongoro kujionea mambo ya utalii.
Ofa hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Maliasili na Utalili, Shamsa Mwangunga katika kutimiza ahadi yake aliyowapa washiriki hao siku nne kabla ya shindano halijamalizika.
Waziri Mwangunga baada ya kutamka kauli hiyo kuliwafanya washiriki kuripuka kwa shangwe na kuanza kuimba ‘Mama… Mama”, ikiwa ni ishara ya kumpongeza kutokana na ahadi yake aliyowapa.
Kwa upande wake, Mbunge Janeth Massaburi naye alitoa ahadi kwa washiriki 18 walioshiriki shindano hilo kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali utengenezaji wa zao la Uyoga na chaki.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269