Breaking News

Your Ad Spot

Mar 2, 2010

HOTUBA YA RAIS JAKAYA KIKWETE KWA WANANCHI MWISHO WA MWEZI FEBRUARI, 2010

RAIS JAKAYA KIKWETE

Ndugu Wananchi, Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kukutana kwa mara nyingine tena na kuzungumza kwa mujibu wa utaratibu wetu mzuri wa kuzungumza kila mwisho wa mwezi.
     Mwisho wa mwezi uliopita hatukuweza kuzungumza kwa sababu nilikuwa Addis Ababa, Ethiopia kwenye mkutano wa kila mwaka wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika. Hata hivyo niliitumia fursa ya hotuba yangu katika Sherehe za Miaka 33 ya CCM tarehe 6 Februari, 2010 kuzungumzia baadhi ya masuala muhimu kitaifa.
    Siku ya leo nataka kuzungumzia jambo moja tu, nalo ni Muswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi uliopitishwa na Bunge letu tukufu katika kikao chake kilichopita. Hivi karibuni nitatia saini muswada huo kuwa Sheria.
     Kwa sasa matayarisho ya shughuli hiyo yanaendelea. Ndugu Wananchi; Chimbuko la kutungwa sheria hii ni mwenendo usiyoridhisha wa matumizi ya fedha katika chaguzi zetu nchini. Kuna matumizi mabaya ya fedha katika uchaguzi ndani ya vyama vya siasa na baina ya vyama vya siasa katika chaguzi za kiserikali.
      Katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge tarehe 30 Desemba, 2005, nilizungumzia kutokuridhishwa kwangu na hali hii na nilielezea nia yangu ya dhati ya kutaka kuchukua hatua thabiti za kuweka utaratibu utakaoongoza na kudhibiti matumizi ya fedha katika uchaguzi. Naomba ninukuu maneno niliyosema siku ile: “Jambo lingine linalonisumbua linahusu upatikanaji na matumizi ya fedha na michango mingine kwenye Uchaguzi.
    Yanaweza kujitokeza mawazo, pamoja na kuanza kujengeka utamaduni kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha. [............] tusipokuwa waangalifu nchi yetu inaweza kuwekwa rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo.
      Ni kweli kwamba fedha ni nyenzo mojawapo muhimu katika kufanikisha uchaguzi, kwa kila chama na kwa kila mgombea. Lakini, fedha kutumika kununua ushindi si halali. Kwa maoni yangu hatuna budi kupiga vita utamaduni huu kwa nguvu zetu zote. Ni vema sasa tuanzishe mjadala wa kitaifa na hatimaye kuelewana kuhusu utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutafuta fedha za uchaguzi; na utaratibu halali ulio wazi, wa chama au mgombea kutumia fedha hizo. Na utaratibu tutakaokubaliana uwe ni sehemu ya maadili ya uchaguzi katika uchaguzi wa kiSerikali na ndani ya vyama vya Siasa.” Mwisho wa kunukuu.
      Ndugu wananchi, Jambo hili tumekuwa tunalifanyia kazi Serikalini tangu tuingie madarakani. Kwa vile ni jambo jipya na kwa nia ya kuepuka kuanza vibaya, tumefanya utafiti wa kutosha na kujifunza kutoka mifano ya nchi ambazo zina utaratibu wa aina hii. Kadhalika, hapa nchini, tuliwahusisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, asasi zisizo za kiserikali, Tume ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama vya Siasa na watu wengine wengi.
     Ndugu Wananchi; Matokeo ya kazi hiyo nzuri ni kutengenezwa kwa Muswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi ambao uliwasilishwa katika kikao kilichopita cha Bunge kwa uamuzi. Kabla ya kupelekwa Bungeni, rasimu ya Muswada huu ilijadiliwa kwa kina Serikalini.
     Dodoma Bungeni, muswada huu ulijadiliwa kwa siku kadhaa katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na kwenye vikao vya Kamati za Vyama vya Siasa. Katika jamii nako, Muswada huu uliibua mijadala iliyokuwa na hisia za namna mbalimbali na wakati mwingine mijadala hiyo ilikuwa mikali. Kwa ujumla, mijadala yote hiyo ilisaidia kuboresha maudhui ya Muswada na hatimaye kupata ule uliopitishwa na Bunge letu Tukufu tarehe 11 Februari, 2010.
    Ndugu Wananchi; Tumetunga Sheria hii mpya kwa nia ya kupata majawabu kwa tatizo la matumizi mabaya ya fedha katika shughuli za uchaguzi. Tunatambua kuwa matatizo haya si mageni, yamekuwepo tangu miaka mingi huko nyuma na hata historia ya Bunge letu ina ushahidi wa ushindi wa baadhi ya Wabunge kutenguliwa kwa makosa ya rushwa. Lakini, siku hizi matatizo ya matumizi mabaya ya fedha yamekuwa makubwa zaidi na yanakua kwa kasi inayotishia kugeuzwa kuwa ndiyo utaratibu wa kawaida au utamaduni katika chaguzi zetu. Ni hali ambayo haifai kuachwa kuendelea na kuzoeleka. Hatuna budi kuchukua hatua za dhati kurekebisha mambo na kulirejesha taifa katika mstari ulionyooka.
      Ndugu Wananchi; Tuliamua kuwa, hatua muafaka ya kuchukua ni hii ya kutunga sheria ya kuongoza na kudhibiti matumizi ya fedha katika uchaguzi. Sheria hii ikitekelezwa ipasavyo itazuia kugeuza uongozi kuwa ni kitu cha kununuliwa kama bidhaa na wenye pesa au wanaoweza kupata pesa za kufanya hivyo. Aidha, itakomesha kabisa tabia mbaya inayoanza kujitokeza ya wapiga kura kugeuza kura yao kama bidhaa ya kuchuuza kwa wagombea.

Misingi ya Sheri
Ndugu Wananchi, Katika kufikiria na kutayarisha rasimu ya muswada wa sheria hii, mambo saba ya msingi yalizingatiwa. Mambo hayo ni haya yafuatayo: Kuutambua kisheria mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya vyama vya siasa na kuusimamia kisheria. Kuweka utaratibu wa kisheria utakaosimamia na kuratibu mapato na kudhibiti matumizi pamoja na gharama za uchaguzi kwa vyama vya siasa na wagombea. Kuweka viwango kwa matumizi na gharama za uchaguzi.
     Katika utaratibu utakaosimamia mapato na matumizi ya vyama vya siasa ikiwa ni pamoja na zawadi, misaada na michango itakayotolewa na wagombea au wahisani wakati wa kampeni za uchaguzi. Kudhibiti michango na zawadi kutoka nje ya nchi.
     Kuweka utaratibu na mfumo wa udhibiti na uwajibikaji kwa mapato na matumizi ya fedha za uchaguzi kwa upande wa vyama vya siasa na wagombea. Kuainisha adhabu kwa watakaokiuka masharti yatakayowekwa na Sheria hii. Uteuzi Ndani ya Vyama Umetambuliwa
    Ndugu Wananchi, Katika Sheria ya Gharama za Uchaguzi, mambo yote hayo ya msingi yamezingatiwa. Ni Sheria inayojitosheleza kwa kila hali pamoja na ukweli kwamba ni mara ya kwanza tunakuwa na sheria ya namna hii. Sheria yetu mpya imezitambua rasmi gharama zinazotumika na vyama vya siasa na wagombea kuanzia wakati wa mchakato wa uteuzi ndani ya vyama mpaka wakati wa uchaguzi wenyewe.
    Sheria hii sasa inafafanua gharama za uchaguzi kuwa ni zile zinazotumika na Vyama, Wagombea au Serikali wakati wa uteuzi ndani ya vyama, wakati wa uteuzi kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, wakati wa kampeni na hadi siku ya kupiga kura.
   Ndugu Wananchi; Kabla ya Sheria hii kutungwa, matumizi mabaya ya fedha wakati wa uteuzi wa wagombea katika vyama vya siasa yalionekana kuwa ni matatizo ya ndani ya vyama husika, hivyo yaliachiwa vyama vyenyewe kushughulika nayo wajuavyo. Kwa mujibu wa Sheria yetu mpya mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya vyama umetambuliwa rasmi kuwa ni sehemu kamili ya uchaguzi, hivyo matumizi ya fedha ya vyama na wagombea yametengezewa utaratibu wa udhibiti.
       Kwa hiyo, kuanzia sasa kuhonga au kuhongwa katika mchakato wa uteuzi ndani ya vyama kutamulikwa kwa karibu na wahusika wataadhibiwa na vyombo vya dola.

Uwazi wa Mapato na Matumizi
Ndugu Wananchi; Jambo lingine muhimu katika Sheria hii ni kwamba, inaweka sharti la uwazi katika mapato na matumizi ya vyama na wagombea kwa ajili ya uchaguzi kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Sheria pia inaelekeza utaratibu wa kufuatwa na vyama na wagombea katika kutoa taarifa zao za mapato na matumizi ya uchaguzi.
     Kila mgombea, kwa mfano, atatakiwa kutoa kabla ya uchaguzi, taarifa ya fedha alizonazo na makisio ya fedha anazotarajia kupata kwa ajili ya kampeni na uchaguzi, ndani ya siku saba (7) baada ya uteuzi wa wagombea kufanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
    Baada ya uchaguzi atatakiwa kutoa taarifa ya mapato na matumizi halisi siku tisini (90) baada ya matokeo kutangazwa. Ndugu Wananchi; Vyama vya siasa, navyo hali kadhalika, vitatakiwa kutoa taarifa ya mapato yao pamoja na makisio ya mapato wanayotegemea kuyapata kwa ajili ya gharama za uchaguzi kabla ya uteuzi wa wagombea.
      Baada ya uchaguzi, vyama hivyo vinatakiwa vitoe taarifa ya mapato na matumizi yake halisi ndani ya siku tisini (90) baada ya matokeo rasmi ya uchaguzi kutangazwa.
     Taarifa hizo za vyama na wagombea zinatakiwa zionyeshe wazi vyanzo vyote vya mapato ikiwemo michango ya fedha na mali (vifaa, zana, magari n.k.), pamoja na mchanganuo wa matumizi yake. Uwazi wa Michango Ndugu Wananchi, Kwa upande wa michango ya hiyari na zawadi zinazotolewa kwa Chama na wagombea, Sheria inataka pawepo na uwazi katika utoaji wake.
     Sheria inaelekeza kwamba, kila chama cha siasa kilichopokea mchango unaozidi shilingi milioni moja kutoka kwa kila mchangiaji binafsi au shilingi milioni mbili kutoka kwa taasisi, kitoe taarifa kwa Msajili.
    Aidha, Sheria inataka fedha hizo zihifadhiwe katika akaunti maalum itakayofunguliwa kwa ajili hiyo. Fedha hizo zitalipwa na kutumika kutoka katika akaunti hiyo. Naomba ieleweke kuwa, si nia ya Sheria hii kuzuia wananchi kuchangia shughuli za siasa au za kampeni za Chama wakipendacho au mgombea wanayempenda. Sheria inaruhusu michango ya aina yoyote kutolewa kwa chama chochote au kwa mgombea yeyote ila inataka michango hiyo itolewe kwa utaratibu ulio wazi. Kusiwe na usiri au kificho cha namna yoyote.
      Ndugu Wananchi; Sheria pia inafafanua utaratibu wa vyama au wagombea kupata misaada kutoka nje ya nchi. Sheria inazuia michango na misaada hii isitolewe wakati wa kampeni. Inaruhusu vyama vya siasa au wagombea kupokea misaada kutoka nje ya nchi siku 90 kabla ya Uchaguzi Mkuu au siku 30 kabla ya uchaguzi mdogo.
        Pia, inataka kuwepo uwazi na taarifa itolewe kwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Najua suala la masharti yaliyowekwa kwa watu wa nje kuchangia vyama vya siasa na wagombea nchini lilizua mjadala miongoni mwa wadau mbalimbali. Kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa kupinga masharti yaliyowekwa. Naomba ieleweke kuwa, kwa kweli, si jambo jema kwa Chama cha siasa au mgombea nchini kufadhiliwa na watu wa nje. Wahenga wanasema “anayemlipa mpiga zumari huchagua wimbo”.
     Ipo hatari kwa kiongozi au chama kupokea amri kutoka nchi za nje kwa kuwasikiliza wale watu wa nje waliowasaidia badala ya kujali maslahi ya nchi yetu na watu wake.

Uwajibikaji Kuhusu Michango
    Ndugu Wananchi, Sheria pia inaweka sharti la uwajibikaji wa vyama vya siasa, wagombea na washiriki wengine kuhusu michango, mapato na matumizi katika uchaguzi. Sheria inaelekeza kwamba:- Kila mchango unaopokelewa na matumizi yatakayofanyika kwa ajili ya uchaguzi vifanywe na Chama na siyo vinginevyo. Chama cha siasa kitawajibika kwa matumizi yote yatakayofanywa na chama au wagombea wake, na kwamba matumizi yote yanatakiwa kuwa na risiti. Kila mgombea atawekewa mgawo wake wa matumizi ya kampeni na chama kitatoa taarifa ya fedha iliyokaguliwa kwa matumizi hayo.
      Chama kitakachoshindwa kutunza taarifa hizo kitakuwa kimetenda kosa na kitastahili adhabu. Kila mgombea atakayepokea mchango atapaswa kutoa taarifa kwa chama chake kuhusu mapato na matumizi yanayohusu mchango huo. Kila chama cha siasa, taasisi ya kiraia, taasisi ya kidini au taasisi ya kijamii itakayohusika katika kuchangia shughuli za uchaguzi, inayo wajibu wa kutunza taarifa za fedha zinazoelezea mapato na matumizi yao.
       Haya ni muhimu sana kwani bila ya kuwepo utaratibu wa uwajibikaji kwa upande wa wahusika, Sheria yote itakuwa haina maana. Matatizo tunayojaribu kuyapatia ufumbuzi yatakuwa hayakushughulikiwa ipasavyo. Mambo Yaliyokatazwa Ndugu Wananchi; Sheria imeainisha vizuri mambo yanavyokatazwa kwa upande wa matumizi ya fedha za uchaguzi.
       Sheria inakataza, kwa mfano, vitendo vifuatavyo visifanyike pamoja na matumizi ya fedha kwa ajili hiyo kuzuiliwa:

*Kufanya malipo kwa wapiga kura ili wamchague mgombea fulani; Kuahidi kazi au cheo au wadhifa kwa mpiga kura ili amchague mgombea;

*Kutoa zawadi, ahadi, mkopo, au makubaliano yoyote kwa mpiga kura ili amchague mgombea; Kukubali kurubuniwa kwa mambo yoyote yaliyotajwa hapo juu ili ampigie kura mgombea yeyote;

*Kufanya vitendo vyovyote kati ya hivyo wakati wowote kabla au hata baada ya uteuzi wa mgombea;

*Kutoa malipo kwa ajili ya takrima ya chakula, vinywaji au starehe yoyote kwa ajili ya kuwashawishi wapiga kura wamchague mgombea;

*Kuwasafirisha wapiga kura ili wamchague mgombea.

Kwa hivyo Sheria inaruhusu wapiga kura wenyewe kujilipia nauli kwenda kupiga kura au Serikali kuwasafirisha wapiga kura pale ambapo kuna shida ya usafiri;

Kuweka mkataba wowote ule wa pango kwa niaba ya wapiga kura ili wamchague mgombea; Chama au mgombea au mtu yeyote atakayetenda vitendo hivi nilivyovitaja atakuwa ametenda kosa kwa mujibu wa Sheria hii na ataadhibiwa ipasavyo. Viwango vya Gharama za Uchaguzi

Ndugu Wananchi, Sheria ya Gharama za Uchaguzi inaweka utaratibu wa kudhibiti gharama za uchaguzi kwa kumpa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya uchaguzi kuweka viwango vya gharama za uchaguzi.
      Waziri huyo atatangaza kiwango cha juu ambacho kila mgombea ataweza kutumia katika kampeni na katika uchaguzi. Kiwango hicho cha gharama kitazingatia tofauti ya majimbo, idadi ya watu, aina ya wagombea pamoja na miundombinu.
     Chama au mgombea atakayevuka viwango vya mtumizi alivyowekewa bila maelezo ya kuridhisha, atakuwa ametenda kosa na anastahili kuwajibishwa ipasavyo. 
     Utaratibu huu ni muhimu katika kujenga nidhamu na usawa miongoni mwa vyama na wagombea katika uchaguzi. Hivi sasa kwa sababu ya kutokuwepo ukomo, wako watu wenye pesa ambao wanafanya matumizi kupita kiasi. Wapo wanaopitiliza au hata kukufuru na kuwadhalilisha wenzi wao wasiokuwa na uwezo kama wao.
       Ndugu Wananchi, Mimi naamini, hatua zilizomo katika Sheria ya Gharama za Uchaguzi zikitekelezwa, zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza au hata kudhibiti kabisa vitendo na hisia za rushwa katika uchaguzi.
     Mara nngi vitendo hivyo vinapofanyika, au hata kule kuwepo hisia tu kwamba vinaweza kuwa vimefanyika, huwa ni chanzo cha manung’uniko na kukosekana utulivu. Wakati mwingine huathiri taswira ya demokrasia yetu na heshima ya uongozi uliochaguliwa hasa pale uhalali wa matokeo ya uchaguzi unapotiliwa shaka.
     Inabidi kuchukua hatua kulinda hadhi ya chaguzi zetu nchini na kuzifanya kweli ziwe huru na za haki na kufanya mfumo wa demokrasia uzidi kustawi. Hatima ya yote haya tufanyayo ni kusaidia nchi yetu kuwa na viongozi wanaotokana na ridhaa ya wananchi.
   Ndugu zangu; Demokrasia ya vyama vingi katika nchi yetu bado ni changa. Uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa nne tangu turudi kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Ni muhimu sana, mapema kabisa, kuchukua hatua thabiti za kuilinda demokrasia yetu hii na kuhakikisha inakua na kujengeka katika misingi iliyo sahihi. Sheria hii mpya, tukiisimamia vizuri na kuitekeleza itafanikisha azma yetu hiyo.
    Tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika maendeleo na ustawi wa demokrasia nchini. Mafanikio ya dhamira yetu njema yanategemea sana utashi na ushirikiano wa viongozi na wanachama wa vyama vya siasa pamoja na wananchi katika utekelezaji. Ni matumaini yangu kwamba viongozi wenzangu wa siasa tutaipokea kwa moyo mkunjufu na kuiunga mkono Sheria hii mpya.
    Ni matumaini yangu pia kwamba, sisi viongozi tutawahamasisha wanachama wetu, wapenzi wa vyama vyetu na wananchi wenzetu kwa jumla kuzingatia na kutekeleza Sheria hii. Ndugu Zangu,
    Wananchi Wenzangu, Nimetumia muda wenu mwingi kuwadokeza baadhi ya mambo ya msingi yaliyomo katika Sheria ya Gharama za Uchaguzi. Nia yangu ni kufanya mambo matatu muhimu.
    Kwanza, kuwathibitishia Watanzania wenzangu kwamba tunalitambua tatizo la rushwa katika uchaguzi na tunayo dhamira ya dhati ya kupambana nalo. Kukemea peke yake hakutoshi, lazima tutumie nguvu ya sheria kudhibiti vitendo vya rushwa na kuwaadhibu ipasavyo wahusika.
     Pili, kuwathibitishia kuwa sisi wenzenu tuliopo katika Serikali tunatambua wajibu wetu wa kuhakikisha kuwa Sheria hii inatekelezwa kwa ukamilifu. Nimekwishaviagiza vyombo vya dola, ikiwemo TAKUKURU, kujipanga vizuri kuisimamia Sheria hii na kuwabana ipasavyo wale wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kuanzia katika uchaguzi wa mwaka huu. Nawaomba wananchi mtoe ushirikiano kwa vyombo vyote vinavyohusika na usimamizi wa Sheria hii ili vitimize kwa ukamilifu malengo yake ambayo yana maslahi kwa nchi yetu na kwetu sote.
    Tatu, napenda kuwaambia kwamba, sisi katika Serikali tunatambua wajibu wa kuhakikisha kuwa wananchi, wanachama na viongozi wa vyama vya siasa wanaelimishwa vya kutosha ili waielewe vizuri Sheria hii. Umuhimu wa kuielewa vizuri Sheria hii hauhitaji kusisitizwa kwani watu wakiielewa vizuri inarahisisha utekelezaji wake.
    Na, kwa vyama vya siasa na wagombea, uelewa mzuri utasaidia kuepuka makosa ambayo yanaweza kuwa na gharama kubwa ya wao kupoteza ushindi. Natambua kwamba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Ofisi ya Waziri Mkuu wanajiandaa vizuri kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma kuhusu maudhui ya Sheria hii muhimu.
    Nawaomba ndugu wananchi tusikilize kwa makini ufafanuzi watakaoutoa kwa manufaa yetu na ya nchi yetu.
    Ndugu Wananchi; Naomba nimalize hotuba yangu kwa kuwashukuru kwa mara nyingine tena kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali yetu. Naomba tuendelee kushirikiana katika utekelezaji wa Sheria hii muhimu kwa ajili ya kukuza na kuendeleza demokrasia katika nchi yetu.
     Nataka kuona katika chaguzi zetu nchini tunajenga utamaduni wa kushindanisha sera za vyama na uwezo wa wagombea kuliko kushindanisha uwezo wa kukusanya fedha za kampeni.

Asanteni kwa kunisikiliza!

Mungu Ibariki Afrika


Mungu Ibariki Tanzania

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages