Breaking News

Your Ad Spot

Apr 12, 2010

WABUNGE WATEMBELEA WAZALISHAJI SARUJI SOKO LIKIWA MATATANI

Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi imetembelea Kiwanda cha Saruji Tanga ambacho ni miongoni mwa Wazalishaji Saruji wa Afrika Mashariki (EACPA), kwa ajili ya kujionea athari za uingizaji wa saruji rahisi katika soko la Afrika Mashariki.
     “Ikiwa kasi ya uingizaji wa saruji inayopatiwa ruzuku kutoka nchi inakozalishwa, hasa Pakistan, India, China na Misri utaendelea bila kudhibitiwa, utakuwa sababu ya kufungwa kwa viwanda vya saruji Afrika Mashariki,” Mbunge wa Morogoro Kusini, Hamza Mwenegoha ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa ziara hiyo jana.
   Alisema kwamba kuna haja kubwa ya kuweka uwanja sawa wa ushindani katika biashara ya saruji katika eneo hili, ikiwa ni pamoja na kurejesha kodi kadhaa kama ushuru wa stempu kwa saruji yote inayoingizwa kutoka nje.
    Kwa mujibu wa Mwenegoha, ziara hiyo iliwafungua macho wabunge; kwa hiyo akaahidi kwamba kamati yake itatafakari zaidi juu ya suala hilo na kuwashirikisha mawaziri husika pamoja na kuwasilisha hoja maalumu katika moja ya vikao vya Bunge vinavyoanza wiki hii.
   “Kwa mfano, tuligundua kwamba Tanzania inazalisha karibu tani milioni tatu za saruji kwa mwaka, wakati mahitaji ya sasa ni tani milioni mbili. Hii ina maana kwamba kuna ziada ya tani moja kwenye bohari za wazalishaji. Katika mazingira haya, kweli tunahitaji kudekeza uingizaji wa saruji kutoka nje?” alihoji.
   Mwenegoha alisisitiza haja ya kukomesha uingizaji huo wa saruji kutoka nchi za kigeni katika eneo la Afrika Masharini, akieleza kwamba ikiwa hali hiyo itaendelea, uchumi wa nchi kama Pakistan utakua kwa mgongo wa nchi za Afrika Mashariki ambazo viwanda vyake vitafungwa, wakati kampuni zao zimeshajiorodhesha kwenye soko la hisa.
   Akizungumzia suala hilo hilo, Mwenyekti wa EAPCA, Mbuvi Ngunze, ambaye pia ni Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Saruji Mbeya, alisema kwamba ziara ya wabunge hao imefanyika wakati mwafaka, kwa sababu suala nyeti kwa sasa linalogonga vichwa vya watu katika biashara ya saruji Afrika Mashariki.
   “Julai 2008 Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi na Rwanda katika bajeti zao ziliamua kwa pamoja kufuta kodi ya zuio hadi watakapokuja kupitia suala hilo kutokana na uhaba wa saruji uliokuwapo kutokana na uwezo mdogo wa viwanda. Hii ndiyo sababu ya tatizo lote hili linaloikabili sekta hii leo,” alisema.
   Kwa mujibu wa Ngunze, kwa sasa mahitaji ya saruji katika Afrika Mashariki ni tani milioni 7.1 tu wakati uwezo wa uzalishaji ni tani milioni 10. Hii inatokana na uwekezaji mkubwa wa Dola bilioni 1.1 za Marekani uliofanywa na wazalishaji saruji wa Afrika Mashariki mwaka 2007, ukilenga kuongeza uwezo wao wa uzalishaji kutoka tani milioni 6.6.
   Anatishwa zaidi na ukweli kwamba hata baada ya uwezo wa viwanda kuzalisha kuongezwa, viwango vya kodi havijapitiwa tena na wahusika, na kuhoji inakuwaje kampuni zilizowekeza kiasi kikubwa namna hiyo kwenye eneo hili zinaachwa kuonewa na wafanyabiashara wa saruji rahisi, wanaopewa ruzuku na serikali zao.
    Alisema ipo haja kwa serikali za Afrika Mashariki kuiweka saruji kuwa ni bidhaa muhimu, inayotakiwa kulindwa, kwani gharama zake za uzalishaji ni kubwa katika eneo hili, tofauti na ilivyo katika nchi nyingine kwa sababu mbalimbali, ikiwamo gharam aya umeme na jinsi ya kuifikisha bidhaa hiyo sokoni.
    Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Biashara wa Twiga Cement,  Steiner Harstad, kampuni yake yenye uwezo wa kuzalisha tani 1.4 za saruji kwa mwaka, ikiwa na wafanyakazi 350, ni kampuni pekee Tanzania yenye ISO 14001 kwani huhakikisha udhibiti wa utoaji vumbi wakati wa uzalishaji.
   Makampuni wanachama wa EACPA nchini Tanzania yaani Mbeya Cement, Tanga Cement and Twiga Cement wanajivunia chokaa yyenye viwango vya ubora wa hali ya juu huku kulikoviwanda vingine duniani.Kwa pamoja, viwanda hivyo vimezaliza ajira za moja kwa moja zaidi ya 1600 huku ajira zingine zaidi ya 600,000 ambazo ni kwa makampuni washirika mbalimbali walioko kwenye sekta ya ujenzi. Aidha viwanda hivyo ni mfano bora wa utekelezaji wa dhamira ya Rais Kikwete inayohusu uongezaji thamani wa bidhaa zilizopo nchini.
Mwenyekiti wa wazalishaji Saruji nchini na Meneja Mkuu wa Mbeya Cement, Mbuvi Ngunze (kushoto) akizungumza na baadhi ya Wabunge wa kamati ya Bunge ya Uchumi na Fedha, Clement Lyamba (Mikumi) na Dk Mzeru Nibuka wakati kamati hiyo ilipotembelea Kiwanda cha Cement cha Twiga, Dar es Salaam jana. Kulia ni Mkurugenzi wa Biashara wa Kiwanda hicho, Steinar Harstad



No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages