Breaking News

Your Ad Spot

Dec 24, 2010

ARUSHA KUWA MAKAO YA TAWI LA MFUMO WA KIMATAIFA WA KUSHUGHULIKIA MASHAURI YA MASALIA YA MAKAMA YA MAUAJI YA KIMBARI

NA MWANDISHI MAALUM



NEW YORK
Katika kutunza na kudumisha hadhi ya mahakama za kimataifa za mauaji ya kimbari ya Rwanda (ICTR) na mauaji ya halaiki ya iliyokuwa Yugoslavia ya zamani ( ICTY).Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, limepitisha Azimio la kuanzisha Mfumo wa Kimataifa wa kushughulikia umaliziaji wa mashauri ya masalia ya Mahakama hizo mbili.


Wajumbe wa Balaza hilo (pichani)wamepitisha azimio hilo lililopewa namba 1966 linaloeleza kwamba, mfumo huo wa kimataifa(International Residual Mechanism), utakuwa na matawi mawili yaani tawi la ICTR ambalo makao(seating) yake yatakuwa Arusha na tawi la ICTY ambalo makao yake yatakuwa The Hague, Uholanzi.


Azimio hilo limepitishwa siku ya jumatano kwa kupigiwa kura na wajumbe 15 wa Baraza la Usalama. Katika kura hiyo wajumbe 14 wameunga mkono na mjumbe mmoja hakufungamana na upande wowote.


Kwa tawi la ICTR Mfumo huo utaanza kazi Julai Mosi 2012 na kwa Tawi la ICTY Mfumo huo utaanza kazi Julai Mosi 2013. Mfumo huo wa Kimataifa wa kushughulikia mashauri ya masalia utakuwa na haki, stahili na wajibu kama ilivyo kwa mahakama hizo ambazo zinatarajiwa kukamilisha kazi zake zote si zaidi ya desemba 31 2014.


Kupitishwa kwa azimio hilo na kuanzishwa kwa mfumo huo, licha ya kwamba kunaziongezea muda mahakama hizo kukamilisha kazi zake, lakini pia kunahusisha suala zima la uhifadhi wa nyaraka na kumbukumbu zote muhimu zinazohusiana na shughuli zote za mahakama hizo za kimataifa.


Baraza Kuu la Usalama wa kupitia azimio hilo, limezitaka Mahakama hizo mbili kuweka mazingira mazuri ya kipindi cha mpito kuelekea kuanzishwa kwa mfumo huo wa kimataifa. Na pia kuhakikisha kwamba zinakamilisha kazi zake zote ifikapo desemba 31. 2014, ili kuruhusu mfumo huo kushughulikia mashauri ya masalia na kesi ambazo watuhumiwa kwake bado hawajapatikana.


Vile vile Baraza la limetoa wito kwa nchi zote kuhakikisha kwamba zinatoa ushirikiano madhubuti kwa Mahakama hizo katika kipindi chote cha kuelekea uhitimishaji wa kazi zake.


Ushirikiano huo ni pamoja na kuwakamata watuhumiwa na wahalifu wote wanaosadikiwa kujificha katika nchi zao ili waweze kufikishwa mbele ya sheria.


Baadhi ya wajumbe waliozungumza mara baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, wameeleza kuwa kupitishwa kwa azimio hilo ni moja yahatua muhimu sana si tu katika kuhakikisha kwamba haki inatendeka kwa wahutuhumiwa kufikishwa mbele ya sharia, lakini ni kielelezo tosha kwamba hakuna mhalifu ambaye yuko juu ya sheria.


Kukamilisha na hatimaye kupitishwa wa Azimio hilo kuna hitimisha mchakato na majadiliano ya muda mrefu, ndani ya Baraza Kuu la Usalama na Jumuia ya Kimataifa, kuhusu hatima ya Mahakama hizo za Kimataifa pamoja na uhifadhi wa nyaraka na kumbukumbu zake baada ya kukamilisha kazi zake.


Tanzania kupitia taasisi zake mbalimbali ukiwamo Ubalozi wake katika Umoja wa Mataifa, na kama nchi ambayo ndiyo mweyeji wa Mahakama ya Rwanda iliendesha kampeni na kujenga hoja za nguvu za kutaka ifikiriwe kupewa stahili ya si tu kuhifadhi nyaraka na kumbumbuku za mahakama ya Rwanda bali pia kuwa tawi la kushughulikia ukamilishaji wa mashauri ya masalia ya Mahakama hiyo.

1 comment:

  1. Twashukuru kwa taarifa hii, na kibishara imekaa vyema, na kimahusiano ni ishara njema

    ReplyDelete

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages