Breaking News

Your Ad Spot

Jun 8, 2011

HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA, MHESHIMIWA MUSTAFA HAIDI MKULO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI TAARIFA YA HALI YA UCHUMI WA TAIFA KWA MWAKA 2010 NA MALENGO KATIKA KIPINDI CHA MUDA WA KATI (2011/12- 2015/16)

                   JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA FEDHA


Waziri Mukulo akionyesha mkoba wenye
 hotuba yake ya bajeti leo mjini Dodoma

1.          Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa likae kama Kamati ili liweze kupokea na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa katika kipindi cha mwaka 2010 na malengo katika kipindi cha Muda wa Kati (2011/12 – 2015/16). Pamoja na hotuba hii, nawasilisha Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2010; na Kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2011/12.
2.          Mheshimiwa Spika, kikao hiki cha Bunge la Bajeti ni cha kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika tarehe 31 Oktoba, 2010. Katika uchaguzi huo, Chama Cha Mapinduzi kilishinda na kupata ridhaa ya wananchi ya kuongoza nchi kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

3.        Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuongoza kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne. Aidha, ninampongeza Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Billal kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Vile vile, nampongeza Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge na kuteuliwa tena na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupitishwa na Waheshimiwa Wabunge kwa kishindo kuwa Waziri Mkuu kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne.

4.          Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi kwa kuchaguliwa na hivyo kuwa mwanamke wa kwanza Tanzania kuwa Spika wa Bunge hili. Aidha, nampongeza Naibu wako Mhe. Job Ndugai (Mb.) kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo wa juu katika Bunge kwa kipindi cha Muhula wa Pili wa Serikali ya Awamu ya Nne. Nawapongeza pia mawaziri wenzangu wote pamoja na naibu mawaziri wote kwa kuteuliwa kwao na Mhe. Rais. Aidha, napenda niwapongeze wabunge wote kwa kuchaguliwa na kuteuliwa kwao kuingia katika Bunge hili Tukufu.

5.            Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mhe. Dkt. Abdallah Omari Kigoda, Mbunge wa Handeni, kwa kuchaguliwa tena kuiongoza Kamati ya Fedha na Uchumi katika Bunge lako Tukufu. Aidha, napenda kutoa shukurani za dhati kwa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi kwa kutupatia ushauri wa kina wakati wa kuandaa taarifa hii. Mchango wa Kamati hii siku zote umekuwa na umuhimu wa pekee katika kuboresha taarifa ya Hali ya Uchumi na mapendekezo ya Mpango wa Muda wa Kati. Napenda kuchukua nafasi hii pia kumshukuru Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dr. Philip Mpango kwa ushirikiano wake katika kufanikisha maandalizi ya taarifa hii.

6.          Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa maelezo ya mapitio ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2010, kwanza nibainishe vipaumbele vya mwaka 2011/12 ambavyo serikali itavipa umuhimu katika bajeti ijayo. Vipaumbele hivi vinatokana na changamoto zinazowakabili wananchi katika kukabiliana na hali ngumu ya maisha kwa hivi sasa na umuhimu wa kujenga uchumi imara na wenye ushindani. Vipaumbele hivyo ni:

(i)         Nishati ya umeme: Kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa uhakika wa umeme ili kuziwezesha shughuli za kiuchumi na maendeleo ya jamii kufanyika kwa wakati wote;

(ii)        Usalama wa chakula: Kuongeza upatikanaji wa chakula kwa kuhimiza kilimo, hasa cha umwagiliaji na kuimarisha hifadhi ya chakula ili kujikinga na tatizo la uhaba wa chakula nchini;

(iii)      Miundombinu: Kuimarisha miundombinu ya maji, reli, bandari na barabara pamoja na kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam;

(iv)      Ukosefu wa ajira: Kuongeza fursa za ajira na kuwanufaisha wananchi walio wengi hasa vijana ambao ndio kundi kubwa katika soko la ajira. Aidha, wizara, idara na taasisi za serikali zinaelekezwa kuzingatia suala la kuongeza ajira katika maeneo yao; na

(v)        Mfumuko wa bei: Mfumuko wa bei umesababishwa na kuongezeka kwa wastani wa bei za chakula, bei za mafuta, umeme na gharama za uzalishaji na usafirishaji. Hatua zitachukuliwa kudhibiti ongezeko la bei za mafuta, bei za chakula na kuongeza uzalishaji wa umeme.

7.        Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sasa naomba nianze kutoa muhtasari wa mapitio ya Hali ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii kwa mwaka 2010  ikiwa ni mapitio ya  kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Oktoba 2010.  Aidha, ikumbukwe kuwa taarifa hii ni ya kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2010 na sehemu chache zimegusia robo ya kwanza ya mwaka 2011.

8.        Mheshimiwa Spika, taarifa hii inatokana na uchambuzi wa mwenendo wa viashiria muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na unyambuaji wa masuala muhimu yaliyojitokeza nchini, kikanda na duniani katika mwaka 2009/10 hususan, suala la ukame uliojitokeza nchini mwishoni mwa mwaka 2010 na athari zake kwa sekta mbalimbali za kiuchumi kama vile kilimo, nishati, uzalishaji viwandani pamoja na kupanda kwa kasi bei za mafuta katika soko la dunia.

MAPITIO YA MWENENDO WA UCHUMI DUNIANI KATIKA KIPINDI CHA MWAKA 2010:

9.        Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, uchumi wa dunia na wa Tanzania kwa ujumla ulianza kuimarika baada ya kupita katika kipindi cha mdororo wa uchumi duniani. Kuimarika kwa uchumi wa dunia kulichochea kuongezeka kwa mahitaji ya mauzo nje, uwekezaji wa moja kwa moja na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na utalii. 

Hali ya Uchumi Duniani

10.      Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, biashara duniani iliimarika ikilinganishwa na miaka iliyotangulia kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa katika Nchi Zilizoendelea na Zinazoendelea. Aidha, Pato la dunia liliimarika baada ya kuathiriwa na matokeo ya kuyumba kwa uchumi wa dunia. Mwaka 2010, kasi ya ukuaji wa uchumi duniani iliongezeka hadi wastani wa asilimia 5.0 ikilinganishwa na ukuaji hasi wa asilimia 0.5 mwaka 2009. Kuimarika huko kwa uchumi ni matokeo ya jitihada zilizochukuliwa na Nchi Zilizoendelea za kunusuru uchumi zikiwemo zile za kibajeti na kifedha.

11.    Mheshimiwa Spika, Pato la Nchi Zilizoendelea lilikua kwa asilimia 3.0 mwaka 2010 ikilinganishwa na ukuaji hasi wa asilimia 3.4 mwaka 2009. Kwa upande wa Nchi Zinazoendelea na Nchi za Asia zinazoinukia kiviwanda (China na India), viwango vya ukuaji wa Pato viliongezeka hadi wastani wa asilimia 7.3 na 9.5 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 2.7 na 7.2 mwaka 2009 kwa mtiririko huo. Hii  ilichangiwa  na  kuongezeka kwa uwekezaji na uuzaji bidhaa nje, kupanda  kwa bei za bidhaa  na uvutiaji wa mitaji toka nje ya nchi.

Hali ya Uchumi wa Bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara
             
12.    Mheshimiwa Spika,  kiwango cha ukuaji wa Pato la Bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kiliongezeka kwa wastani wa asilimia 5.0 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 2.8 mwaka 2009. Ongezeko hilo lilitokana na kuimarika kwa bei na mahitaji ya bidhaa za kilimo katika nchi zilizoendelea. Aidha, ukuaji huu wa uchumi kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ulitokana na ukuaji mkubwa kwa nchi zinazouza mafuta nje ambapo kiwango cha ukuaji kilikuwa wastani wa asilimia 6.5 mwaka 2010 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 mwaka 2009.

MWENENDO WA VIASHIRIA VYA UCHUMI JUMLA NCHINI KATIKA KIPINDI CHA MWAKA 2010:

Pato la Taifa
               
13.    Mheshimiwa Spika, ukuaji halisi wa Pato la Taifa ulikuwa asilimia 7.0 mwaka 2010, sawa na ilivyokadiriwa ikilinganishwa na asilimia 6.0 mwaka 2009. Shughuli za kiuchumi zilizochangia ukuaji huu ni pamoja na kilimo na ufugaji; uzalishaji viwandani; biashara na matengenezo ya zana na mitambo; na usafirishaji na mawasiliano. Ukuaji wa viwango vya juu ulijionesha katika shughuli ndogo za kiuchumi za: mawasiliano (asilimia 22.1); ujenzi (asilimia 10.2); umeme na gesi (asilimia 10.2); fedha (asilimia 10.1); na uzalishaji viwandani (asilimia 7.9).

14.    Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, Pato la Taifa lilikuwa shilingi 32,293,479 milioni kwa bei za soko au shilingi 16,828,563 milioni kwa bei za mwaka 2001. Hali kadhalika, kwa mujibu wa kiwango cha ukuaji wa watu cha asilimia 2.9, idadi ya watu Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa watu milioni 41.9. Hivyo, pato la wastani la kila mtu lilikuwa shilingi 770,464.3 mwaka 2010 ikilinganishwa na shilingi 693,185 mwaka 2009, sawa na ongezeko la asilimia 11.1.

Kasi ya Upandaji Bei

15.    Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ilibadilisha mwaka wa kizio wa Fahirisi za Bei za Taifa kutoka mwaka 2001 kuwa mwaka 2007 kwa kutumia matokeo ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa mwaka 2007. Mabadiliko haya yalifanywa kwa kutumia makundi yaliyokubalika Kimataifa ya Mchanganuo wa Matumizi Binafsi “Classification of Individual Consumption by Purpose (COICOP)” na maeneo ambayo mara nyingi jamii hununua bidhaa au hupata huduma mbalimbali (Outlets). Mfumo huu mpya wa ukokotoaji wa fahirisi za bei unatumia wastani wa kijiometria (geometric mean) badala ya wastani wa kawaida (arithmetic mean) katika kutengeneza fahirisi za bei katika ngazi za mwanzo kama inavyokubalika kimataifa kwa ulinganisho. Mizania mpya zinajumuisha matumizi ya kaya zote binafsi kutoka mijini na vijijini wakati mizania iliyokuwa inatumika zamani ilijumuisha kaya binafsi za maeneo ya mijini tu.

16.    Mheshimiwa Spika, Mfumo huu wa kutumia wastani wa kijiometria ulianza kutumika Oktoba 2009, kwa kipindi cha miezi 12 ulitoa mfumuko wa bei wa asilimia 4.2 kwa mwezi Oktoba 2010. Hii ilikuwa ni badiliko la asilimia 0.3 ikilinganishwa na mfumuko wa bei uliotumia wastani wa kawaida wa mwezi Septemba 2010 ambao ulikuwa asilimia 4.5.  

17.    Mheshimiwa Spika, pamoja na mfumuko wa bei kuendelea kuwa tarakimu moja, umekuwa na mwelekeo wa kupanda, hususan, katika robo ya kwanza ya mwaka 2011. Mfumuko wa bei uliongezeka kutoka asilimia 5.6 kwa kipindi kilichoishia Desemba 2010 hadi asilimia 6.4 Januari 2011 na kuendelea kupanda hadi  asilimia 8.6 mwezi Aprili 2011. Kasi hiyo ya ongezeko la bei ilitokana hasa na kupanda kwa fahirisi za bei za nishati, maji na makazi; fahirisi za bei za usafirishaji; na fahirisi za bei za chakula na vinywaji visivyokuwa na kilevi.

Ukuzaji rasilimali
                          
18.    Mheshimiwa Spika, ukuzaji rasilimali kwa bei za miaka husika uliongezeka hadi kufikia shilingi 10,342,536 milioni mwaka 2010 kutoka shilingi 8,173,221 milioni mwaka 2009, sawa na ongezeko la asilimia 26.5. Hii ilitokana na kuongezeka kwa uwekezaji katika ujenzi wa majengo na shughuli nyingine za ukuzaji rasilimali katika ujenzi ikijumuisha uendelezaji ardhi, barabara na madaraja. Uwiano wa ukuzaji rasilimali kwa Pato la Taifa kwa bei za miaka husika ulikuwa asilimia 32.0 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 29.0 mwaka 2009. Hivyo, kadiri uchumi unavyokua, ndivyo na ukuzaji rasilimali unavyoongezeka.

Ujazi wa Fedha na Karadha

19.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2010/11, sera ya fedha ililenga kuwa na kiwango cha ongezeko la ujazi wa fedha kinachoenda sambamba na mahitaji halisi ya uchumi, kasi ya upandaji bei, ongezeko la mikopo ya ndani lisiloathiri uzalishaji mali na ambalo linalingana na malengo ya ujazi wa fedha, na kuwa na akiba ya fedha za kigeni itakayoweza kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi mitano.

20.    Mheshimiwa Spika, hadi Desemba 2010, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana (M2) ulikua kwa   asilimia 21.8 kiwango ambacho kilikuwa chini ya kiwango cha ukuaji cha asilimia 26.3 kwa mwaka ulioishia Juni, 2010. Hata hivyo, kiwango hicho kilikuwa juu kidogo ikilinganishwa na makadirio ya kiwango cha asilimia 20.8 hadi Desemba 2010. Katika kipindi hicho, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ulikua kwa asilimia 25.4 ikilinganishwa na asilimia 25.1 kwa mwaka ulioishia Juni, 2010, na hali kadhalika ikilinganishwa na makadirio ya ukuaji wa asilimia 23.5 Desemba 2010. Kasi ya ongezeko la ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi ilitokana na kasi ya ongezeko la amana katika fedha za kigeni, ambapo ziliongezeka kwa asilimia 23.3 kutoka dola za kimarekani milioni 1,657.3 mwezi Desemba 2009 hadi dola milioni 2,043.6 mwezi Desemba 2010, pamoja na kuimarika kwa dola ya Kimarekani dhidi ya sarafu nyingine.

21.      Mheshimiwa Spika, kiwango cha ukuaji wa mikopo inayotolewa kwa sekta isiyo ya Serikali kiliendelea kuongezeka na kufikia asilimia 20.0 Desemba 2010 kutoka asilimia 16.3 Juni 2010. Hii inatokana na kuanza kujengeka kwa imani ya mabenki dhidi ya sekta binafsi kufuatia kuanza kuimarika kwa hali ya uchumi wa dunia baada ya kupitia katika kipindi cha msukosuko wa Masoko ya Fedha na Mitaji. Sehemu kubwa ya mikopo hii ilielekezwa katika sekta za: biashara asilimia 17.6; uzalishaji bidhaa viwandani asilimia 13.6; uchukuzi na mawasiliano asilimia 9.0; kilimo asilimia 12.3; na mikopo kwa shughuli binafsi asilimia 23.1.

Mwenendo wa Viwango vya Riba

22.     Mheshimiwa Spika, wastani wa jumla wa viwango vya riba za mikopo katika benki za biashara ulipungua hadi asilimia 13.45 Desemba 2010 kutoka asilimia 14.38 Desemba 2009. Wastani wa riba za kukopa kwa muda mfupi (hadi mwaka mmoja) ulipungua kutoka asilimia 13.96 Desemba 2009 hadi asilimia 12.40 Desemba 2010. Aidha, wastani wa jumla wa riba za amana za akiba za muda maalum ulipungua kutoka asilimia 6.36 Desemba 2009 hadi asilimia 5.11 Desemba 2010. Vile vile, wastani wa riba za amana za akiba za muda maalum (miezi 12) ulipungua na kufikia asilimia 7.09 Desemba 2010 kutoka asilimia 8.99 Desemba 2009. Aidha, wastani wa riba za amana za akiba ulipungua na kufikia asilimia 2.41 Desemba 2010 kutoka asilimia 2.83 Desemba 2009. Kutokana na mwelekeo huo wa riba, tofauti baina ya viwango vya riba za amana na mikopo (mwaka mmoja) iliongezeka kutoka asilimia 4.97 Desemba 2009 hadi asilimia 5.31 Desemba 2010.

23.    Mheshimiwa Spika, tofauti kati ya viwango vya riba vinavyotozwa kwenye mikopo na vile vinavyotolewa kwenye amana kama faida imeendelea kuwa juu, licha ya kuongezeka kwa ushindani katika sekta ya kibenki. Hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa na kukosekana kwa taarifa sahihi za wakopaji (credit reference data bank) na kutokuwepo kwa taasisi ya utoaji wa taarifa sahihi za waombaji mikopo (Credit Rerefence Bureau) nchini. Aidha, ukosefu wa vitambulisho vya kitaifa na gharama kubwa za kufanya biashara kutokana na miundombinu hafifu, umechangia kuongeza viwango vya riba vinavyotozwa kwenye mikopo.

Thamani ya Shilingi ya Tanzania

24.    Mheshimiwa Spika, thamani ya Shilingi ya Tanzania kwa mwaka 2010 ilishuka kwa asilimia 8.5 hadi wastani wa shilingi 1,432.3 kwa dola moja ya Kimarekani kutoka wastani wa shilingi 1,320.0 mwaka 2009. Hata hivyo, thamani ya shilingi ilishuka kwa kiwango kidogo mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 10.4 mwaka 2009. Kushuka kwa thamani ya shilingi kulitokana na kuongezeka kwa mahitaji ya dola nchini pamoja na kuimarika kwa dola ya Kimarekani dhidi ya sarafu za mataifa mengine. Aidha, bei ya dola moja ya Kimarekani mwishoni mwa Desemba 2010 ilikuwa na thamani ya shilingi 1,453.5 ikilinganishwa na shilingi 1,313.3 mwishoni mwa Desemba 2009.


Sekta ya Nje

25.    Mheshimiwa Spika, mwenendo wa biashara ya bidhaa na huduma nje kwa mwaka 2010 uliendelea vizuri na ulikuwa wa kuridhisha ikilinganishwa na mwaka 2009. Thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje iliongezeka kwa asilimia 24.1 hadi Dola za Kimarekani milioni 6,388.2 kutoka dola milioni 5,149.5 mwaka 2009. Ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa thamani ya bidhaa zisizo asilia hususan, madini ya dhahabu na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na huduma za usafirishaji na utalii. Vile vile, thamani ya bidhaa na huduma zilizoagizwa toka nje (f.o.b) iliongezeka hadi dola za Kimarekani milioni 8,974.7 kutoka dola milioni 7,543.2 mwaka 2009, sawa na ongezeko la asilimia 19.0. Hii ilitokana na kupanda kwa bei za bidhaa katika soko la dunia na kupanda kwa gharama za malipo ya huduma za usafirishaji.



Akiba ya Fedha za Kigeni

26.        Mheshimiwa Spika, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuongezeka hadi kufikia Dola za Kimarekani milioni 3,948.0 Desemba 2010, kutoka Dola milioni 3,552.5 Desemba 2009, sawa na ongezeko la asilimia 11.1. Kiasi hiki cha akiba ya fedha za kigeni kwa mwaka 2010 kinakidhi uagizaji wa bidhaa na huduma nje kwa muda wa miezi 6.3.

Maboresho ya Sekta ya Fedha

27.    Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza kutekeleza Awamu ya Pili ya Mageuzi katika Sekta ya fedha mwaka 2006/07.  Mageuzi haya ni pamoja na kuimarisha sekta ya mabenki kwa lengo la kuimarisha mazingira ya ushindani katika utoaji wa huduma, kuimarisha masoko ya fedha, mageuzi katika usimamizi wa uwekezaji rasilimali kwa Mifuko ya Hifadhi za Jamii, kuboresha utoaji wa mikopo ya muda mrefu ikiwa ni pamoja na mikopo kwa ajili ya kilimo, mikopo ya makazi na Mikopo ya karadha na kuboresha taarifa za wakopaji kwa kuanzisha chombo cha kutoa taarifa hizo.

28.      Mheshimiwa Spika, hadi sasa mafanikio yamekwisha patikana ikiwa ni pamoja na sekta ya fedha nchini kuendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha. Kulingana na vigezo na viashiria vya uimara wa sekta ya fedha, mabenki yote nchini yanakidhi viwango vya mtaji unaoweza kuhimili madai (capital adequacy ratio); yana ukwasi wa kutosha kukidhi malipo kwa wateja (liquidity ratio); na ukuaji wa kuridhisha wa mikopo kwa sekta binafsi.

29.      Mheshimiwa Spika, taasisi za kifedha zinaendelea kufungua matawi kwenye maeneo nje ya miji mikubwa ili kuweza kupata wateja na pia kwa sababu ya ushindani mkubwa uliopo sasa maeneo ya mjini.  Taasisi nyingine kama vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) na Benki za wananchi zimeweza kujipenyeza hata kwenye miji midogo na vijijini. Huduma asilia za kibenki kwa ujumla zimeongezeka sambamba na ongezeko kubwa kwenye huduma zinazotolewa kwa njia za teknolojia ya mawasiliano ya simu na mashine za kuweka na kutoa fedha - ATMs. Changamoto kubwa kwa sasa ni juu ya suala la usimamizi kwani makampuni ya simu yanayotoa huduma hizi yanasimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania –TCRA, ambayo haihusiki na masuala ya kifedha bali ya mawasiliano. Hata hivyo, Benki Kuu inakamilisha mazungumzo na TCRA kuiwezesha kushiriki katika kusimamia masuala ya huduma za kifedha zinazofanywa na makampuni ya simu.

30.    Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa hadi mwishoni mwa mwaka 2010 huduma na taasisi za fedha zilikuwa kama ifuatavyo: Idadi ya benki na taasisi za fedha - 43; Akaunti za benki - 4,241,610;  Matawi ya benki na taasisi za fedha - 475; Mashine za kutolea fedha  - ATMs, - 969;  Mtandao wa malipo  (Switches) - 2;  Vituo vya mauzo  (POS) - 1,427. Aidha, baadhi ya taasisi za fedha hutoa huduma za kibenki bila matawi. Idadi ya benki zinazotoa huduma za kibenki kupitia simu za mkononi - 5; Idadi ya benki zinazotoa huduma za kibenki kupitia intaneti - 5; Watumiaji wa huduma za kibenki za malipo kwa njia ya simu za mkononi – 10,372,331.

31.      Mheshimiwa Spika, elimu ya masuala ya kifedha ni muhimu katika kusaidia kupanua wigo wa huduma za kibenki na serikali imefanya juhudi za kuweka mazingira bora ya kuongeza elimu hii ambapo mwongozo wa kitaifa umeshaandaliwa. Aidha, maandalizi ya utafiti wa msingi juu ya uelewa wa umma kuhusu maana ya uwezo kifedha yanaendelea. Matokeo ya utafiti huu yatarahisisha utoaji wa elimu ya kifedha kwa umma. Vilevile, mchakato wa kuandaa mfumo wa kumlinda mtumiaji wa huduma za kifedha umeshaanza. Mfumo huo utaongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa kuwawezesha wananchi kuwa na taarifa sahihi na za uwazi kuhusu huduma hizo.

32.    Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Huduma za Kifedha Vijijini umeandaliwa. Lengo la Mkakati huo ni kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa mtu mmoja mmoja, kaya na wajasiriamali wadogo na wa kati ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini kwa maeneo ya vijijini. Mkakati huo upo katika mchakato wa kuridhiwa na Serikali.

33.     Mheshimiwa Spika, Serikali imeanzisha kampuni itakayohusika kutoa mikopo ya nyumba kwa kupitia katika benki za biashara, na hivyo wananchi kuweza kukopa kupitia katika benki hizo. Kampuni hizo inajulikana kwa jina la “Tanzania Mortgage Refinance Company” (TMRC) na iko chini ya usimamizi wa Benki kuu. Aidha, mchakato kwa ajili ya kuanzisha mfuko wa kutoa mikopo midogo na ya muda mrefu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kwa wananchi wa kipato cha chini umeanza.

34.      Mheshimiwa Spika, mchakato wa kuanzisha benki ya Maendeleo ya Kilimo uko kwenye hatua za mwisho. Lengo la uanzishwaji wa benki hii ni kuwasaidia wananchi kupata mikopo kwa riba nafuu na ya muda mrefu ili waweze kujikwamua kiuchumi. Aidha, wakati mchakato wa uanzishwaji wa benki hiyo unaendelea, Serikali kwa muda mfupi, imefungua dirisha la kutoa mikopo ya kilimo katika Benki ya Rasilimali Tanzania. Serikali pia imeibadili Benki ya Rasilimali na kuwa taasisi ya kutoa mikopo ya maendeleo ya muda mrefu. Aidha, Serikali inaandaa mfumo wa kisera, sheria, kanuni na taratibu za upatikanaji na utoaji wa mikopo ya muda mrefu.

35.    Mheshimiwa Spika, mfumo wa malipo nchini umeboreshwa na kuleta ufanisi katika kutekeleza sera za kiuchumi na fedha. Mfumo wa malipo baina ya mabenki nchini ulioanza kutumika rasmi mwaka 2004 umeendelea kuboreshwa kwa kuhakikisha kwamba unatumika kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali na baadhi ya malipo yanayofanywa na Serikali. Hali kadhalika, mfumo wa malipo ya hundi umeendelea kuboreshwa kwa kupunguza malipo kwa njia ya hundi.

36.      Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, Kanuni zitakazotumika katika masuala ya taarifa za mikopo zilichapishwa kupitia Tangazo la Serikali namba 177 na 178 la mwaka 2010 na kuanza kutumika rasmi mwezi Oktoba 2010. Hali kadhalika, Serikali ilihitimisha mchakato wa uanzishwaji wa Mamlaka ya Kusimamia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (Social Security Regulatory Authority - SSRA) ambayo jukumu lake ni kukuza ufanisi na kuongeza ushindani katika mifuko ya pensheni na hivyo kuchangia zaidi kwenye ustawi wa uchumi. Aidha, Serikali inaendelea na mchakato wa kuboresha taratibu za mafao ya mifuko yote ya hifadhi ya jamii ili ilingane na iwe endelevu.

37.    Mheshimiwa Spika, licha ya mafanikio yaliyopatikana chini ya programu ya uboreshaji wa sekta ya fedha, zipo changamoto ambazo Serikali itaendelea kutafuta ufumbuzi wake. Changamoto kubwa ni viwango vikubwa vya riba kwenye mikopo ambavyo vimeendelea kutozwa na benki za biashara ikilinganishwa na riba ndogo inayolipwa kwa amana. Serikali inaendelea na mkakati wa kuimarisha soko la dhamana za serikali ili kufikia viwango halisi vya riba vinavyotokana na nguvu za soko na visivyobadilika mara kwa mara. Hali kadhalika, Serikali inaendelea na mikakati yenye lengo la kuimarisha miundombinu katika sekta ya fedha pamoja na kuimarisha mazingira ya ushindani katika sekta hiyo.

Bajeti ya Serikali

Mapato

38.    Mheshimiwa Spika, mapato ya ndani yaliongezeka kwa asilimia 8.2  mwaka 2009/10 kufikia shilingi bilioni 4,661.5 kutoka shilingi bilioni 4,293.1 mwaka 2008/09. Hata hivyo, kiasi hicho kilichokusanywa ni pungufu ya makadirio kwa asilimia 8.8 kwa mwaka 2009/10. Wastani wa makusanyo kwa mwezi uliongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 357.8 kwa mwezi mwaka 2008/09 hadi shilingi bilioni 388.5 kwa mwezi mwaka 2009/10 na shilingi bilioni 473 kwa mwezi kwa miezi tisa ya mwaka 2010/11.

39.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2010 hadi Machi 2011, mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 4,256.3, ikiwa ni asilimia 31 chini ya lengo la bajeti ya mwaka 2010/11 ambalo ni shilingi bilioni 6,176.2.  Mapato yaliyopatikana katika kipindi hicho cha Julai 2010 hadi Machi 2011 yalikuwa asilimia 21 zaidi ya mapato yaliyokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2009/10.

Misaada na Mikopo
                    
40.    Mheshimiwa Spika, misaada ya nje katika mwaka 2009/10 ilikuwa shilingi bilioni 1,405.3 ikilinganishwa na matarajio ya shilingi bilioni 2,090.9 katika kipindi hicho. Aidha, mikopo ya nje katika mwaka 2009/10 ilikuwa shilingi bilioni 1,379.6 na mikopo ya ndani ilikuwa shilingi bilioni 568.5 ikilinganishwa na matarajio ya shilingi bilioni 1,037.1 na shilingi bilioni 500.2 kwa mtiririko huo. Katika kipindi cha Julai 2010 hadi Machi 2011, jumla ya  misaada na mikopo ya kibajeti  ilikuwa shilingi bilioni 845.7, sawa na asilimia 3 zaidi ya makadirio ya bajeti. Misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo ilifikia shilingi bilioni 1,427.6, sawa na asilimia 58 ya bajeti.
Matumizi

41.      Mheshimiwa Spika, matumizi ya Serikali yalifikia shilingi bilioni 8,173.7 mwaka 2009/10, sawa na asilimia 92.0 ya makadirio. Kati ya hizo, matumizi ya kawaida yalikuwa shilingi bilioni 5,562.4 na ya maendeleo yalikuwa shilingi bilioni 2,611.3. Matumizi  ya maendeleo yalikuwa asilimia 8.0 chini ya lengo hasa kutokana na kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi kulikosababishwa na  baadhi ya Wizara, Idara,  Mikoa na Halmashauri kuchelewa kukamilisha taratibu za ununuzi  na kutoa taarifa za matumizi ya fedha za miradi. Matumizi ya kawaida pia yalikuwa asilimia 8.0 chini ya malengo.

42.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2010 hadi Machi 2011, matumizi ya Serikali yalifikia shilingi bilioni 7,169.3, ikiwa ni asilimia 67 ya makisio ya matumizi kwa mwaka mzima wa 2010/11. Katika kipindi hicho cha robo tatu mwaka, matumizi ya maendeleo yalikuwa shilingi bilioni 1,942.4 na ya kawaida yalikuwa shilingi bilioni 5,226.9 ikilinganishwa na bajeti ya shilingi bilioni 3,819.0 na shilingi bilioni 7,790.5 kwa mwaka 2010/11 kwa mtiririko huo. Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2011/12 nitakayowasilisha leo jioni itabainisha kwa kina mwenendo wa mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2010/11 na makadirio ya mwaka 2011/12.

Deni la Taifa

43.      Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Desemba 2010, deni la Taifa lilikuwa limefikia Dola za Kimarekani milioni 11,380.2 ikiwa ni ongezeko la Dola milioni 654.28 ikilinganishwa na deni la kipindi kama hicho mwaka 2009. Ongezeko hili lilitokana na mikopo mipya ya ndani na nje yenye masharti nafuu kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
44.        Mheshimiwa Spika, malipo ya deni la Taifa katika kipindi cha robo tatu ya mwaka ulioishia Machi 2011 yalikuwa shilingi bilioni 803.64. Malipo ya deni la nje kwa kipindi hicho yalikuwa shilingi bilioni 73.66. Kati ya hizo, shilingi bilioni 29.06 zilikuwa ni malipo ya mtaji na shilingi bilioni 44.6 zilikuwa ni malipo ya riba. Malipo ya deni la ndani kwa robo tatu mwaka ulioishia Machi 2011 yalikuwa shilingi bilioni 730.3. Kati ya hizo, shilingi bilioni 556.7 zilitumika kulipia dhamana za Serikali zilizoiva kwa utaratibu wa kukopa na kulipia dhamana zilizoiva na shilingi bilioni 173.6 zilikuwa ni malipo ya riba.

Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kikanda na Kimataifa

45.    Mheshimiwa Spika, mwaka 2010 ushirikiano wa Tanzania kimataifa na kikanda uliendelea kuimarika na hivyo kuendelea kulijengea taifa mazingira mazuri ya shughuli za kiuchumi na kijamii. Kanda hizo ni pamoja na za Jumuiya ya Afrika Mashariki; Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika; Umoja wa Afrika na Tume ya Uchumi ya Bara la Afrika; Umoja wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Udhibiti wa Biashara ya Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi; na Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano.

Jumuiya ya Afrika Mashariki

46.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010, Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walikutana mjini Arusha na kuichagua Burundi kuwa Mwenyekiti kwa kipindi cha mwaka mmoja. Wakuu hao walielekeza Baraza la Mawaziri la Jumuiya kuchagua kwa makini vipaumbele vinavyotekelezeka katika kuandaa Mkakati wa Maendeleo ya Afrika Mashariki kulingana na uwezo wa kibajeti. Aidha, walielekeza Baraza la Mawaziri la Jumuiya likamilishe majadiliano ya kuanzishwa kwa Soko la Pamoja la Jumuiya ili kuweka mpangilio wa taasisi zitakazosaidia utekelezaji wake kuanzia mwaka 2011.  Vilevile, walielekeza kuongeza kasi ya kufikia malengo ya pamoja ya uchumi jumla kwa nchi za Jumuiya ambayo ni kigezo muhimu kwa ajili ya kuanzisha matumizi ya sarafu moja.

47.    Mheshimiwa Spika, kufuatia hatua zilizochukuliwa za kuimarisha biashara miongoni mwa nchi wanachama, biashara kati ya Tanzania na nchi hizi za Jumuiya ya Afrika Mashariki iliendelea kukua ambapo mauzo ya bidhaa za Tanzania katika nchi hizi yaliongezeka  kwa asilimia 70.6 kufikia Dola za Kimarekani milioni 450  mwaka 2010 kutoka Dola milioni 263.8  mwaka 2009, wakati ambapo uagizaji wa bidhaa ulipungua kwa asilimia 8.2.

48.      Mheshimiwa Spika, kumekuwa na matukio ya meli kutekwa kwenye eneo la Bahari ya Hindi hadi kufikia pwani za baadhi ya nchi za Jumuiya. Hali hii inahatarisha usalama na uchumi wa nchi wanachama. Hivyo, Wakuu wa Nchi walielekeza zichukuliwe jitihada za kukabiliana na tishio hilo katika ngazi za kitaifa, kijumuiya na kimataifa ili maharamia hao wasiweze kuhatarisha amani na usalama wala kuhujumu uchumi wa nchi wanachama.
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika

49.      Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC ilishiriki kwenye mkutano wa pamoja wa uwekezaji kwenye miundombinu kwa Jumuiya Tatu za Afrika Mashariki; Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika na Soko la Pamoja la Nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika uliofanyika Nairobi Kenya. Mkutano huo ulitoa fursa ya pekee kwa SADC kubainisha maeneo ya uwekezaji kwenye miundombinu ya Mashariki na Kusini mwa Afrika kwa washirika wa maendeleo na wawekezaji binafsi kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Vipaumbele vilivyoainishwa vipo katika miradi ya ukanda wa usafirishaji, usambazaji wa maji na usafi (water and sanitation), nishati na mawasiliano. Vipaumbele hivyo vipo katika Programu ya Uhamasishaji wa Uwekezaji ndani ya SADC ya mwaka 2010.



Umoja wa Afrika na Tume ya Uchumi ya Bara la Afrika

50.    Mheshimiwa Spika, pamoja na ukuaji wa uchumi kwa nchi za Afrika katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, imebainika kuwa tatizo la ajira limeendelea kuwa kubwa na kuongezeka. Hivyo, Umoja wa Afrika - AU, na Tume ya Uchumi ya Bara la Afrika - ECA, katika kikao chake cha tatu cha pamoja kilichofanyika Machi 2010, kilijadili namna ya kusaidia ukuaji wa Uchumi endelevu kwa lengo la kupunguza ukosefu wa ajira ndani ya Afrika. Hii ni kwa sababu ukosefu wa ajira sio kwamba unakwamisha tu jitihada za kupunguza umaskini bali pia ni chanzo cha kudidimiza rasilimali watu, kuongezeka kwa tofauti za vipato na kusababisha vurugu za kijamii katika nchi. Aidha, nchi zilishauriwa kuwa na mwelekeo wa kukuza uchumi unaoendana na ongezeko la ajira kwa wingi ili kufanikisha lengo la kupunguza umaskini.



Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano
                                                  
51.     Mheshimiwa Spika, Tume za pamoja za Ushirikiano kati ya Tanzania na nchi marafiki ziliendeleza mahusiano, ambapo mkutano wa nne wa Tume ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Algeria ulifanyika Dar es Salaam, Juni 2010. Mkutano huo ulikuwa wa manufaa makubwa kwa Tanzania kwa kuwa mkataba wa kufuta deni la dola za kimarekani milioni 144.14 ulitiwa saini. Aidha, mazungumzo juu ya makubaliano ya kutotoza kodi mara mbili baina ya nchi hizi mbili bado yanaendelea.

52.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, mkutano wa wataalam kati ya Tanzania na Brazil ulifanyika, ambapo suala la masharti nafuu ya kulipa deni la Tanzania inalodaiwa na Brazil kiasi cha dola za Kimarekani milioni 237.0 lilijadiliwa. Makubaliano ya awali ilikuwa kwamba tulipe sehemu ya deni ambalo lilikuwa ni kiasi cha dola za kimarekani milioni 17.6 na sehemu iliyobaki tungesamehewa.  Mpaka sasa tumeshalipa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 6.4. Aidha, ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji ulifanikisha ujenzi wa daraja la Umoja kati ya nchi mbili hizi, ambapo uzinduzi wake ulifanyika mwezi Mei 2010 na Marais wa Msumbiji na Tanzania.

Umoja wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Udhibiti wa Biashara ya Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi (ESAAMLG)

53.        Mheshimiwa Spika, Tanzania inaendelea kushiriki katika mikutano ya Baraza la Mawaziri la Umoja huo ambao makao makuu ya Sekretarieti yapo mjini Dar es Salaam. Aidha, Tanzania inaendelea kuboresha mfumo wa usimamizi wa Sekta ya Kifedha ili kuboresha mifumo hiyo kwa lengo la kudhibiti biashara ya fedha haramu katika shughuli za kiuchumi ambazo zinaweza kudhoofisha uchumi wa nchi.

MAENDELEO YA SHUGHULI MBALIMBALI ZA KIUCHUMI NA KIJAMII:

54.    Mheshimiwa Spika, mawaziri wa wizara husika wataeleza kwa kina maendeleo katika maeneo yao; hivyo katika hotuba hii, nitatoa tathmini ya kiujumla tu ya maendeleo katika baadhi ya maeneo hayo.

Kilimo, Mifugo, Misitu na Uwindaji

55.      Mheshimiwa Spika, shughuli za kiuchumi za kilimo zinazojumuisha mazao; mifugo; na misitu na uwindaji zilikua kwa kiwango cha asilimia 4.2 mwaka 2010  ikilinganishwa na asilimia 3.2 mwaka 2009. Ukuaji huu ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao kufuatia kuwepo kwa hali nzuri ya hewa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2009/10; kuimarika kwa miundombinu ya umwagiliaji; jitihada za Serikali za kuongeza ruzuku ya pembejeo za kilimo; na utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo ASDP. Aidha, mchango wa shughuli za kiuchumi za kilimo ulikuwa asilimia 24.1 ya Pato la Taifa mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 24.6 mwaka 2009.

Uvuvi

56.    Mheshimiwa Spika, shughuli za kiuchumi katika uvuvi zilikua kwa kiwango cha asilimia 1.5 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 2.7 mwaka 2009. Kiwango kidogo cha ukuaji kilitokana na kuongezeka kwa ushindani wa mauzo ya samaki na mazao yake nje ya nchi; kupungua kwa kasi ya uvuvi, hususan katika maji baridi uliotokana na kudhibiti uvuaji holela na uharibifu wa mazingira katika mazalia ya samaki; vitendo vya uvuvi haramu; na matumizi ya zana duni za uvuvi. Aidha, mchango wa shughuli za uvuvi katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 1.4 kama ilivyokuwa mwaka 2009.



Viwanda na Ujenzi

57.      Mheshimiwa Spika, shughuli za viwanda na ujenzi zinajumuisha: uzalishaji bidhaa viwandani; umeme na gesi; usambazaji wa maji; madini, uchimbaji wa mawe na ujenzi. Shughuli za kiuchumi katika viwanda na ujenzi zilikua kwa kiwango cha asilimia 8.2 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2009. Aidha, mchango wa shughuli za viwanda na ujenzi katika Pato la Taifa uliongezeka kutoka asilimia 22.0 mwaka 2009 hadi asilimia 22.4 mwaka 2010.

58.      Mheshimiwa Spika, shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani zilikua kwa kiwango cha asilimia 7.9 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 8.0 mwaka 2009. Kupungua kwa kiwango cha ukuaji kulitokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji. Mchango wa shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani katika Pato la Taifa uliongezeka kutoka asilimia 8.6 mwaka 2009 hadi asilimia 9.0 mwaka 2010.
59.    Mheshimiwa Spika, kiwango cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika umeme na gesi kilikuwa asilimia 10.2 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 8.4 mwaka 2009. Hii ilitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme unaotokana na nguvu za maji; na juhudi za Serikali za kuweka mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi. Shughuli za kiuchumi za umeme na gesi zilichangia asilimia 1.8 katika Pato la Taifa mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 1.7 mwaka 2009. Pamoja na kuwa na mchango kidogo katika Pato la Taifa, umeme na gesi ni sekta muhimu inayotegemewa sana kwa maendeleo ya sekta nyingine kama vile uzalishaji viwandani na huduma.

60.    Mheshimiwa Spika, shughuli za kiuchumi za ujenzi zilikua kwa kiwango cha asilimia 10.2 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 7.5 mwaka 2009. Ukuaji huo ulichangiwa na kuongezeka kwa shughuli za ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja; majengo ya kuishi na yasiyo ya kuishi; viwanja vya ndege; na miundombinu ya maji. Mchango wa shughuli za ujenzi katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 8.0 mwaka 2010 ukilinganisha na asilimia 7.9 mwaka 2009.

Huduma

61.    Mheshimiwa Spika, shughuli za utoaji huduma zinajumuisha biashara na matengenezo; uchukuzi; mawasiliano; hoteli na migahawa; utawala; elimu; afya; huduma za fedha na bima; na upangishaji wa majengo. Kiwango cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika utoaji huduma kilikuwa asilimia 8.2 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 7.2 mwaka 2009. Viwango vya ukuaji katika shughuli zote ndogo za huduma viliongezeka mwaka 2010 kutokana na kuanza kuimarika kwa shughuli zilizoathiriwa na hali ya mdororo wa uchumi duniani kama vile shughuli ndogo za fedha, hoteli na migahawa, biashara na matengenezo na uchukuzi. Mchango wa shughuli za utoaji huduma katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 43.9 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 43.6 mwaka 2009.
62.    Mheshimiwa Spika, huduma za mawasiliano katika mwaka 2010 zilikua kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko shughuli nyingine za kiuchumi. Kiwango cha ukuaji kwa shughuli hizi kilikuwa asilimia 22.1 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 21.9 mwaka 2009. Ukuaji huu ulichangiwa na kuongezeka kwa wateja wa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi. Mchango wa shughuli za mawasiliano katika Pato la Taifa uliendelea kuwa asilimia 2.1 mwaka 2010 kama ilivyokuwa mwaka 2009.

63.      Mheshimiwa Spika, shughuli za biashara na matengenezo zilikua kwa asilimia 8.2 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 7.5 mwaka 2009. Ukuaji huo ulichangiwa zaidi na kuongezeka kwa mahitaji kufuatia kuanza kuimarika kwa uchumi wa dunia. Shughuli ndogo za biashara na matengenezo ndizo zilizokuwa na mchango mkubwa katika utoaji wa huduma. Mchango wa shughuli za biashara na matengenezo ulikuwa asilimia 12.1 ya Pato la Taifa mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 11.8 mwaka 2009.

MASUALA MTAMBUKA:


64.    Mheshimiwa Spika, idadi ya watu Tanzania kwa mwaka 2010 ilikadiriwa kuwa 43,187,823. Kati ya hao, wanawake walikuwa 21,935,400, sawa na asilimia 50.8 na wanaume walikuwa 21,252,423, sawa na asilimia 49.2. Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa na jumla ya watu 41,914,311, sawa na asilimia 97.1 ya watu wote ambapo Tanzania Zanzibar ilikuwa na watu 1,273,512, sawa na asilimia 2.9 ya watu wote. Mgawanyo wa watu unaonesha kuwa watu 31,809,808, sawa na asilimia 73.7 ya watu wote wanaishi vijijini, wakati watu 11,378,015, sawa na asilimia 26.3 wanaishi mijini. Makadirio haya yanatokana na kiwango cha ukuaji wa idadi ya watu cha asilimia 2.9 cha Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002. Sensa kama hii inatarajiwa kufanyika tena mwakani (2012) na maandalizi yake yanaendelea vizuri.

65.    Mheshimiwa Spika, mchanganuo wa idadi ya watu Tanzania unaonesha kuwa asilimia 44.4 ya watu wote ni wenye umri chini ya miaka 15. Idadi ya watu waliokuwa na umri kati ya miaka 15 - 24 walikadiriwa kuwa 8,580,351, sawa na asilimia 19.9 ya watu wote. Idadi ya watu wenye miaka kati ya 15 - 64, ambao ndio nguvukazi, ilikuwa ni 22,661,280, sawa na asilimia 52.5 ya watu wote. Watu wenye umri wa miaka 65 au zaidi walikuwa ni 1,361,435, sawa na asilimia 3.2 ya watu wote. Kati ya hao, wanawake walikuwa 718,299 na wanaume ni 643,136. 

Nguvukazi na Ajira

              
66.    Mheshimiwa Spika, kulingana na matokeo ya Utafiti wa Nguvukazi na Ajira wa mwaka 2006, nguvukazi nchini ilikuwa watu milioni 18.8 ambapo milioni 9.0 walikuwa wanaume na milioni 9.7 walikuwa wanawake. Vilevile, matokeo hayo yanaonesha kuwa watu milioni 16.6 walikuwa wameajiriwa na milioni 2.2 walikuwa hawajaajiriwa, sawa na asilimia 11.7 ya nguvukazi yote nchini. Kati ya walioajiriwa, watu milioni 8.5 walikuwa wanawake na wanaume milioni 8.0. Hata hivyo, kulingana na matokeo ya Sensa ya Idadi ya Watu na Makazi ya mwaka 2002, ilikadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2010 kutakuwa na   nguvukazi nchini (miaka 15 – 64) ya watu 22,661,280. Sekta ya kilimo iliendelea kuongoza, ambapo zaidi ya asilimia 70 ya walioajiriwa nchini wanajishughulisha na kilimo.

Utawala Bora


67.    Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, Serikali iliendelea kutekeleza azma yake ya utoaji haki kwa wote kwa kutafsiri Sheria kumi na nne kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili. Vilevile, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliendelea na juhudi zake za kukuza, kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na utawala bora katika jamii.

68.      Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, Tume iliendelea kushughulikia malalamiko ya wananchi ambapo jumla ya malalamiko mapya na ya zamani 7,858 yalishughulikiwa. Kati ya hayo, Tume ilihitimisha malalamiko 1,003 mwaka 2010 ikilinganishwa na malalamiko 657 yaliyoshughulikiwa na kuhitimishwa mwaka 2009. Malalamiko 6,855 yaliyobaki yanaendelea kushughulikiwa.

69.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010, jumla ya mashauri 2,624 yalipokelewa na Mahakama ya Rufani. Kati ya hayo, mashauri 627 yalikamilishwa na mashauri 1,997 yaliendelea kushughulikiwa. Aidha, katika Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya, kulikuwa na jumla ya mashauri 62,154.  Kati ya hayo, mashauri 46,977 yalisikilizwa na mashauri 15,177 yaliendelea kufanyiwa kazi. Vile vile, katika Mahakama za Mwanzo, jumla ya mashauri 218,767 yalipokelewa ambapo mashauri 167,228 yalisikilizwa na 51,939 yaliendelea kusikilizwa.

70.      Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, Serikali iliendelea na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa (NACSAP II). Katika utekelezaji wa Mkakati huo, TAKUKURU ilipokea na kufanyia uchunguzi kesi za rushwa 870. Kati ya kesi hizo, kesi 587 zilifikishwa mahakamani na kesi 64 zilitolewa hukumu.

71.    Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, Serikali iliendelea na utoaji wa mafunzo ya Utawala Bora ambapo kamati za maadili za wizara 21 na taasisi za umma 32 zilipatiwa mafunzo ya utawala bora na usimamiaji wa Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa.

72.    Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kupambana na ukatili nchini, Serikali ilitoa mafunzo kuhusu utokomezaji wa ukatili dhidi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu wa ngozi. Mafunzo haya yaliwahusisha wakuu wa vituo vya polisi 40 na viongozi wa vijiji 43 kutoka mikoa ya Kigoma, Arusha, Dodoma, Tabora na Manyara. Aidha, mafunzo hayo pia yalitolewa kwa wasimamizi wa sheria katika wilaya za Rorya, Tarime, Bukombe na Kahama.


Mazingira

73.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010, miongozo mitatu ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira iliandaliwa. Miongozo hiyo ni: Mwongozo wa Kuandaa Mipango ya Usimamizi wa Mazingira ya Wizara na Wakala wa Serikali za Mitaa; Mwongozo wa Ujenzi wa Minara ya Mawasiliano; na Mwongozo wa Kushughulikia Changamoto za Mabadiliko ya Tabianchi.

74.    Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kutekeleza programu na miradi mbalimbali kwa ajili ya kuhifadhi bioanuwai katika ziwa Tanganyika, mradi wa kuhifadhi mazingira Bonde la Kihansi, na Mradi wa Kuhifadhi Mazingira Pwani katika Bahari ya Hindi. Aidha, Serikali iliendelea kuratibu utekelezaji wa Mkataba wa Kyoto unaolenga kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.



Vita Dhidi ya UKIMWI

75.    Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, upanuzi wa huduma kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ulifanyika ambapo huduma ziliongezeka kutoka halmashauri 110 mwaka 2009 hadi halmashauri 133. Idadi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI  na  ambao  wanapata dawa  za kupunguza makali  ya VVU iliongezeka kwa asilimia 10.3 kutoka watu 284,227  mwaka 2009 hadi 313,384 mwaka 2010. Katika idadi hiyo, watoto chini ya miaka 15 walikuwa 28,309 na watu wazima kuanzia miaka 15 walikuwa 285,075.

76.      Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, vituo vinavyotoa huduma ya unasihi na upimaji viliongezeka kwa asilimia 24.5 kutoka vituo 1,743 mwaka 2009 hadi vituo 2,170. Mafunzo mbalimbali yalitolewa kwa washauri 300 na kufanya idadi ya watoa huduma kuwa 5,365 nchini kote. Hadi Desemba 2010, watu wapatao 8,890,207 walikuwa wamepimwa na majibu kutolewa.


77.      Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, Serikali iliendelea kuhakikisha uwepo wa uwiano wa kijinsia kwenye ngazi mbalimbali za uongozi nchini. Katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2010, uwiano wa wanawake kushiriki katika ngazi za maamuzi uliongezeka kutoka asilimia 26 mwaka 2006 hadi asilimia 31 mwaka 2010. Kiwango hiki ni juu ya lengo la MKUKUTA la asilimia 30 mwaka 2010 lakini chini ya lengo la SADC la asilimia 50. Mchanganuo wa baadhi ya nafasi zilizoongezeka zinazoshikiliwa na wanawake tangu mwaka 2006 hadi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ni kama ifuatavyo: Majaji 13 hadi 34; Mawaziri 4 hadi 10; Makatibu Wakuu 7 hadi 9; Makatibu Tawala za Mikoa 4 hadi 10; Wakuu wa Wilaya 20 hadi 25; Wakurugenzi wa Halmashauri 14 hadi 35; na Wakurugenzi kwenye wizara na taasisi, 19 hadi 133. Aidha, kufuatia matokeo ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 2010, idadi ya wabunge wanawake imefikia 126, sawa na asilimia 36 ya wabunge wote 350 waliopo kwa sasa. Aidha, idadi ya mawaziri wanawake ni asilimia 26.7 ya mawaziri wote 30 waliopo.

DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2025:

78.    Mheshimiwa Spika, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ilizinduliwa rasmi mwaka 2000. Mwaka 2010, Serikali ilifanya mapitio ya utekelezaji wa Dira. Malengo makuu ya mapitio hayo yalikuwa: kuchambua mafanikio yaliyofikiwa katika kutekeleza malengo ya Dira tangu ilipozinduliwa; kubainisha fursa na changamoto ambazo inabidi zifanyiwe kazi katika kipindi kilichobaki toka sasa hadi 2025; na kupendekeza malengo mahsusi ya miaka mitano mitano na hatua au sera mbadala ambazo zitaingizwa katika mipango ya maendeleo.

79.    Mheshimiwa Spika, mapitio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 yalibainisha kwamba dhana ya Dira ya Taifa ya Maendeleo bado ni sahihi na inatekelezeka. Aidha, mapitio hayo yalibainishahaja ya kuwa na mfumo linganishi wa utayarishaji na utekelezaji wa mipango ya muda wa kati na mrefu. Vile vile, mapitio yaliweza kubainisha changamoto ambazo Serikali inaendelea kuzifanyia kazi. Changamoto hizo ni kama ifuatavyo:

         (i)        Kwamba ingawa ukuaji wa uchumi ulikuwa unaongezeka, ukuaji huo ulikuwa  chini ya  kiwango kinachohitajika kufikia shabaha na malengo ya Dira;

        (ii)        Vyanzo vya ukuaji wa uchumi havikuwagusa watu wengi hususan, maskini vijijini na katika maeneo ya pembezoni, na havikuweza kuzalisha fursa za ajira za kutosha;

      (iii)        Umaskini ulipungua lakini kwa kiwango kidogo hususan, vijijini na katika kaya zinazotegemea kilimo;

      (iv)        Japokuwa kwa kipindi kirefu mfumuko wa bei uliendelea kuwa wa chini na tarakimu moja, athari za majanga yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa katika uzalishaji wa mazao, sambamba na ongezeko la bei za mafuta katika soko la dunia zimesababisha kuongezeka kwa kasi ya upandaji bei katika siku za karibuni pamoja na gharama za uzalishaji; na

Tanzania imejaliwa kuwa na fursa za rasilimali za asili nyingi, kijiografia imekaa eneo zuri linalopakana na bahari na inashiriki kikamilifu katika mtangamano wa jumuiya za kikanda na kimataifa. Hata hivyo, fursa hizo hatujaweza kuzitumia kikamilifu kuinua uchumi. Tunahitaji kuboresha  miundombinu hususan, ya usafirishaji ili tuweze kutumia kikamilifu fursa ya kupakana na bahari kuweza kuwa kitovu cha biashara cha kuhudumia nchi za maziwa makuu na zisizopakana na bahari. Aidha, suala la upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika ni budi litafutiwe ufumbuzi na mkakati uliopo ni kuboresha miundombinu yake pamoja na kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali vikiwemo maji, upepo, jua, gesi na makaa ya mawe.

MKUKUTA na Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs):

80.      Mheshimiwa Spika, awamu ya kwanza ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA) ilitekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2005/06 hadi 2009/10. Katika utekelezaji wake, mafanikio kadhaa yalipatikana yakiwemo ukuaji wa uchumi, ongezeko katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, usimamizi thabiti wa fedha za umma, uimarishaji wa barabara vijijini, pamoja na uboreshaji wa sekta za elimu, afya na maji.  Wastani wa kiwango cha ukuaji wa uchumi ulikuwa asilimia 6.9 kati ya mwaka 2005 na 2010 na hivyo kuwa ndani ya lengo la MKUKUTA la asilimia 6 – 8. Hata hivyo, zipo changamoto zilizojitokeza  ikiwa  ni pamoja na kasi ndogo ya kupungua kwa kiwango cha umaskini, upatikanaji na ubora wa huduma kwa viwango vilivyokusudiwa, ushiriki mdogo wa sekta binafsi, na uhaba wa rasilimali.

81.      Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine zilikuwa nje ya uwezo wa Serikali, zikiwemo kupanda kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia, ukame uliotokea katika maeneo mengi nchini katika kipindi cha mwaka 2005/06 na 2008/09, ukosefu wa umeme wa uhakika na kuyumba kwa uchumi wa dunia kulikoanza mwishoni mwa mwaka 2008. Pamoja na uhaba wa rasilimali, Serikali ilikuwa ikiongeza mwaka hadi mwaka kiasi cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa MKUKUTA kutoka asilimia 54.1 ya bajeti yote mwaka 2005/06 wakati utekelezaji wa MKUKUTA ulipoanza hadi asimia 71.2 mwaka 2009/10. 

82.    Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana, changamoto, na mambo tuliyojifunza katika kipindi chote cha utekekelezaji wa awamu ya kwanza ya MKUKUTA yamechambuliwa kwa kina katika taarifa ya utekelezaji wake kwa mwaka 2009/10. Serikali iliandaa awamu ya pili ya MKUKUTA ambao ulipitishwa mwezi Oktoba 2010. Mchakato wa uandaaji wa awamu hii uliwashirikisha wadau wengi na ulizingatia zaidi mambo tuliyojifunza na mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya MKUKUTA.

83.    Mheshimiwa Spika, mapitio ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia yanaonesha kuwa, Tanzania imefanya vizuri katika baadhi ya viashiria kama vile uandikishaji katika elimu ya msingi, kupunguza vifo vya watoto wachanga, kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano na usawa wa jinsia. Mwaka 2010, kiwango cha kukatisha masomo katika elimu ya msingi kilishuka hadi asilimia 2.6 kutoka asilimia 3.7 mwaka 2009 kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Aidha, wastani wa uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi uliimarika kutoka uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 54 (1:54) mwaka 2009 hadi 1:51 mwaka 2010 ikilinganishwa na lengo la 1:45. Aidha, kwa mujibu wa Utafiti wa Afya na Idadi ya Watu wa mwaka 2009/10, kiwango cha vifo vya watoto wachanga kilipungua mwaka 2010 kufikia vifo 51 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai kutoka vifo 68 mwaka 2007, wakati kiwango cha vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kilipungua mwaka 2010 kufikia 81 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa kutoka vifo 112 mwaka 2007.

84.      Mheshimiwa Spika, changamoto bado zipo katika viashiria vingine, kama vile, afya ya uzazi wa mama na umaskini wa kipato. Hivyo, kipaumbele sasa kimewekwa katika kuongeza ufanisi katika maeneo hayo ya changamoto na kuimarisha zaidi utekelezaji pale ambapo Tanzania imepata mafanikio kiasi.

Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi

85.    Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, mafanikio yamepatikana katika utoaji wa mikopo na uanzishwaji wa SACCOS na vikundi vidogo vidogo vya kiuchumi vya vijana na wanawake. Mikopo hiyo ilitolewa kupitia mifuko na program mbalimbali ikijumuisha Program ya Taifa ya Kuongeza Kipato; Mpango wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira; Mfuko wa Uwezeshaji Mwananchi; na Mradi wa Kutoa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo (SELF).

86.    Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, Serikali kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi ilitoa mikopo yenye masharti nafuu ya thamani ya shilingi bilioni 1.2 na hivyo kufanya jumla ya mikopo iliyotolewa na Mfuko hadi sasa kufikia shilingi bilioni 4.6 kwa wajasiriamali. Mikopo hiyo ilitolewa kwa vyama 30 vya akiba na mikopo (SACCOS) katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Manyara, Singida na Rukwa. Aidha, mikopo hiyo iliwawezesha wajasiriamali kukuza uchumi wao kwa kusaidia ununuzi wa pembejeo za kilimo, kama matrekta ya mikono (power tillers) na hivyo kuwa na uwezo wa kuongeza ukubwa wa mashamba na kipato. Hadi kufikia Desemba 2010, kiasi cha shilingi bilioni 4.34 zilirejeshwa, ikiwa ni sawa na asilimia 94 ya fedha zilizokopeshwa.

87.      Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, utekelezaji wa Mpango wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi na kuongeza Ajira uliendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kupitia Benki na asasi nyingine za kifedha. Mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 47.14 ilitolewa kwa wajasiriamali 72,197. Kati ya wajisiriamali hao, wanaume walikuwa 45,858, sawa na asilimia 64 na wanawake walikuwa 26,339, sawa na asilimia 36. Hadi kufikia Desemba 2010, shilingi bilioni 36.1 ambazo ni sawa na asilimia 76.6 ya mikopo iliyotolewa zilikuwa zimerejeshwa.

88.      Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, Serikali kupitia Mradi wa Kutoa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo (SELF) ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 8.7. Aidha, katika kipindi hicho, Mradi ulikusanya marejesho ya mikopo kiasi cha shilingi bilioni 6.1 sawa na asilimia 70.1 ya mikopo iliyotolewa. Mikopo hiyo iliwafikia wananchi 8,631, wenye kipato cha chini waliopo mijini na vijijini. Kati ya hao, wanawake walikuwa 5,092 sawa na asilimia 58 na wanaume walikuwa 3,539 sawa na asilimia 41.


Uendelezaji wa Sekta Binafsi

89.    Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu lilipitisha Sheria ya Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Binafsi - PPPA Na. 19 ya mwaka 2010 mwezi Agosti 2010. Madhumuni ya Sheria hii ni kuweka mfumo mzuri wa kisheria kwa ajili ya kuratibu ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji wa miradi na huduma za ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi.  Vitengo vya PPP tayari vimeanzishwa katika Wizara ya Fedha na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuratibu masuala yanayohusiana na PPP. Kupitia vitengo hivyo, Serikali imekamilisha mkakati na mwongozo wa utekelezaji wa sheria ya PPP, hususan katika miradi mikubwa ya miundombinu. Kanuni za utekelezaji wa Sheria ya PPP pia zimekamilika. Sambamba na hilo, Serikali kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Tanzania (MKUMBITA) inaendeleza jitihada za kuondoa urasimu ili kupunguza muda na gharama za kuendesha shughuli za uchumi na biashara nchini.

Uwekezaji Mitaji ya Kigeni ya Moja kwa Moja

90.     Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, thamani ya mitaji ya uwekezaji kutoka nje ya nchi – FDI, ilikuwa Dola za Kimarekani milioni 573.3 ikilinganishwa na dola za Kimarekani milioni 558.4 mwaka 2009, sawa na ongezeko la asilimia 2.7. Ongezeko hili linatokana na kuanza kuimarika kwa uchumi wa dunia. Sekta za Viwanda, Utalii, na Majengo ya Biashara ziliongoza katika uwekezaji na kutoa fursa za ajira.

MISINGI NA MALENGO YA UCHUMI NA MAENDELEO YA JAMII:

91.      Mheshimiwa Spika, malengo ya sera za uchumi jumla katika mwaka 2011/12 yatakuwa yafuatayo:

(i)     Pato halisi la Taifa litakua kwa asilimia 6.0 mwaka 2011, na asilimia 7.2 mwaka 2012;
(ii)    Kuendelea kudhibiti kasi ya upandaji bei ili ibaki kwenye viwango vya tarakimu moja;

(iii)  Kuongezeka kwa mapato ya ndani yatakayofikia uwiano wa asilimia 17.2 ya Pato la Taifa mwaka 2011/12 na kuendelea kuongezeka kwa wastani wa asilimia 17.5 kwa mwaka kwa kipindi cha muda wa kati;

(iv)  Kudhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi unaotarajiwa kukua kwa asilimia 19.0 mwaka 2011/12 na asilimia 18.6 mwaka 2012/13; Ukuaji huu unalenga kuwiana na malengo ya ukuaji wa uchumi, na kasi ya upandaji bei;

(v)    Kuwa na akiba ya fedha za kigeni itakayoweza kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma toka nje kwa kipindi kisichopungua miezi  4.6;


(vi)  Kupunguza tofauti ya viwango vya riba; na

(vii)Kuwa na kiwango  imara cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha.

92.       Mheshimiwa Spika, malengo tuliyokusudia ya uchumi jumla katika kipindi cha mwaka 2011/12 yatafikiwa kwa kuzingatia misingi ifuatayo:-
(i)         Kuendelea kuimarika kwa amani, utulivu na utengamano;

(ii)       Vyanzo vya maji vitaendelea kuhifadhiwa na kukidhi mahitaji;

(iii)     Utengamavu wa viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii utaendelea kuimarika;


(iv)     Mapato ya ndani yataongezeka na kuboreshwa ikiwa ni pamoja na kubuni vyanzo vipya vya kodi, kuimarisha ukusanyaji wa kodi ya majengo, na kupunguza misamaha ya kodi ili kuweza kugharamia vipaumbele vilivyoainishwa;

(v)       Ufanisi katika usimamizi wa matumizi ya fedha za umma utaongezeka;

(vi)     Rasilimali zitaelekezwa kwenye maeneo yanayochochea ukuaji wa uchumi  kwa haraka zaidi;

(vii)   MKUKUTA II utatekelezwa kama ulivyopangwa;

(viii) SAGCOT na Nguzo 10 za Kilimo Kwanza zitatekelezwa kama ilivyopangwa;

(ix)     Mazingira ya biashara yataboreshwa ili kuendeleza ushirikishwaji wa sekta binafsi; na


(x)       Sera ya fedha (monetary policy) itaimarika ili iendane na sera za bajeti (fiscal policies) zitakazosaidia kupunguza mfumuko wa bei na tofauti ya riba za kukopa na amana, na kuongeza mikopo kwa sekta binafsi.

MAJUMUISHO:

93.        Mheshimiwa Spika, baada ya kueleza hali ya uchumi wa Taifa, matarajio, misingi na malengo ya mpango na bajeti kwa kipindi cha mwaka 2011/12 ni wazi kwamba hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha uchumi kwa kiasi kikubwa zimeweza kuzaa matunda yaliyotarajiwa. Juhudi zitaendelea kuelekezwa katika kuhakikisha ukuaji wa uchumi unaimarika zaidi.

94.    Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza mambo muhimu ambayo tunahitaji kuyapa msukumo zaidi katika utekelezaji na ufuatiliaji wa karibu kwa mwaka 2011/12 kama ifuatavyo:

(i)     Kuongeza msukumo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025;

(ii)    Kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi  na kukuza Pato la Taifa;

(iii)  Kuongeza uwekezaji katika maeneo ya kimkakati na yenye mwingiliano kisekta hususan, umeme, bandari, reli, maji na chakula cha hifadhi na kuhimiza ushiriki wa sekta binafsi katika maeneo hayo;

(iv)  Kutumia fursa ya nchi yetu kuwa kiungo muhimu kibiashara na nchi zinazotuzunguka ambazo hazina bandari;

(v)    Kuhimiza na kuhamasisha utekelezaji wa Kilimo Kwanza;

(vi)  Kujizatiti katika kuboresha mazingira ya biashara; na
(vii)Kuongeza na kusimamia mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi na kuimarisha usimamizi katika matumizi ya fedha za umma.

95.      Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
UTANGULIZI:

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages