Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania |
Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo katika Ikulu ya Dar-es-Salaam amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi kazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) Dr. Tonia Kandiero.
Taarifa iliyotolewa na Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi Ikulu, Premi Kibanga, imesema Dr. Kandiero amefika Ikulu kujitambulisha baada ya kuanza kazi hapa nchini mwezi Mei, mwaka huu kuchukua nafasi ya Dr. Sipho Moyo ambaye alimaliza muda wake hapa Tanzania.
ADB ni moja ya wahisani wakubwa hapa Tanzania ambapo sehemu kubwa ya misaada yake inaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na hasa sekta za barabara, Kilimo, Maji na Nishati.
Dr. Kandiero pia amefika Ikulu kumueleza rasmi Rais Kikwete kuhusu mkutano mkuu wa magavana wa benki hiyo utakaofanyika mjini Arusha tarehe 30 Mei – 01 Juni, 2012.
Mapema kabla ya kuonana na mwakilishi wa AFDB, Rais Kikwete amekutana na Balozi Sander Gurbuz wa Uturuki ambaye amefika Ikulu kumuaga Rais Kikwete baada ya kufikia ukingoni mwa muda wake wa kuiwakilisha nchi yake hapa Tanzania.
Nchi ya Uturuki imefungua ubalozi wake kwa mara ya kwanza hapa Tanzania mwaka 2009 na Balozi Gurbuz ndiye amekua muanzilishi wa Ubalozi huo.
Tangu kufunguliwa kwa Ubalozi huo, mahusiano baina ya Uturuki na Tanzania yamekua kwa kiwango kikubwa na miradi mbalimbali ya maendeleo, kibiashara na kijamii imeanza na kuimarika katika kipindi chake.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269