Na Mwandishi Maalum, New York
Wakati majadiliano kuhusu uanzishwaji wa mkataba wa kisheria utakaoratibu na kudhibiti biashara ya silaha duniani yakiendelea, Tanzania imesema, inashiriki majadiliano hayo si kwa sababu inazalisha au kusambaza silaha bali ni mazingira inayozungukwa nayo.
“Tunashiriki madiliano haya muhimu si kwa sababu tunazalisha silaha au kusambaza silaha, tunashiriki kwa sababu tumezungukwa na majirani ambao ama wamo katika migogoro ya wenyewe kwa wenyewe au migogoro kati ya nchi moja na nyingine”.
Msimamo huo umetolewa siku ya jumanne na Kaimu Balozi wa Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Dkt. Justin Seruhere wakati alipokuwa akichangia majadiliano ya jumla kuhusu uanzishwaji wa mkataba wa kisheria wa biashara ya silaha duniani.
Kaimu Balozi Seruhere anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo akishirikiana na Brigedia Jenerali Dkt. Charles Muzanila kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ)
Mkutano huu unaohusu majadiliano kuhusu mkataba wa biashara ya silaha duniani, ni mkutano muhimu na nyeti kwa mustakabali suala zima la ulinzi na usalama na hususani katika eneo la uagizaji, usambazaji, na matumizi ya silaha ndogo ndogo na nyepesi.
Ni majadiliano yanayovuta hisia na kugusa maslahi ya watu wengi, na ni mkataba ambao vilivile kama hautajadaliwa vema na kuzingatia maslahi na matakwa ya nchi nyingi hasa zinazoendelea unaweza kwa namna moja ama nyingine kuingilia uwezo na uhuru wa mataifa kujilinda na kulinda mipaka yake.
“ Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa mwenyeji wa kuhifadhi wakimbizi wanaokimbia machafuko katika nchi zao. Lakini pia tumekuwa tukishuhudia usafirishaji wa silaha haramu kupitia mipaka yetu. Hali hii inatishia misingi ambayo tumejiweka , misingi ambayo ni amani , ulinzi na usalama” akasisitiza Dkt. Seruhere.
Na kwa sababu hiyo, Tanzania inasisitiza kwamba kuanzishwa kwa mkataba huo kutasaidia sana katika kuthibiti usambazaji na matumizi haramu ya silaha hizo , silaha ambazo zimekuwa zikipoteza maisha ya mamilioni ya watu wasio na hatia.
Hata hiyo, Tanzania imebainisha na kueleza wazi kwamba ingawa inaamini katika kuwapo kwa mkataba huo, lakini kamwe mkataba huo usiingilie haki ya mataifa kujilinda na kulinda mipaka yake.
“ Tunaposhiriki majadiliano haya, lengo letu ni moja tu kwamba tutatoka na mkataba wa kisheria ambao utazingatia viwango vya kimataifa katika kuagiza, kusafirisha au kuhamisha silaha ndogo ndogo na nyepesi. Lakini tunaamini kwamba haki ya nchi kujilinda itabaki kuwa msingi mkuu wa mkataba huu. Kwa maneno mengine mkataba usiingilie na kuzuia bali kudhibiti”. Akasisitiza
Aidha Tanzania imesisitiza kwamba utengenezaji wa silaha kwa madhumuni ya kujilinda isiwe sehemu ya mkataba huo.
Karibu kila nchi ambayo imezungumza katika mkutano huu zimejaribu kutoa mwelekeo wa nini inataka kiingizwe au kisiingizwe katika mkataba huo.
Baadhi zimeeleza umuhimu wa kuzingatia uwazi na ukweli wakati wa majadiliano haya, huku wakibainisha kwamba kwa namna yoyote ile mkataba huo usilenge katika kuzipendelea nchi chache.
Wengine wanataka mkataba uandikiwe katika lugha nyepesi na inayoeleweka na ufafanue na kuweka wazi madhumuni na malengo halisi ya mkataba huo.
Wazungumzaji wengine wamesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kwamba mkataba unakuwa katika hali itakayopelekea nchi nyingi kuuridhia mara utakapoandaliwa. Na kuongeza kwamba litakuwa kama jambo jema kama mkataba huo utapitishwa na nchi zote bila ya kupigiwa kura.
Mkutano huu wa mwezi mmoja unafanyika hapa Makao makuu ya Umoja wa Mataifa, na mchakato wa majadiliano ya kuanzishwa kwa mkataba huu umeanza miaka sita iliyopita.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269