Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma linawashikilia watu watatu mbaroni kwa tuhuma za kujichukulia sheria mikononi na kusababisha mauaji kwa mtuhumiwa wa wizi wa mifugo aliyejulikana kwa jina la Juma Kidongoi, mwenye umri wa miaka (36) Mgogo wa Mugunga Wilaya ya Chamwino.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwanadamizi wa Jeshi la Polisi Bw. Zelothe Stephen alisema watu hao walifanya tukio hilo la kijichukulia sheria mikononi siku ya jumanne tarehe 17/07/2012 majira ya saa tisa na nusu alasiri katika kijiji cha Sejeli, Kata ya Sejeli Tarafa ya Kongwa na Wilaya ya Kongwa.
Aliwataja watuhumiwa hao wa kujichukulia sheria mikononi na kusababisha kifo kuwa ni Msafiri Matonya miaka (27) Elikana Majimoto miaka (37) na Joel Mazengo miaka (34) wote ni wakazi wa Kijiji cha Sejeli Wilaya ya Kongwa Mkoani Dododma
Akizungumzia tukio hilo Bw. Zelothe Stephen alisema watuhumiwa hao walimshambulia kwa mawe na fimbo mtuhumiwa wa wizi wa mifugo baada ya kujaribu kukimbia wakati alipokamatwa na mgambo wakiswaga punda wa wizi kijijini hapo na kumsababishia kifo chake.
“Mgambo wa Kijiji cha Sejeli walikuwa wamewakamata watuhumiwa watatu wa wizi wa mifugo, ghafla mmoja wao akajaribu kukimbia ndipo wakapiga mwano, na wanakijiji wakatoka kwa ajili ya ukamataji miongoni mwao wakiwa watuhumiwa hao ambao walianza kumshambulia mtuhumumiwa huyo kwa mawe na fimbo.” alieleza Kamanda Zelothe Stephen
Bw. Zelothe Stephen alieleza kwamba watuhumiwa hao wa wizi wa mifugo walikuwa wakiswaga Punda kumi na moja kati ya Punda hao kulikuwa na Punda wanne mali ya Bw. Petro Chikumbi wa kijiji cha Banyibanyi kata ya Hogoro, Kongwa ambao waiibwa katika mji wake mwingine huko katika kijiji cha Ngusele wilaya ya Kiteto.
Kamanda Zelothe Stephen alisema katika kuwatafuta punda hao ndipo mlalamikaji huyo alikutana na watu watatu wakiwa wanaswaga punda kumi na moja katika kijiji cha Sejeli, Kwa kuwa alikuwa peke yake aliogopa kuwauliza watu hao na badala yake akaenda kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho kutoa taarifa.
Aidha Bw. Zelothe Stephen alieleza kwamba Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Sejeli Bw. Maiko Machimo ailitisha mgambo wa kijiji hicho na kuwaelekeza kwenda kuwafuatilia watu hao, ambapo waliwakamata wakiwa na punda hao kumi na moja, ambapo mlalamikaji aliwagundua punda wake wanne kwa alama alizowawekea katika masikio.
Katika utambuzi huo, ndipo mmoja wa watuhumiwa wa wizi wa mifugo alijaribu kukimbia ambapo wanakijiji walianza kumkimbiza mtuhumiwa huyo na kumkamata na kuanza kumshambulia kwa mawe na fimbo mpaka akawa hoi na kumfikisha katika ofisi za Mtendaji ambako alifariki dunia
Aidha Katika tukio hilo Kamanda Zelothe aliwataja, watuhumiwa wawili wa wizi wa mifugo ambao wamekamatwa kuwa ni Msafiri Chomola mwenye umri wa miaka (24) mgogo na makazi wa kijiji cha mugunga katika wilaya ya Chamwino na Mtachi Kogani Miaka (38) mgogo wa Kijiji cha Ng’inila kata ya Berege wilaya ya mpwapwa.
Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma alito wito kwa wanakijiji wa Sejeli kupitia mkakati wake wa Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi kuacha vitendo vya kujichukuilia sheria mikononi na badala yake pindi wanapowakamata wahalifu wawafikishe sehemu husika wakiwa salama ili kuruhusu upelelezi kufanyika kwa makini ili kuweza kubaini mtandao wa uhalifu wa aina hiyo na kuutokomeza katika maeneno yao.
CONTACT: POLISI MKOA WA DODOMA, DAWATI LA HABARI, ELIMU NA MAHUSIANO,
Phone: 0715 006523, Luppy Kung’alo – Mrakibu msaidizi wa Polisi (ASP)
Phone: 0712 360203, Silyvester Onesmo – Police Konstebo (PC)
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269