Mke
wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi
(aliyefunikwa mwamvuli) akiwasili kwenye sherehe ya siku ya wanawake
duniani iliyoandaliwa na Zanzibalicious Women Group na kufanyika ndani
ya ukumbi wa Salama, Bwawani Hotel mwishoni mwa wiki.
Na Mwandishi wetu, Zanzibar
UTAFITI
uliofanywa na taasisi ya wanawake nchini Zanzibar ya Zanzibalicious
Women umeonyesha kuwa asilimia 40 ya wanawake Zanzibar, wanaishi katika
mazingira duni ya umasikini kwa kutojitambua na kukosa elimu ya uelewa
jinsi ya kukabiliana na mazingira waliyomo.
Akisoma
risala siku ya wanawake mbele ya mgeni rasmi mke wa rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Mama Mwanamwema Shein , katika
siku ya wanawake hafla iliyofanyika hoteli ya Bwawani, Mweka hazina wa
Zanzibalicious Women Group, Shekha Hilal alisema hali hiyo ni changamoto
kubwa na sasa kunatafutwa namna ya kumfikia mwanamke huyu ambaye
ameshagota katika jamii yetu.
“Mama
Shein asilimia hii ni kubwa saana, na sisi kama wanawake ambao tayari
tumejaaliwa elimu na tunajitambua, ikiwa ni pamoja na tayari tumepiga
hatua kimaendeleo katika nyanja mbalimbali, tumeguswa sana sana na
suala hili.” Alisema Shekha.
Zanzibalicious
ni umoja wa wanawake wanaoishi Zanzibar,ulioanzishwa mwaka 2011,na
kusajiliwa rasmi mwaka 2013, ikiambatana na uzinduzi uliofanyika tarehe
28 Machi 2014.
Mke
wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama
Mwanamwema Shein akiwasili kwenye sherehe ya siku ya Wanawake duniani
iliyoandaliwa na Zanzibalicous Women Group mwishoni mwa wiki katika
ukumbi wa Salama, Bwawani Hotel.
Mweka
hazina huyo alisema kwamba wanajiuliza maswali mengi kama mwanamke huyo
elimu ya kujikwamua imemfikia au kama kuna jitihada zozote za
kumfikishia elimu hiyo.“Je
hili ni jukumu la serikali peke yake? Au sisi tunatakiwa tujumuike na
serikali? mheshimiwa mgeni rasmi tumeona ya kwamba tuungane pamoja na
serikali katika kutekeleza suala hili.” Alisema Shekha akielezea nia ya
taasisi hiyo ya kuondoa umaskini miongoni mwa wanawake nchini Zanzibar.
Alisema
taasisi yao inajipanga kutoa elimu za aina mbili ili awali kumuwezesha
kujikimu kupitia ujasiriamali, kwa kumpatia elimu kwa vitendo,kwa
mfano:-ushonaji,ufugaji na utengenezaji wa bidhaa mbali mbali na pili
kumtoa katika hali ya upweke ili elimu atakayopata imfikishe kwenye
mifuko mbali mbali pamoja na mfuko wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein .
Alisema
katika program hiyo wanatarajia baada ya miaka 2 wanawake 100 watakuwa
wanajitegemea wenyewe na kuwa mabalozi katika kuelimisha wanawake
wengine zaidi.
Mke
wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama
Mwanamwema Shein akisoma hotuba wakati wa sherehe ya siku ya wanawake
duniani iliyoandaliwa na Zanzibalicous Women Group na kufanyika ndani
ukumbi wa Salama, Bwawani hoteli mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Mke wa
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akifuatiwa na
Mwenyekiti mstaafu wa Zanzibalicious Women Group, Bi. Ummukulthum
Ansel.
“Na
kama kila mwanamke akiweza kuelimisha wanawake katika kaya yake ,baada
ya miaka kadhaa, Zanzibar itakuwa na wanawake walioweza kujikomboa
katika dimbwi hili la kuishi maisha duni.” Alisema.
Akizungumzia
mafanikio ya asasi hiyo alisema kwamba imefanikiwa kutoa elimu na
kuwawezesha kina mama kuunda vikundi vidogo vidogo vya maendeleo kwa
kuanzisha miradi mbalimbali, kwa mfano kina mama wa Chaani na Matemwe. Aidha
imetoa misaada ya hali na mali kwa waathirika wa madawa ya kulevya
ikiwa ni moja ya kumkwamua mwanamke na kutoa misaada mbali mbali kwa
wanawake wasiojiweza ikiwemo hospital kuu ya Mnazi mmoja na kina mama
wajane.
Alisema
pamoja na mafanikio hayo bado wanawake wanakabiliwa na changamoto za
ndoa za utotoni, uzazi salama, ukatili wa kijinsia,mfumo dume, ubaguzi
na mimba za utotoni.
Mhe.Mgeni rasmi, Umoja huu umekuwa ukiendesha shughuli zote tokea mwaka 2011 kwa kutegemea michango yetu sisi binafsi.
Baadhi ya wakinama waliohudhuria sherehe hiyo wakionekana kufurahishwa na hotuba ya Mke wa Rais wa Zanzibar (hayupo pichani).
Changamoto
hii imesababisha kutokutimiza kwa malengo yetu kwa muda tulioupanga
kutokana na kukosa fedha za kutosheleza utekelezaji wa malengo hayo.
Akijibu
risala hiyo Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein, ameikumbusha jamii kuunganisha nguvu
zao kuwakomboa wanawake kujiendeleza kimaisha na kujiongezea kipato.
Alisema
hatua hiyo itaongeza kasi ya kuimarisha ustawi wa familia na jamii
hususan wanawake wanaoishi vijijini ambao wanakabiliwa na changamoto
zaidi.
Alisema
sherehe ya siku ya wanawake duniani inakuwa na maana zaidi kama juhudi
zitafanyika kuangalia changamoto na kujipanga kuzifanyia kazi.
“Rai
yangu ni kuwa tuwazingatie zaidi akina mama wanaoishi vijijini na wenye
mahitaji maalum kutokana na kukosa fursa kama hizo za kuwaendeleza
kimaisha”, alisisitiza.
Mweka
hazina wa Zanzibalicious Women Group, Bi. Shekha Hilal akisoma risala
kwa mgeni rasmi Mke wa Rais wa Zanzibar (hayupo pichani) Kulia ni
Mwenyekiti wa Zanzibalicous Women Group, Bi. Evelyne Wilson.
Aidha,
aliongeza kuwa wanawake ni jeshi kubwa ambalo likiandaliwa vyema
linaweza kushinda katika mapambano yanayokusudiwa huku akisisitza
mshikamano ili kufikia malengo yanayowekwa.
Akizungumzia
ujumbe wa sherehe hizo ambao ni kuhamasisha hatua mathubuti
kumwendeleza na kumtambua mwanamke, alitoa rai kwa wanawake kushirikiana
na serikali katika kampeni za kupambana na madhila wanayokabiliana nayo
ikiwa ni pamoja na ukatili wa watoto na wanawake.
Kuhusu
uzoefu wake katika maisha na malezi ya watoto, alisema amebahatika
kupata watoto 11 ambao amewalea katika mazingira mbalimbali ikiwa ni
kwenda na kurudi kazini na kuwa pekee huku mumewe akiwa safarini kikazi.
Aidha, aliwataka wanawake kuwa wastahamilivu katika malezi ya watoto hasa watoto Njiti ambao huzaliwa kabla ya kufikisha muda.
Hata
hivyo aliwaonya wanawake wanaojali kujiremba na kuwa sahau watoto na
kukumbusha kwa ‘watoto ni wageni’ kwamba wanahitaji matunzo na ukarimu
mkubwa kutoka kwa wazazi wao.
Mke
wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, akizindua Mfuko wa
Zanzibalicious Women Group kwa kuchangia shilingi milioni tano, wakati
wa maadhimisho ya sherehe ya wanawake duniani visiwani Zanzibar
yaliyoandaliwa na Zanzibalicious Women Group na kufanyika katika ukumbi
wa Salama uliopo Bwawani Hotel Zanzibar. Kulia ni Mwenyekiti wa
Zanzibalicious Women Group, Bi Evelyne Wilson Baruti.
Mweka
hazina wa Zanzibalicious Women Group, Shekha Hilal akinakili majina ya
watu waliokuwa wakichangia kwenye harambe ya mfuko wa Zanzibalicous
Women Group uliozinduliwa rasmi na Mke wa Rais wa Zanzibar Mama
Mwanamwema Shein (hayupo pichani).
Mbunifu
nguli wa mavazi Mama wa mitindo, Asia Idarous akinadi moja ya nguo
alizotengeneza kwa ajili ya kuchangia mfuko wa Zanzibalicious Women
Group.
Mke
wa Naibu Waziri wa Afya serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi. Zakhia
Kombo akitangaza dau la kununua nguo hiyo iliyokuwa ikinadiwa kwenye
harambe ya mfuko wa ZWG iliyozinduliwa na Mama Mwanamwema Shein.
Meza kuu kwenye picha ya pamoja na Zanzibalicous Women Group.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269