Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia katika
mkutano wa Kiuchumi na maendeleo wa Misri, uliofunguliwa jana Machi 13,
2015 na Rais wa Misri, Abdel-Fattah El- Sisi, mjini Sharm El-Sheikh,
Misri.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, (katikati) akiwa na
baadhi ya viongozi kutoka mataifa mbalimbali wakati akiwa katika mkutano
wa Kiuchumi na maendeleo wa Misri, uliofunguliwa jana Machi 13, 2015 na
Rais wa Misri, Abdel-Fattah El- Sisi, mjini Sharm El-Sheikh, Misri
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Rais
wa Misri, Rais wa Misri, Abdel-Fattah El- Sisi, wakati walipokutana kwa
mazungumzo baada ya mkutano huo, uliofanyika jana Machi 13, 2015 mjini
Sharm El-Sheikh, Misri.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na
Wawekezaji wa Misri wanaotaka kuwekeza katika Sekta ya Viwanja Wilayani
Mkuranga, wakati alipokutana nao kwa mazungumzo leo, Machi 14, 2015
mjini Sharm El- Sheikh, Misri, alikohudhuria mkutano wa Kiuchumi na
maendeleo wa Misri, uliofunguliwa jana Machi 13, 2015 na Rais wa Misri,
Abdel-Fattah El- Sisi, mjini Sharm El-Sheikh, Misri.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na wageni
wake Wawekezaji wa Misri wanaoataka kuwekeza katika Sekta ya Viwanda
Wilayani Mkuranga, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika leo Machi 14,
2015 mjini Sharm El- Sheikh, Misri alikohudhuria mkutano wa Kiuchumi na
maendeleo wa Misri, uliofunguliwa jana Machi 13, 2015 na Rais wa Misri,
Abdel-Fattah El- Sisi, mjini Sharm El-Sheikh, Misri.
Picha na OMR
………………………………………………………………………………………………………
NA SHARM EL SHEIKH, MISRI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed
Gharib Bilal jana Machi 13, 2015 ameiwakilisha Tanzania katika Mkutano
wa Kimataifa wa Kiuchumi na Maendeleo nchini Misri. Mkutano huo
umeandaliwa na Rais wa Misri Mheshimiwa Abdel Fattah Al Sisi na
umehudhuriwa na viongozi karibu wote kutoka katika nchi za Kiarabu,
marais na viongozi wakubwa wa nchi mbalimbali za Afrika pamoja na wakuu
wa vyombo mbalimbali vya Kimataifa akiwemo pia Waziri wa Mmabo ya Nje wa
Marekani John Kerry.
Akizungumza katika Mkutano huo, Rais wa Misri aliueleza
ulimwengu kuwa Misri imepita jaribio kubwa na sasa iko imara tayari
kusonga mbele hivyo wale wote walio na nia ya kuwekeza nchini Misri
wafanye hivyo kwa kuwa serikali yake itashirikiana nao katika kuwalinda
wao na mali zao. Pia Rais Sisi alifafanua kuwa, nchi yake inarejesha
heshima yake iliyokuwa nayo zamani kutokana na mchango wake katika Umoja
wa nchi za Kiarabu huku pia akisisitiza kuwa Misri sasa inarejea Afrika
ambako anatambua kuna ndugu wa dhati.
Akihutubia mkutano huo Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Mohammed
Gharib Bilal aliishukuru Misri kwa kuialika Tanzania kuhudhuria mkutano
huo na akafafanua kuwa Tanzania inafurahia uamuzi wa Misri wa kujijenga
upya huku ikikumbuka historia ya kutaka kujiwekea nafasi yake katika
Afrika na katika nchi za Kiarabu.
“Mheshimiwa Rais, uitishaji wako wa mkutano huu mkubwa ni
kiashirio kuwa sasa Misri inajijenga upya na kwamba inarejesha heshima
yake katika Bara la Afrika, Nchi za Kiarabu na Dunia kwa ujumla,”
alisema Mheshimiwa Dkt Bilal na kuendelea kuwa:
“Tunakupongeza kwa uongozi thabiti uliouonesha hadi sasa ambapo
Misri inaonekana kuwa imara na thabiti. Uhusiano wetu ni wa kihistoria
hivyo Tanzania inakupongeza na inaahidi kushirikiana nanyi katika ujenzi
mpya wa Taifa lenu.”
Mheshimiwa Makamu wa Rais pia alitumia nafasi hiyo kuueleza
mkutano huo kuwa eneo ilipo Misri linaunganisha Afrika, Nchi za Kiarabu
na Ulaya na Tanzania nayo iko katika eneo la kitajiri kijiografia ambapo
ukiwekeza nchini Tanzania unakuwa unapata fursa za ziada za kuwekeza
katika nchi za Afrika Mashariki na nchi za Kusini mwa Afrika. “Ukiwekeza
Tanzania utakuwa na uhakika wa soko la watu wasiopungua milioni 400 na
nchi zetu ni lango la nchi zipatazo nane ambazo hazina bahari,”
mheshimiwa Makamu wa Rais alisema na kufafanua kuwa Tanzania
inakaribisha wawekezaji kama ambavyo Misri inafanya na zaidi akaeleza
kuwa fursa za uwekezaji Tanzania ni nyingi na hasa sasa ambapo
tunaelekea kuwa nchi ya uchumi wa kati.
Katika mkutano huu, Mheshimiwa Makamu wa Rais alipata nafasi ya
kukutana na Mheshimiwa Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi na kuzungumza
naye na kisha kuhudhuria mada ya kiuchumi iliyowasilishwa na Waziri Mkuu
wa Misri Ibrahim Mahlab. Mheshimiwa Makamu wa Rais na msafara wake
wanarejea nyumbani kesho tayari kuendelea na majukumu mengine ya
Kitaifa.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269