Breaking News

Your Ad Spot

Apr 12, 2015

DK.SHEIN : SERIKALI YA MAPINDUZI IMEDHAMIRIA KUREJESHA NA KUINUA HADHI YA MICHEZO ZANZIBAR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Umbuji Jape Mdumbu Ramadhan Fotokopi Mashine wakati hafla ya Sherehe ya kukabidhi vifaa vya Michezo kwa Timu 40 za Jimbo la Uzini vilivyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo Mohamed Raza katika Uwanja wa mpira Bambi leo. (Picha zote na Ikulu)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Viongozi mbali mbali wakati alipowasili katika viwanja vya Mpira Bambi katika sherehe ya kukabidhi vifaa vya Michezo kwa kwa Timu za Jimbo la Uzini leo,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akisalimiana na Viongozi mbali mbali wakati alipowasili katika viwanja vya Mpira Bambi katika sherehe ya kukabidhi vifaa vya Michezo kwa kwa Timu za Jimbo la Uzini leo, 
Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohamed Raza Daramsi akimkaribisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiwa mgeni rasmi kukabidhi vifaa vya michezo kwa Timu za Jimbo la Uzini leo katika uwanja wa Mpira Bambi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimkabidhi Kikombe Mwenyekiti wa Jimbo la Uzini CCM Ali Shaaban  wakati hafla ya Sherehe ya kukabidhi vifaa vya Michezo kwa Timu 40 za Jimbo la Uzini vilivyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo Mohamed Raza katika uwanja wa Mpira Bambi leo. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimkabidhi Mahmoud Ame seti ya jezi wakati hafla ya Sherehe ya kukabidhi vifaa vya Michezo kwa Timu 40 za Jimbo la Uzini vilivyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohamed Raza (kushoto) katika uwanja wa Mpira Bambi leo. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimkabidhi Mkuu wa Wilaya Kati Unguja Vuai Mwinyi Seti za jezi na vifaa vyengine kwa Timu za Wilaya yake wakati hafla ya Sherehe ya kukabidhi vifaa vya Michezo kwa Timu 40 za Jimbo la Uzini vilivyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo Mohamed Raza katika uwanja wa mpira Bambi leo. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alipokuwa akitoa nasaha zake kwa wanamichezo wa Jimbo la Uzini baada ya kukabidhi vifaa mbali mbali vya Michezo leo katika uwanja wa mpira Bambi vilivyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mohamed Raza Daramsi na kuwataka vijana hao kuvitunza na kuthamini mchamngo huo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alipokuwa akisalimiana na Mtoto Munira Khamis wa Bambi baada ya kumalizika kwa sherehe za utoaji wa Vifaa vya Michezo kwa Jimbo la Uzini leo vilivyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mohamed Raza. 

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amekabidhi vifaa vya michezo kwa timu za Jimbo la Uzini vilivyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe. Mohammed Raza na kusema kuwa hivi sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kurejesha na kuinua hadhi ya michezo hapa nchini.

Dk. Shein aliyasema hayo leo huko uwanja wa mpira wa Bambi, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo vya michezo kwa wanamichezo wa timu mbali mbali vikiwemo, mashine ya photokopi kwa skuli ya Umbuji, vikombe vitakavyoshindaniwa mashindano mbali mbali, seti za jezi kwa ajili ya timu za mpira wa miguu za Jimbo hilo, Afisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kati pamoja na vikundi vya mazoezi.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa ugawaji wa vifaa hivyo ni miongoni mwa  juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinazohakikisha kuwa michezo hapa Zanzibar inapewa hadhi na umuhimu wake inaostahiki na inatumika katika kujenga vijana wenye siha, nguvu, na vipaji mbali mbali.

“Nakupongezeni vijana kwa kujitokeza kwa wingi katika hafla hii ili kutudhihirishia ari, hamu na hamasa mliyonayo katika kuitikia wito wa kuifufua michezo hapa Zanzibar”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha kuwa Zanzibar inashiriki na kushinda mashindano mbali mbali katika ngazi za Kimataifa na kusisitiza kuwa michezo ni chachu ya maendeleo ambapo pia,hujenga udugu na mafahamiano miongoni mwa jamii.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe. Mohamed Raza kwa juhudi zake za kuendeleza michezo si kwa Jimbo la Uzini pekee bali kwa Zanzibar nzima katika nyakati mbali mbali na kusifu mashirikiano yaliopo na wananchi.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa Serikali imefanya jitihada mbali mbali za kuwatafuta vijana wenye vipaji vya michezo na baadae kuwaendeleza huku akiwaeleza wananchi na wanamichezo waliohudhuria hafla hiyo miongoni mwa mazungumzo waliozungumza hivi karibuni na wachezaji wakongwe wa Timu ya Barcelona ya Hispania wakati alipowaalika huko Ikulu kuwa mbali na mambo mengineyo ni kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza vipaji vya vijana.

Dk. Shein alitoa nasaha kwa wanamichezo hao na kuwataka kuendeleza na kuongeza juhudi katika michezo kwani dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa vipaji viliopo vinakuzwa kwa njia yoyote na vinatumika kwa manufaa ya nchi.

Pia, aliwakumbusha wananmichezo hao umuhimu wa nidhamu katika michezo na kusisitiza kuwa mwana michezo bora ni yule mwenye nidhamu na tabia njema ikiwa ni pamoja na nidhamu akiwa kiwanjani, nyumbani na popote pale alipo.

Aidha, Dk. Shein alitoa wito kwa mashabiki, wachezaji na wazalendo kupenda timu za nyumbani na kufuatilia kwa karibu ligi zinazochezwa hapa nchini na kuwataka vijana wa Jimbo hilo kuimarisha michezo.
Dk. Shein ambaye pia, ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, alisema kuwa katika Ilani ya CCM sekta ya michezo imepewa kipaumbele na ndio maana juhudi zimekuwa zikichukuliwa katika kuimarisha miundombinu ya michezo hapa nchini na kugusia dhamira ya Serikali ya kuujenga uwanja wa Mao tse tung.

Pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Raza kwa kutekeleza kikamilifu mambo 12 katika Jimbo hilo ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake sambamba na kuwapelekea wananchi hao maendeleo ya harakaharaka.

Mapema Mhe. Raza alieleza kuwa hatua hiyo ni kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, viongozi na wananchi pamoja na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwani anatambua kuwa uongozi ni dhamana na mashirikiano na wananchi.

Alisema kuwa uongozi ni kuwatumikia wananchi na yeye yuko tayari kuendelea kuwatumikia wananchi ikiwa ni pamoja na kuwaunga mkono katika kuendeleza miradi yao mbali mbali ya maendeleo na kueleza kuwa tayari ameshatekeleza ahadi zake kwa zaidi ya asilimia mia moja katika Jimbo hilo.

Aidha, alieleza kuwa wananchi wa Jimbo la Uzini wako tayari kukitumikia chama chao cha CCM, pia, alieleza kuwa ataviimarisha zaidi viwanja vyote vitatu vya mpira wa miguu ambavyo ameshaviwekea taa za kisasa kwa ajili ya kucheza wakati wa usiku na kuahidi kuzipa skuli zote za Jimbo hilo vifaa kama hivyo vya michezo.
Nae Mkuu Mkoa wa Kusini Unguja Dk. Idriss Muslim Hija alipongeza juhudi za Mhe. Raza katika Mkoa huo.

Vifaa hivyo vimegharimu Tsh. Milioni 22.5 ambavyo vilikabidhiwa kwa timu 40 za Jimbo hilo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages