Tunapoelekea
kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka ambayo inaanza kesho Ijumaa Kuu,
Jeshi la Polisi nchini, linatoa tahadhari kwa wananchi, kuwa makini
katika suala zima la ulinzi na usalama wa maisha na mali zao. Uzoefu
unaonyesha kwamba, katika kipindi kama hiki cha sikukuu kuna baadhi ya
watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo vya uhalifu. Hata hivyo,
Jeshi la Polisi katika mikoa yote limejipanga vizuri kwa kushirikiana
na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba hakuna
vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza na pale vitakapoonyesha
dalili ya kujitokeza viweze kudhibitiwa kwa haraka.
Aidha, ulinzi umeimarishwa kwenye
maeneo yote, yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za
starehe na maeneo mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya
watu.
Vilevile, Jeshi la Polisi linawataka madereva na watu wote
watakaokuwa wakitumia barabara, kuwa makini na kuzingatia sheria za
usalama barabarani, kuepuka kwenda mwendo kasi, kujaza abiria kupita
kiasi na kutumia vilevi wawapo kazini. Wamiliki wa kumbi za starehe
wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao hususani katika uingizaji wa
watu kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya
fedha kwa kujaza watu kupita kiasi.
Aidha, wazazi wawe makini na
watoto wao, kutokuwaacha watembee peke yao ama kwenda disko toto bila
kuwa chini ya uangalizi wa watu wazima ili kuepusha ajali na matukio
mengine yanayoweza kusababisha madhara juu yao.
Wananchi wakumbuke kutokuacha
makazi yao bila uangalizi na endapo italazimu kufanya hivyo watoe
taarifa kwa majirani zao, na pale wanapowatilia mashaka watu
wasiowafahamu watoe taarifa haraka kwenye vituo vya polisi vilivyo
karibu yao, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka.
Mwisho, Jeshi la Polisi linapenda kuwashukuru wale wote ambao
tayari wamefunga kamera za CCTV katika maeneo yao ya biashara hususani
yale yanayokuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu, yakiwemo maduka,
mahoteli na maeneo ya benki. Jeshi la Polisi linaendelea kuwasisitiza
ambao bado hawajaweka kamera hizo, kuweka ili ziweze kusaidia kubaini
wahalifu na hata kurahisisha ukamataji wa wahalifu hao endapo uhalifu
unatokea.
Tunawatakia watanzania wote Pasaka njema.
Imetolewa na:-
Advera Bulimba -SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269