JESHI la Polisi mkoani Kagera, linawashikilia watu wawili
wakituhumiwa kufukua kaburi la marehemu Baltazar John mwenye ulemavu wa
ngozi (albino) na kuchukua viungo viungo vyake.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Henry Mwaibambe, tukio
hilo limetokea 27 Machi mwaka huu, ambapo watuhumiwa walinaswa katika
nyumba ya kulala wageni ya Ford iliyopo eneo la Kyaka wilayani Missenyi.
Watuhumiwa hao ni Laston Faustine (41) mkazi wa Lukulaijo na January
Korongo (43) wakazi wa Kadengesho wilayani Karagwe mkoani Kagera, ambapo
walikutwa na mifupa mitatu ya binadamu.
Kamanda Mwaibambe amesema “katika mahojiano mtuhumiwa wa kwanza-
Faustine, alituambia kuwa alipewa viungo hivyo na Korongo kwa ajili ya
kuviuza Sh. 20 milioni.”
Ameongeza kuwa, Korongo alipohojiwa amekiri kwamba alifukua kaburi la
mjomba wake aitwae Baltazari John (albino), ambaye alifariki mwaka 1991
na mwili wake kufukuliwa 2009.
“Baada ya kumuhoji zaidi mtuhumiwa huyo, alikubali kuongozana na
polisi hadi nyumbani kwake ambapo alionyesha fuvu la kichwa, mifupa
mitatu ya miguu pamoja na mifupa ya sehemu mbalimbali ambayo ilikuwa
imefungwa kwenye mfuko nje ya nyumba yake.
“Ili kujiridhisha, jeshi liliomba kibali cha mahakama wilayani
Karagwe ili kufukua kaburi hilo kuhakikisha kama kweli kuna mabaki ya
mwili huo. Tulipofukua hakuna kilichopatikana,” amesema kamanda.
CHANZO: BUKOBA WADAU BLOG
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269