Na Mwandishi Maalum, New York
Jumuiya ya Kimataifa inajiaanda kwa mkutano maalum na wa aina yake kufanyika, ambapo nchi wanachama watakutana na kujadiliana kwa kina kuhusu changamoto na adhari kubwa zitokanazo na biashara haramu na matumizi ya dawa za kulevya.
Jumuiya ya Kimataifa inajiaanda kwa mkutano maalum na wa aina yake kufanyika, ambapo nchi wanachama watakutana na kujadiliana kwa kina kuhusu changamoto na adhari kubwa zitokanazo na biashara haramu na matumizi ya dawa za kulevya.
Mapema wiki iliyopita, wajumbe wanaoziwakilisha nchi zao hapa Umoja wa Mataifa, walikuwa na mkutano wa siku moja ambao ulikuwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano huo maalum utakaofanyika mwezi Aprili 2016.
Mkutano huo wa maandalizi uliofanyika hapa Umoja wa Mataifa na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwamo mawaziri kadhaa kutoka nchi hasa za Amerika ya Kati ambako nchi nyingi zinakabiliwa na changamoto kubwa ya biashara hiyo, uliandaliwa na Bw. Sam Kutessa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Katika majadiliano ya mkutano huo , ilidhihirika wazi kwamba hakuna nchi hata moja duniani iwe tajiri au maskini ambayo haijakumbwa na janga la biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
“ Hakuna nchi ambayo imepona kutokana na biashara hii yenye thamani ya mabilioni ya dola. Licha ya juhudi kubwa na raslimali nyingi ambazo mataifa yanatumia kukabiliana na janga hili, lakini tatizo linaendelea kukua” akasema Bw. Sam Kutessa wakati akifungua mkutano huo.
Naye Naibu Katibu Mkuu Bw, Jan Eliason naye akizugumza kwenye mkutano huo. Pamoja na mambo mengine alieleza kwamba, mitandao ya kihalifu inazidi kustawi kutokana na biashara hiyo na kuongeza kuwa mitandao hiyo inaharibu mifumo imara ya ustawi wa kijamii, pamoja na kuyumbisha utawala wa kidemokrasia.
Kama hiyo haitoshi Naibu Katibu Mkuu, ameongeza kuwa biashara haramu ya dawa za kulevya inatumika kama vyanzo vya mapato kwa makundi ya wanagambo wenyenye silaha na hivyo kuwa tisho kubwa katika mataifa ambayo yanamigogoro.
Kwa sababu hizo na nyingine nyingi zilizobainishwa na wajumbe walioshirikia mkutano huo, wameshauri na kupendekeza kwamba, kwa kuwa tatizo la dawa za kulevya ni la dunia nzima, basi utashi wa kisiasa, ushirikiano, uwazi na ukweli utahitajika sana katika mkutano huo maalum utakaofanyika mwakani.
Baadhi ya wachangiaji walikwenda mbali Zaidi kwa kubainisha kuwa, katika kulikabili tatizo la dawa za kulevya haitoshi nguvu kuelekezwa kule zinakozalishwa dawa hizo bali nguvu hizo pia zinatakiwa kuelekezwa pia katika nchi ambazo zina matumizi makubwa ya dawa.
Aidha wachangiaji wengine walitaka pia uwazi na uwajibikaji katika udhibiti wa vyanzo vya fedha chafu ambazo zinatumika katika biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya. Ikiwa ni pamoja na udhibiti wa magenge ya wahalifu wanaomiliki na kuendesha biashara hiyo.
Vile vile wazungumzaji wengi pia walizungumzia namna gani biashara na matumizi ya dawa za kulevya inavyoendelea kushamiri licha ya juhudi mbalimali za kimataifa na kimataifa za kuikabili.
Na kwamba kuendelea kwa biashara hiyo ambayo tayari imeshaathiri na kuendelea kuathiri maisha ya watu wengi hususani vijana, wanawake na watoto ni janga la dunia.
Wengi wamekiri bayana kwamba si rahisi sana kumaliza tatizo na biashara haramu na matumizi ya dawa hizo kutokana na ukweli kwamba linawashirika na wadau wengi na ni biashara yenye kubeba uzito mkubwa kiasi kwamba si rahisi kuimaliza mara moja.
Wapo baadhi ya wajumbe waliogusia kuhusu adhabu kali zikiwamo za kuuawa kwa watu wanaokamatwa wakisafirisha au kuuza dawa hizo, na kwamba adhabu kama za kifo licha ya kwamba ni ukiukwaji ya haki ya mtu kuishi lakini pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu na kwamba hukumu ya adhabu ya kifo haijapunguza kasi ya biashara hiyo au matumizi yake.
Wengine walielezea haja na umuhimu ya kutowanyanyapaa watu ambao wameathirika na dawa hizo au hata kuwatenga kwa kile walichosema wanachohitaji waathirika hao ni msaada wa matibabu yatakayowawezesha kuondoka na dhahama hiyo.
Akichangia majadiliano hayo, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, alisema kama ilivyo kwa nchi nyingine, Tanzania nayo haijapona na janga la biashara na matumzi ya dawa za kulevya.
Akasema Tanzania imekuwa njia ya kupitishia dawa hizo kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine, na kwamba katika usafirishaji huo, kiasi cha dawa hizo hubakia nchini na hivyo kuathiri sehemu kubwa ya jamii ya watanzania ambao tayari wanakabiliwa na umaskini wa kila aina.
Akaongeza kuwa, tatizo la dawa za kulevya limekuwa kikwazo katika jitihada za kuwapatia watanzania maisha yenye hadhi kutokana na kwamba tatizo hilo linaathiri nguvu kazi inayohitajika katika ujenzi na uendeshaji wa maendeleo ya jamii na ukuaji wa uchumi.
Kama hiyo haitoshi, Balozi Manongi ameeleza kwamba, dawa za kulevya zimekuwa kichocheo cha ongezeko la vitendo vya uhalifu ikiwa ni pamoja na uhalifu wa wanyamapori na misitu, ugaidi na pia kuongeza mzigo katika huduma za afya.
“Lengo letu ni kuzuia uingiaji wa dawa za kulevya kwenye ndani ya nchi yetu, lakini uzoefu umetuonyesha hii ni kazi kubwa na ngumu na hasa kutokana na muingiliano baina ya mataifa ni kwa sababu hii, tunashirikiana na nchi jirani nasi na washirika wengine katika kuboresha jitihada za kukabiliana na changamoto hii” akasema Balozi Manongi.
Akatilia mkazo umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, pamoja na mipango mbadala inayoweza kutoa fursa kwa jamii kufanya shughuli nyingine badala ya kutegemea biashara ya dawa za kulevya.
Mkutano wa mwakani unafanyika ikiwa miaka kadhaa imepita tangu ulipofanyika mkutano mwaka 2008 huko Vienna, ambapo kulipitishwa Tamko la Kisiasa na Mpango wa Utekelezaji juu ya ushirikiano wa uwiano ili kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya. Mkutano huo wa mwakani utafanya tathmini ya tamko hilo pamoja na masuala mengine.
Washiriki wakiwa kwenye mkutano huo kuhusu dawa za kulevya uliofanyika mwishoni mwa wiki hapa Umoja wa Mataifa na kuwakutanisha wadau mbalimbali.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269