Vijana mkoani Lindi wametakiwa
kuwa wazalendo na kutobaguana bali wasambaze upendo na kujiona wote ni
sawa kwa kufanya hivyo wataondoa chuki na kudumisha amani, mshikamano na
umoja katika jamii inayowazunguka.
Mwito huo umetolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akifungua klabu zalendo zilizopo katika Manispaa ya Lindi.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kama jamii itajenga tabia ya ubaguzi
italeta chuki na upendo utatoweka na hivyo kusababisha vurugu
zitakazopoteza amani iliyopo.
Alisema uzalendo ni kiini cha
maendeleo hivyo huwezi kuwa mzalendo kama hupingi rushwa na matumizi ya
madawa ya kulevya, hutunzi mazingira, hushiriki kuchangia utoaji wa damu
salama na kutokuchangamkia fursa mbalimbali za maendeleo zilizopo
katika jamii yako.
Mama Kikwete alisema, “Leo hii
nimezindua klabu zalendo, Mzalendo ni mtu mwenye huruma na mtu anayeona
thamani ya kitu alichonacho tunzeni vitu mlivyonavyo ikiwemo Amani ya
nchi yetu na mjitoe kufanya kazi kwa bidii ili muweze kupata maendeleo.
Aidha Mama Kikwete aliwahimiza
wanafunzi kujitendea haki kwa kusoma kwa bidii hadi elimu ya chuo kikuu
kwa kufanya hivyo wataweza kuajiriwa na kujiajiri katika katika fani
mbalimbali na kujiletea maendeleo katika mkoa wao wa Lindi.
Akisoma historia fupi ya klabu
zalendo Mwalimu Mwajuma Malugu ambaye ni Mwenyekiti alisema lengo kuu la
kuanzishwa kwa klabu hiyo ni kuutetea na kuulinda muungano wa
Tanganyika na Zanzibari ndiyo maana wanatumia namba za
#26464#ikimaanisha tarehe 26 mwezi wa 4 mwaka 1964 siku ya muungano
Aliyataja malengo mengine kuwa ni
kuhamasisha wanafunzi na vijana waliopo mtaani kuwa wazalendo na
kuipenda nchi yao kwa kufanya hivyo wataepukana na mambo yasiyofaa kwa
maslai ya nchi yao.
“Mafanikio tuliyoyapata ni kujenga
umoja na ushirikiano, kuongeza idadi ya wanachama na hii inatokana na
kufunguliwa kwa matawi mengine ya uzalendo mashuleni na mitaani,
kuongeza na kupanua uelewa kwa wanafunzi na raia kuhusu klabu ya
uzalendo, kuwahamasisha watu kuwa wazalendo na kujitoa katika uchangiaji
wa damu, kupinga rushwa, madawa ya kulevya pamoja na kulinda Amani ya
nchi.
Mwalimu Mwajuma alizitaja
changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni uhaba wa fedha kwa ajili ya
kuandaa makongamao na mabonanza yatakayosaidia kuimarisha harakati zote
za klabu ya uzalendo na kushindwa kutuma wawakilishi katika mikutano na
makongamano ya wanaklabu ngazi ya taifa
Pia kikundi kimekosa semina kwa wanaklabu hali inayoplekea wanachama kukosa uelewa wa kutosha kuhusu madhumuni ya klabu hiyo.
Klabu zalendo ilianzishwa na
walimu wa Shule ya Sekondari Lindi katikati mwa mwaka jana hadi sasa
inawanachama 1450 kutoka shule za Sekondari Mkonge, Angaza, Ngongo,
Ng’apa, Chikonji, Mingoyo, Kineng’ene , chuo cha ufundi VETA na walimu
wa shule za msingi pamoja na wanafunzi wao.
Pia klabu hiyo imehusisha vijana
kutoka mtaani wanaofanya kazi za udereva wa pikipiki maarufu kama
bodaboda, wavuvi na wanavikundi vya Sanaa.
Mama Kikwete aliahidi kukipatia
kikundi hicho mipira 20 na jezi seti 10 kwa ajili ya wanafunzi wa shule
za msingi na Sekondari ambao watashiriki katika mashindano mbalimbali
`na kuangalia utaratibu wa kuwapatia mradi ambao utawasaidia kuwainua
kichumi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269