Breaking News

Your Ad Spot

May 9, 2015

SHERIA YA MAKOSA YA MITANDAONI IMESHASAINIWA NA RAIS KIKWETE

TAARIFA YA MHE. PROF. MAKAME MBARAWA (MB), WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA KUHUSU SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAO YA MWAKA 2015 KWA WAANDISHI WA HABARI  TAREHE 8 MEI, 2015
____________________________

Ndugu Wananchi,
Ndugu Waandishi wa Habari,
 Kukua kwa kasi kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kumeleta mafanikio mengi katika nyanja mbalimbali za maisha ya kila siku. Mafanikio haya yanathibitika kwa kuongezeka kwa huduma za mawasiliano, huduma za kifedha na matumizi ya mitandao ya kijamii.

Aidha, mafanikio hayo yameleta changamoto nyingi katika jamii. Changamoto hizo ni pamoja na kuibuka kwa makosa mapya ya jinai na pia mbinu mpya za kutenda makosa ya zamani.

Ndugu Wananchi,
 Makosa hayo hujumuisha uhalifu wa Mitandao ambao simu za mkononi, kompyuta au mifumo ya kompyuta hutumika kama nyenzo za kutenda uhalifu huo.
 
Mifano ya makosa hayo ni kama ifuatavyo:
1. Kumekuwepo na wizi wa fedha kwa njia ya mtandao,
2. Kumekuwepo na ugaidi kupitia kwenye mitandao,
4. Kuwepo na mmomonyoko mkubwa wa maadili,
3. Kumekuwepo na uharibifu wa miundombinu muhimu ya Taifa kwa makusudi, Kwa mfano kukatwa kwa makusudi Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. [Hii imepelekea kuisababishia Serikali na Sekta binafsi hasara na kusababisha kukosekana kwa huduma mbalimbali za kiuchumi na za kijamii].

Ndugu Wananchi,
Kama mnavyofahamu kwenye kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililopita, Serikali ilipeleka Mswada wa kutunga sheria ya uhalifu wa mtandao (Cyber Crimes) na Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge.

Madhumuni ya kutunga sheria hii kama sheria nyingine zilizotungwa na Bunge hapa nchini ni kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii hasa kwenye matumizi ya TEHAMA.

Ndugu Wananchi,
Ndugu Wandishi wa Habari,
 Tanzania siyo nchi ya kwanza kutunga sheria  kama hii. Kuna nchi mbalimbali duniani zimetunga sheria kama hii, kwa mfano nchi ya Uingereza (UK Computer Misuse Act, 1990), India (IT Act, 2000), Malaysia (Computer Crime Act 2. ) Uganda (Computer Misuse Act, 2010), Korea ya Kusini (Information and Communications Network Act na Information and Communication Infrastructure Protection Act),  Singapore (The Computer Misuse and Cybersecurity Act), Maturities (Computer Misuse and Cybercrime Act, 2003), Afrika ya Kusini, Marekani (Computer Fraud and Abuse Act, 1984)  na nyingi nyinginezo.

Ndugu Wananchi sasa mmepata pahala pa kukimbilia, kwani mukitendewa uhalifu kupitia mitando sheria hii itawasaidia kupata haki zenu. Ninawashangaa sana wale wanaopinga kutungwa kwa sheria hii hapa Tanzania.

Haikubaliki hata kidogo kuona Wantanzania wengine wanakumbana na uhalifu kupitia Kwenye mtandao na wachache kwa faida zao binafsi wanataka Serikali ikae kimya.

Sheria hii haina tofauti na sheria za nchi nyingine nilizozitaja hapo awali. Sheria hii imetungwa kwa mazingira ya nchi yetu ya Tanzania.

Ndugu Wananchi,
 Sheria hii  sasa imeshasainiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete baada ya kupitia hatua zote za kuiboresha.

Hatua ya MWISHO ilikuwa ni ile ya marekebisho yaliyofanywa na Bunge ambapo baadhi ya vifungu vilivyolalamikiwa  viliboreshwa.

Kwa hivyo wananchi sasa tuipokee sheria hii na kuitumia. Sheria hii ni nzuri na itasaidia sana kuwalinda wananchi, mitandao na miundombinu yetu muhimu ya kitaifa.

Katika kuitumia sheria hii na kama ilivyo kwa sheria nyingine yoyote, patakapoonekana kuna mapungufu, marekebisho yatafanyika. Kwa hivyo kama kuna mtu yeyote mwenye maoni ya kuiboresha sheria hii anaweza kuleta  maoni Serikalini hapa Wizarani.

Ninarejea tena: Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Mabalozi, wadau mbalimbali wa  Sekta ya Mawasiliano, waandishi wa habari, wana-bloggers, na wananchi kwa ujumla kama kuna yeyote mwenye maoni ya kuboresha kifungu chochote cha sheria hii alate maoni hayo hapa Wizarani.

Serikali kupitia Wizara yangu itapokea maoni au ushauri huo, tutayatafakari na kuyafanyia kazi kwa kina. Haitosaidia sana kusema huko pembeni, jukwaa zuri la kuleta maoni ni kupitia Wizara yangu.

Ndugu Wananchi, na
Ndugu Waandishi wa Habari,
Hii haitokuwa sheria ya kwanza kufanyiwa marekebisho kama itaonekana kuna umuhimu wa kufanya hivyo.

Ahsanteni na Ninawashukuru sana kwa  kunisikiliza.
S

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages