Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
(MNH), Profesa Mohamed Janabi akizungumza na mabalozi wanaowakilisha
nchi zao hapa nchini kuhusu shughuli za upasuaji wa moyo zinazofanywa na
taasisi hiyo. Profesa Janabi amezungunza na mabalozi hao katika Hoteli
ya Serena jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Afrika Kusini nchini
Tanzania, Thami Mseleku (kushoto) na Balozi wa Rwanda hapa nchini,
Eugene Kayihura (kulia) wakimsikiliza Profesa Mohamed Janabi wakati
akieleza mambo ambayo watu wanapaswa kuzingatia ili kuepuka shinikizo la
damu kwenye mkutano uliofanyika Hoteli ya Serena jijini Dar
es Salaam.
Balozi wa Zambia nchini Tanzania,
Judith Kangoma (kulia) na mwenzake wa Malawi, Hawa Ndilowe wakimsikiliza
Profesa Mohamed Janabi.
Picha ZOTE kwa Hisani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)
……………………………………………………………………………….
Dar es Salaam, Tanzania. Mabalozi
wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania wameipongeza Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa
kuanzisha huduma ya upasuaji wa moyo.
Mabalozi hao wamefurahishwa na huduma hiyo na kueleza kwamba watawashauri raia wao kwenda kupatiwa matibabu kwenye taasisi hiyo.
Balozi wa Zimbabwe nchini Tanzania, Balozi Edzai Chimonyo
amesema kwamba wamefurahishwa na juhudi za taasisi hiyo na kwamba
wanapenda kujua jinsi ya kuzuia matatizo ya moyo.
“Napenda kujua ni vipi mtu anaweza kuzuia matatizo ya moyo,” amesema Balozi Chimonyo.
Naye Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Thami Mseleku
amesema kwamba ataitumia taasisi hiyo kupima afya yake na kwamba endapo
atatozwa fedha kwa ajili kupatiwa matibabu yupo tayari kutoa ili
kusaidia wagonjwa wa kawaida wanaopatiwa matibabu hapo.
Akizungumza na mabalozi hao, Kaimu Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa
Mohamed Janabi amesema ili watu wasipate shinikizo la damu wanapaswa
kufanya mazoezi, kupima afya mara kwa mara na kuchunguza endapo familia
ina tatizo la shinikizo la damu.
Profesa Janabi amesema kwamba endamba mabalozi hao watazingatia hayo wataepuka kupata shinikizo la damu.
Awali Profesa Janabi amewaeleza mabalozi hao huduma zinazotolewa
na taasisi hiyo ikiwamo kufanya upasuaji kwa watoto 37 hivi karibuni
wakimo watoto wawili kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC).
Profesa Janabi amesema upasuaji wa moyo unaofanywa na hospitali
hiyo unasaidia kupunguza gharama za matibabu endapo wangekwenda kutibiwa
India.
Amesema gharama za mgonjwa kufanyiwa upasuaji wa moyo India ni
kuanzia Dola 10,000 hadi 12,000 wakiwamo ndugu wanaomsindikiza mgonjwa
nchini humo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269