Mahujaji
wengine wawili kutoka Tanzania ambao walikuwa hawaonekani tokea ajali
ya kukanyagana kwa mahujaji ilipotokea Makkah nchini Saudi Arabia tarehe
24 Septemba 2015 wametambuliwa kuwa, ni miongoni mwa mahujaji
waliofariki dunia.
Kutambuliwa
kwa mahujaji hao kunafanya idadi ya mahujaji wa Tanzania waliopoteza
maisha katika ajali hiyo kufikia ishirini na saba (27). Majina kamili ya
mahujaji hao ni Bw. Juma Yussuf Bakula na Bw. Ahmad Awadh Namongo
kutoka Kikundi cha Ahlu Dawaa.
Hadi sasa mahujaji kumi na tatu (13) kutoka Tanzania bado hawajulikani walipo na jitihada za kuwatafuta bado zinaendelea.
Kwa
upande wa mahujaji wanne ambao walikuwa wanapatiwa matibabu kutokana na
kuugua au kujeruhiwa, mmoja wao ni Bw. Mustafa Ali Mchina ambaye
alikuwa amelezwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika mji wa
Maddinah alifariki dunia tarehe 17 Oktoba 2015 na kuzikwa Maddinah siku
hiyo hiyo.
Bi.
Mahjabin Taslim Khan ambaye alijeruhiwa katika ajali hiyo na
kusababisha kukatwa mguu wake amepata nafuu na alirejea nchini tarehe 20
Oktoba 2015. Mwingine ni Bi. Hidaya Mchomvu ambaye alijeruhiwa pia bado
yupo hospitali akiendelea kupatiwa matibabu.
Hujaji
wanne ni Bw. Ahmed Abdallah Jusab ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa
moyo alifanyiwa upasuaji wa kumuwekea kifaa cha kuongeza mapigo ya moyo
tarehe 19 Oktoba 2015 na alitarajiwa kurejea nchini tarehe 21 Oktoba
2015.
Serikali
ya Saudi Arabia inaendelea kutoa taarifa zaidi za kuwatambua mahujaji
waliofariki dunia au kujeruhiwa katika ajali hiyo na Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa itaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu
wahanga wa ajali hiyo kadri itakapokuwa inazipokea.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
22 Oktoba, 2015
|
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269