Serikali
imetoa ufafanuzi kuhusu ukomo wa madaraka ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na mwisho wa uhai wa Baraza la Mawaziri kwa kadri
Tanzania inavyoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaofanyika Jumapili, Oktoba
25, mwaka huu, 2015.
Taarifa
iliyotolewa jioni ya leo, Jumatano, Oktoba 21, 2015, Ikulu, Dar es
Salaam na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Yohana Sefue
imesema kuwa Serikali imetoa ufafanuzi huo kuwasaidia wananchi kuelewa
maelekezo na matakwa ya Katiba na Sheria kuhusu ukomo wa madaraka ya
Rais na mwisho wa Baraza la Mawaziri kufuatia mijadala ya karibu katika
vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Taarifa
hiyo imekariri Ibara ya 42(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inasema kuwa ukiacha sababu nyingine, mtu
anayechaguliwa kuwa Rais atashika madaraka ya kiti cha Urais hadi Rais
Mteule atakapoapishwa.
Ibara
hiyo ya 42(3) inasema: ”Mtu anayechaguliwa kuwa Rais, atashika kiti cha
Rais hadi – (a) siku ambako mtu anayemfuatia katika kushika kiti hicho
atakula kiapo cha Rais.”
Taarifa
hiyo imesema: “Hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Rais anaendelea kuwa Rais, akiwa na madaraka na mamlaka yote
na kamili yanayoambatana na nafasi hiyo, hadi Rais Mteule anakapokula
kiapo cha Urais. Hivyo, ni vyema wananchi waelewe kuwa hakutatokea
wakati wowote ambapo hakuna Rais na Amiri Jeshi Mkuu mwenye mamlaka
kamili na aliye tayari kuyatekeleza mamlaka hayo. Lengo ni kuhakikisha
kuwa haitokei wakati wowote nchi yetu ikakosa Rais na Amiri Jeshi Mkuu.”
Imesisitiza
taarifa hiyo: “Madaraka na mamlaka ya Rais yapo, na hayapugui kwa namna
yoyote ile, hata baada ya Uchaguzi Mkuu, mpaka Rais Mteule
atakapoapishwa.”
Kuhusu
ukomo wa Baraza la Mawaziri, taarifa imefafanua kuwa kwa mujibu wa
Ibara ya 57(2) ya Katiba, Waziri na NaibuWaziri ataendelea kushikilia
mamlaka ya nafasi yake hadi, ukiacha sababu nyingine, Rais mteule
atakapoapishwa.
Ibara
hiyo 57(2) inatamka: “Kiti cha Waziri au NaibuWaziri kitakuwa wazi
litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo – (f) Ukiwadia wakati wa Rais
Mteule kushika madaraka ya Rais, basi mara tu kabla ya Rais Mteule
hajashika madaraka hayo.”
Taarifa
hiyo imeongeza kuwa Mawaziri na NaibuMawaziri wanaendelea kushikilia
nafasi zao, wakiwa na madaraka na mamlaka kamili yanayoambatana na
nyadhifa zao hadi mara tu kabla ya Rais Mteule hajashika madaraka.
Imemalizia
taarifa hiyo: “ Naomba vyombo vya habari, vyenye jukumu la kuelimisha
jamii, kuwaelewesha Watanzania kuhusu utaratibu huu wakubadilishana
madaraka kati ya awamu moja ya uongozi wa nchi na nyingine. Madaraka na
mamlaka ya Rais yapo, na hayapungui kwa namna yoyote ile, hata baada ya
uchaguzi Mkuu mpaka Rais Mteule atakapoapishwa.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
21 Oktoba, 2015
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269