Mjumbe wa kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamesema watakwenda mahakamani kupinga matokeo ya ubunge majimbo ya; Iringa Mjini, Mikumi, Ndanda na Kawe.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mjumbe wa kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba amesema kuwa CCM haijaridhishwa na utaratibu wa ukusanyaji na ujumlishaji wa matokeo katika baadhi ya majimbo.
Taarifa yote soma hapa chini...
MALALAMIKO YA CCM KUHUSU MATOKEO KWENYE BAADHI YA MAJIMBO CCM inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa wana-CCM na kwa umma:
Chama cha Mapinduzi hakijaridhishwa na utaratibu wa kukusanya na kujumlisha matokeo kwenye baadhi ya majimbo. Katika majimbo manne kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi, hasa katika kujumlisha matokeo, uliopelekea wabunge wa upinzani kutangazwa washindi.
Majimbo hayo ni Iringa Mjini, Mikumi, Ndanda na Kawe. Wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo haya wamevuruga uchaguzi. Kutokana na utata uliokuwa umejitokeza wakati wa zoezi la kujumlisha kura, CCM iliomba kura zihesabiwe upya lakini ikanyimwa haki hiyo ya msingi ambayo iko kwenye sheria.
Kwenye baadhi ya majimbo, ikiwemo Nyamagana, wapinzani walipewa haki ya kura kuhesabiwa upya. Kwa msingi huo, CCM imeamua kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi katika majimbo haya.
Tunataka sote tujiridhishe kwamba utashi wa wananchi umeheshimiwa. Bado tunaendelea kukusanya taarifa za maeneo mengine kama kulikuwa na ukiukwaji mkubwa uliobadilisha matakwa ya wapiga kura.
Hata hivyo, tunakiri kwamba kwenye maeneo mengi tulikopoteza viti vya Ubunge, tumepoteza kihalali, hatuna malalamiko, tunaheshimu maamuzi ya wananchi, na tutafanya tathmini baada ya uchaguzi ili tubaini makosa na kuyarekebisha.
MAONI YA WAANGALIZI WA UCHAGUZI
CCM imepokea maoni ya awali ya waangalizi wa uchaguzi. Tumefarijika kwamba karibu wote wametoa kauli ya pamoja kwamba uchaguzi huu ulikuwa wa haki na huru, uliofanyika kwa uwazi na kwa amani – na kwamba changamoto zilizojitokeza ni ndogo na zimetokea katika maeneo machache kiasi zisingeweza kubadilisha matokeo ya uchaguzi yanayotangazwa sasa.(P.T)
Tumepokea
mapendekezo waliyoyatoa kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha
mchakato wa uchaguzi kwa miaka ijayo, na hivyo kuimarisha demokrasia
nchini mwetu. Kwa kauli za waangalizi hawa, kwamba, kwa jinsi uchaguzi
ulivyoendeshwa, matokeo yanayotangazwa sasa ni kielelezo sahihi cha
utashi wa Watanzania kuhusu viongozi wanaowataka.
MALALAMIKO YA UKAWA
Tumesikia
malalamiko ya viongozi wa UKAWA kupitia mkutano wao na waandishi wa
habari jana. Tumeshangazwa na kauli kwamba hawakubali matokeo ya Urais
yanayotangazwa na Tume. Hata hivyo, matokeo ya Ubunge wanayakubali na,
kule wanakoshinda, wanayasheherekea.
Tunashangazwa
kwasababu Tume iliyoandaa uchaguzi wa Rais ni hiyo hiyo iliyoandaa
uchaguzi wa Wabunge, wasimamizi ni walewale, vituo ni vilevile, na
sheria na taratibu zilizotumika ni zilezile. Hata fomu ya matokeo
walizosaini wakala wao kwenye vituo vya kupiga kura, zimegawanywa katika
sehemu (columns) tatu: Urais, Ubunge na Udiwani.
Mawakala
wao walisaini fomu hizo kwenye vituo vya kupiga kura. Wameanza kuwa na
matatizo na matokeo haya baada ya kuona mwelekeo wa kushindwa. Kama
mwelekeo ungekuwa tofauti, wangekuwa na imani na Tume, wasimamizi na
taratibu zote.
Tunaomba
ifike pahala sasa kwamba, katika kuijenga demokrasia yetu na
kuliimarisha taifa letu, tuanze utamaduni mpya wa anayeshindwa kunyanyua
simu kumpigia anayeshinda na kumpongeza.
Nafasi ya
mwisho aliyonayo Mgombea wa UKAWA kuendelea kujijengea heshima katika
jamii yetu, na kuwa mwanademokrasia, ni kwa kufanya hivyo siku Dkt.
Magufuli atakapotangazwa mshindi.
Kwetu
sisi CCM, kuchagua wagombea bora na kuwanadi na kutengeneza sera bora na
kuzinadi, pamoja na rekodi yetu katika uongozi wa nchi, ndio njia zetu
pekee za ushawishi. Katika uchaguzi huu, wananchi wamefanya maamuzi yao
kwa uhuru na utashi, ikiwemo kuwaangusha mawaziri sita ambao
tuliwasimamisha kama wagombea wetu katika majimbo mbalimbali. Nguvu na
utashi wa wananchi umejidhihirisha katika uchaguzi huu.
Mchakato
wa uchaguzi sasa unakaribia kufikia ukingoni, tutawapata madiwani,
wabunge na Rais, tunapaswa kuendelea na maisha na tuwape nafasi
watutumikie. Jitihada tunazoziona sasa za viongozi wa UKAWA za
kuendeleza siasa za uchaguzi kwenye mitaa ya miji yetu kwa njia za
vurugu na maandamano hazikubaliki hata kidogo. Tunalaani kitendo cha
wafuasi wa UKAWA kuchoma ofisi za CCM katika Wilaya ya Mbozi.
Amani ya
nchi hii ina thamani kuliko hitaji la madaraka la mtu yoyote. Wenzetu wa
UKAWA wana haki ya kulalamika lakini hawana haki ya kuiingiza nchi yetu
machafukoni kwa kuwakusanya vijana na kuwaingiza mitaani wafanye vurugu
na kuhatarisha maisha, kuharibu mali na kusimamisha shughuli za watu
wengine.
Tunawaomba
Watanzania waendelee na shughuli zao kama kawaida huku kila mmoja
akitambua wajibu wake wa kuilinda amani ya nchi yetu.
January Makamba
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
28.10.2015
CHAMA CHA MAPINDUZI
Sanduku La Posta: 50047
Dar Es Salaam, Tanzania
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269