Breaking News

Your Ad Spot

Dec 7, 2015

JUKWAA HURU LA WAZALENDO TANZANIA LAWAVAA JIJI, MANJI KUHUSU COCO BEACH


JUKWAA HURU LA WAZALENDO TANZANIA (JUHWATA)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu waandishi wa habari, Jukwaa limewaalika hapa katika muendelezo wake wa kuunga mkono juhudi za Mh. Rais wetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania mh.  Dr. John Magufuli. Hivi karibuni mh. Rais ameongoza mapambano makubwa ya kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi na kuwachukulia hatua wale wote ambao wamehusika kuliingizia taifa hasara ya mabilioni ya shilingi yaliyopotea. Tunaunga mkono juhudi hizi za Rais wetu na tunamuhakikishia kuwa Jukwaa linamuunga mkono na kwamba tunaomba azidishe kasi zaidi ili wale wote waliokwepa kodi wakamatwe, walipe na kufikishwa katika vyombo vya sheria bila huruma yoyote.

Ndugu waandishi wa habari, leo tumewaita hapa dhumuni kuu likiwa ni kuzungumzia uporaji wa maeneo ya wazi yanayotumiwa na wananchi hasa wanyonge. Uporaji huu unafanywa na baadhi ya wafanyabiashara wenye tamaa ambao hutumia nguvu zao za kiuchumi kuwarubuni na wakati mwingine kuwahonga viongozi wetu wachache serikalini wasiokuwa na uzalendo kwa taifa lao wala huruma kwa wanyonge ili wawapatie maeneo ya wazi yanayotumiwa na wananchi.

Katika hotuba yake ya tarehe 3/12/2015, akizungumza na wadau wa sekta binafsi nchini, mh. Rais alizungumza kwa uchungu njama za uporaji wa sehemu ya wazi ya umma ya ufukwe wa bahari wa inayotumiwa na wananchi wa hali ya chini kupumzika na kuogelea. Uporaji huu unafanywa na mfanyabiashara mmoja tajiri akitumia nguvu zake za kiuchumi kuwarubuni baadhi ya viongozi wa serikali ili wampatie eneo hilo. Hapana shaka eneo hilo ambalo wakazi wa Dar es salaam wa hali za chini wanalitumia kuogelea bure ni Coco beach iliyoko Oysterbay. Tumeamua kutoka hadharani kumuunga mkono mh. Rais kwa kuuanika uozo na njama za muda mrefu za kuligawa eneo hilo zinazofanywa na mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni na wenzake kwa mmiliki wa kampuni ya Q Consult Yusuf Manji.

 Mfanyabiashara huyu ameanza kuiitafuta Coco beach kwa miaka mingi sasa. Njama hizo zinahusisha kumfanyia hila na mizengwe muwekezaji mzawa anayetajwa kwa jina la Alphonce ambaye tangu mwaka 1994 amekuwa akitoa huduma kwa wananchi akiwa mpangaji wa manispaa ya Kinondoni. Bwana huyu kwa karibu miaka 9 mfululizo amekuwa akinyanyaswa, kukwamishwa kuendesha biashara yake na kufanyiwa njama za kunyang’anywa eneo hilo na watendaji wa serikali hasa wakurugenzi wa manispaa ya Kinondoni wa vipindi tofauti ili apewe mmiliki wa kampuni ya Q Consult bwana Yusuf Manji.

Njama hizi zimekuwa zikibeba viashiria, dalili na mazingira ya uwepo wa rushwa ya mtandao (syndicate corruption) ambapo viongozi wa serikali na manispaa ya Kinondoni akiwemo Mkurugenzi wa sasa wa manispaa ya Kinondoni bwana Musa Nati.

Mkurugenzi huyu amekuwa akikaidi maagizo ya viongozi wake wa juu kwa kiburi na ubabe na kumfanyia hila mtanzania huyu mnyonge kwa kumnyima mkataba huku akiwa amewekeza jasho lake katika ufukwe huo. Mkurugenzi amekaidi mara kadhaa maagizo ya Katibu mkuu wa Tamisemi, na hata aliyekua Waziri Mkuu mh. Mizengo Pinda. Aidha Mkurugenzi huyu ambaye anaonesha kuwekwa mfukoni na bwana Manji amekuwa akikaidi pia maamuzi ya vikao vya baraza la madiwani vya Full Council na kuidanganya kamati ya bunge ya LAC kuhusiana na sakata hili la Coco beach. Mkurugenzi huyu, kwa kushirikiana na viongozi wengine wa wilaya na Mkoa wa Dar es salaam ambao kwa leo tunahifadhi majina yao, wameonesha wazi kuwa upande wa bwana Yusuf Manji wakati wote wa sakata hili, huku wakionesha viashiria vya kuhongwa na kupindisha haki.

Tunajiuliza, kiburi hiki alichionacho Mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni anakitoa wapi? Jeuri hii ya kukaidi maagizo ya ofisi ya Waziri Mkuu na TAMISEMI anaitoa wapi?

Jukwaa linahoji, kwanini mfanyabiashara Yusuf Manji ang’ang’anie kupewa fukwe ya Coco beach na kutaka muwekezaji mnyonge anyang’anywe? Inawezekanaje mtu mmoja awe na ujasiri wa kuwarubuni watendaji wa serikali kwa miaka kadhaa kiasi cha kutotii maelekezo ya wakubwa wao? Yusuf Manji ni nani katika nchi hii hadi aweze kuabudiwa na viongozi hawa wa serikali?

Jukwaa linaona kila dalili kuwa kuna rushwa kubwa imetumika kuwanunua viongozi wetu ili wawe watetezi wa mabepari badala ya wanyonge. Ili waweze kubadili Coco beach kuwa mahali pa anasa na ghali kiasi cha kuwafanya watoto wa masikini washindwe kufika na kufurahia rasilimali za taifa lao.

MAAZIMIO
Tunamuomba mh. Rais amsimamishe kazi mkurugenzi huyu na kufanya uchunguzi juu ya jambo hili ili kubaini ni viongozi wangapi wamehongwa, wamehongwa nini na kwa muda gani, na ama la kwanini walipata kiburi cha kukaidi maelekezo ya viongozi wakubwa wa serikali kuhusu sakata hili. Jukwaa linamtaka bwana Yusuf Manji kutii kauli ya Mh. Rais na kuachana na suala la Coco beach kwa hiyari yake mwenyewe, kwani yako maeneo mengi ya fukwe katika nchi yetu ambayo angeweza kuwekeza.

Ikiwa bwana Yusuf Manji hatojitokeza hadharani kutoa kauli ya kuachana na na ufukwe wa Coco beach, Jukwaa litaandaa na kuhamasisha maandamano ya amani ya umma kueleza hisia zake juu ya jambo hili. Tunamkumbusha kuwa, mali za matajiri kama yeye hazilindwi na mitutu ya bunduki za polisi, bali zinalindwa na amani na utulivu na kuridhika kwa wanyonge. Wanyonge wenye hasira za kudhulumiwa ni hatari kuliko bomu la kutupa kwa mkono.

Tunafahamu ya kwamba yako maeneo mengi ya wazi ambayo kwasababu ya tamaa na rushwa, viongozi wa serikali wameyauza kwa matajiri na kuwafanya watoto wa wanyonge kukosa mahali pa kucheza.

 Jukwaa litaleta ushahidi wa maeneo mengine ambayo watu wa aina ya Yusuf Manji wamepewa na viongozi walafi wasiokuwa na uzalendo na maadili kinyume na sheria na taratibu za nchi yetu.

Tunamtaka mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni na viongozi wengine wa serikali wa wilaya hiyo kujitafakari mwenyewe kabla ya kuchukuliwa hatua na mh. Rais, kwani uko ushahidi wa ukaidi na ujeuri wake wa kupindisha haki na kumpendelea bwana Yusuf Manji hata kabla ya maamuzi ya kesi kutoka. Akishindwa kufanya hivyo, Jukwaa litaupeleka ushahidi huo kwa mh. Rais na kuweka wazi kwa umma wa watanzania ili waone ukweli wa jambo hilo. Jukwaa linamfahamisha bwana Manji kwamba, hataweza kushinda vita dhidi ya umma, hasa umma wa wanyonge ambao wenye hasira ambao wanaamini haki yao imeporwa kwa rushwa.

Jukwaa litaendelea kumuunga mkono mh. Rais na serikali yake katika mapambano dhidi ya rushwa, ukwepaji kodi na uzembe serikalini. Hatutamuogopa yeyote katika kutimiza wajibu wetu huu wa msingi kwa taifa letu. Tunawaomba wananchi wote kumuunga mkono mh. Rais kwa kumuombea na kufichua maovu yanayofanywa na viongozi wa serikali katika maeneo yao ikiwemo rushwa lugha chafu na ukwepaji kodi.

Mungu ibariki Tanzania.

Ahsanteni.

ALLY S. HAPI, MWENYEKITI

MTELA MWAMPAMBA, KATIBU MKUU

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages