TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Ndugu
zangu waandishi wa habari, nimeamua kuwaita ili kuzungumza nanyi kuhusu
baadhi ya mambo yaliyokuwa yanasemwa katika vyombo vya habari kuhusu
mimi.
Awali
ya yote napenda kusema kuwa habari hizo ni UONGO mtupu, ni mambo
yanayozushwa na waandishi wa habari hizo kwa nia ya kuchafua jina langu
kwa sababu wanazozijua wanaoandika. UKWELI ni kwamba haya ni mambo yenye
kufanywa kwa nia na dhamira mbaya dhidi yangu na hata familia yangu.
Hivi
karibuni, kwa mfano, lipo gazeti moja liliandika na kutoa picha yangu
na mtu mmoja waliyedai ni Mhe. Paul Makonda eti akinifunga kamba za
viatu. Katika maelezo yake mwandishi akadai kuwa Mhe. Makonda alipata
uteuzi kuwa Mkuu wa wilaya ya Kinondoni kwa sababu hiyo. Huu ni uongo
usiokuwa na hata chembe ya ukweli. Napenda watanzania wajue kuwa hakuna
wakati wowote Baba yangu alipokuwa Rais wa nchi yetu alinihusisha kwa
namna yeyote ile katika uteuzi wa mtu yeyote katika Serikali. Hivyo basi
kujaribu kunihusisha na uteuzi wa Mhe. Paul Makonda kuwa Mkuu wa Wilaya
wa Kinondoni ni jambo lisilokuwa na ukweli wowote.
Pili,
Yule mtu anae onekana katika ile picha siyo Mhe. Paulo Makonda bali ni
Bwana Deogratius Kessy anayefanya kazi katika kampuni ya ushonaji na
mavazi ya Bwana Sheria Ngowi. Nilishona safari suti kwenye kampuni hiyo.
Nilipokwenda kuchukua nguo yangu na nilipovaa ili kuona kama imeshonwa
vizuri, Bwana Sheria Ngowi alitaka nivae viatu vya ngozi. Bahati mbaya
nilikuwa nimevaa sandals hivyo akaamua kunipa viatu vya dukani kwake
nivae. Wakati bwana Deogratius Kessy akinisaidia kuvaa viatu ndipo ile
picha ikapigwa nampiga picha wa kampuni ya Bwana Sheria Ngowi ,
inashangaza na kusikitisha kuona picha hiyo inatumiwa kupotosha ukweli
kwa kutoa maelezo ya uongo. Ni dhahiri kwamba mwandishi aliamua kufanya
hivyo kwa maksudi mazima ya kutoa sifa mbaya kwangu na kwa Mheshimiwa
Paul Makonda. Hivi ndivyo uhuru wa habari unavyostahili kutumika ?
Siku
za nyuma gazeti lingine liliandika eti kuwa nilihojiwa kuhusu sakata la
makontena bandarini. Napenda kuwaambia ndugu waandishi wa habari kuwa
sijawahi kuhojiwa na mtu yeyote, chombo chochote au kamati yeyote kuhusu
madai hayo. Ni uongo usiokuwa na ukweli wowote. Ni mambo ya kugushi na
uzushi kabisa, Ninayasema maneno haya kwa kujiamini na kama mwandishi
ana uthibitisho wa madai yake autoe hadharani watu wauone. Aidha,
nasema kama yupo mtu aliyenihoji ajitokeze kukanusha ninayoyasema,
Namtaka aseme wazi. Nawahakikishia kuwa mtu huyo hayupo na wala
hatakuwepo.
Ndugu
waandishi na watanzania wenzangu, inaelekea kuna mtu au genge la watu
mahali Fulani ambao wameamua na kudhamiria kuchafua jina langu na la
familia yangu kwa kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Tangu Serikali ya awamu ya tano ianze jitihada za kuwabana watu
wanaokwepa kulipa kodi za Serikali bandarini wapo watu wamekuwa
wakifanya jitihada za kunihusisha na watu Fulani wanaotuhumiwa kuhusika
na ukwepaji huo. Wapo baadhi ya watu wamekuwa wakidai eti baadhi ya
makontena hayo ni yangu. Na, wapo waliodai eti kuwa nimekuwa nawasaidia
baadhi ya wafanyabiashara hao kukwepa kodi kwa kutoa maagizo kwa maofisa
wa forodha wasiwatoze kodi inayostahili kulipwa.
Napenda
kuwafahamisha kuwa sijawahi kuagiza bidhaa zozote kutoka nje hivyo
sijawahi kuwa na kontena lolote ambalo nililowahi kutakiwa kulipia
ushuru nikakwepa.Aidha,
sijawahi kumuombea msamaha wa kutokulipa au hata kupunguziwa kodi
mfanyabiashara yeyote au mtu yeyote aliyeingiza kontena nchini kutoka
nchi za nje. Kama mtu ana ushahidi autoe hadharani mimi niuone na
dunia iuone. Nawahakikishia ushahidi huo haupo na wala hautokuwepo.
Labda uwe wa kugushi na wakifanya hivyo wataumbuka.
Napenda
pia kutumia nafasi hii kusema kuwa sina na wala sijawahi kumiliki lori
au basi wakati wowote katika maisha yangu. Aidha, sina hisa au ubia na
mtu yeyote au kampuni yeyote ya malori au mabasi. Nayasema haya kwa
sababu wapo wabaya wangu wanaoeneza maneno ya kunihusisha na kumiliki
malori na mabasi. Pia kunihusisha na baadhi ya makampuni yanayomiliki na
kuendesha biashara ya malori na mabasi.
Ndugu
wanahabari, napenda kusema kwa kurudia na kusisitiza kuwa sina lori
wala basi hata moja na sina ubia na wafanyabiashara ama makampuni yoyote
yanayofanya shughuli hizo. kama yupo mtu yeyote ana ushahidi wa
kuhusika kwangu auweke hadharani watu wauone. Napenda ieleweke kuwa kama
ningekuwa na ubia wa namna hiyo nisingekuwa na sababu ya kuficha.
Niogope kitu gani ? Ukweli ni kwamba sizuiliwi kufanya biashara kama
nikipenda kufanya hivyo , Hata kwa nafasi yangu ya sasa ya uongozi yaani
mbunge bado sina kizuizi. Mbona Bungeni wapo wafanyabiashara wakubwa
kwa wadogo. Isingekuwa ajabu kwangu kufanya biashara hivi sasa mimi
pamoja na kuwa mbunge ni mwanasheria wa kujitegemea na nimeiweka katika
TAMKO langu la mali na madeni la viongozi kwa mujibu wa sheria ya
maadili ya viongozi.
Nimewavumilia
sana lakini sasa nimechoka, nimeona leo nivunje ukimya. Nimeona niseme
kidogo kwani bila ya kufanya hivyo nitaliacha genge la watu wenye nia
mbaya na mimi waonekane wanasema kweli. Wahenga wanasema msema pweke
hushinda! Nikiendelea kukaa kimya uongo wao utageuka kuwa ukweli dhidi
yangu.
Naambiwa
hapa nchini siku hizi kila jengo jipya linalojengwa linasemekana ni la
Ridhiwani, kituo kipya cha petrol ni cha Ridhiwan.
Nimeanza
kuona athari za uongo huo, Siku moja kuna mtu alikuja kuniomba
nimpangishe katika lile jengo la PSPF pale stesheni. Nilipomuuliza
nitampangishaje akasema mbona watu wamemwambia ni jengo langu!? Siku
nyingine nikakutana na jamaa mmoja mwenye asili ya kiasia akiwa anahema.
Akasema ananiomba sana niache kutaka kupora kampuni yake,nikamuuliza
kampuni gani hiyo? Na kwanini anasema hivyo? Akanijibu, anasikia
wakisema kampuni yake ni ya ridhiwani wakati kampuni hiyo hata yeye
kairithi kwa baba yake na yeye alirithi kwa baba yake zaidi ya miaka
hamsini iliyopita, Nikamwambia kuwa habari hiyo si kweli, sina mpango
huo na wala sina sababu ya kufanya hivyo. Hayo ni maneno yanayoenezwa na
wabaya wangu walioamua kunipakazia kwa sababu wazijuazo wao. Tukaachana
,sijui kama ameamini kama sina mpango wa kumpora kampuni yake. Siku
moja Mzee wangu mmoja wa kwetu kijijini alinilalamikia kuwa nina roho
mbaya kwa vile sitaki kumpa kazi mwanae kwenye kampuni yangu ya malori
wakati yeye ni dereva mzuri, Nilipomueleza Yule mzee kuwa sina lori hata
moja akashangaa na kusema mbona watu wanasema nina malori mengi. Ndugu
zangu mnaiona fitina kubwa inavyotengenezwa katika jamii kuhusu maneno
haya, Wapo wanaoniona mimi FISADI, Wapo wanaoniana mimi nina Roho mbaya, Wapo wanao niona mie nataka kupora mali zao.
Baada ya Baba kustaafu maneno yamekuwa mengi na yanazidi kupata kasi.
kila kukicha wanazua jambo jipya. Nimeoa niyaseme haya ili watu wajue
ukweli wa upande wangu.
Naomba
nimalize kama nilivyoanza kwamba yanasemwa mengi lakini ni maneno ya
uzandiki, uzushi na ni uongo mtupu usiokuwa na chembe ya ukweli. Wale
wanaosema, kuandika, na kueneza maneno hayo wanajua kuwa wanasema UONGO,
ila wanafanya hivyo kwa vile wana nia mbaya dhidi yangu na familia
yangu , Naomba watanzania muyapuuze maneno hayo, naomba watanzania
wenzangu muupuuze uongo huo.
siko hivyo, sina mali hizo na wala sifanyi hayo wanayodai nafanya na wala sina mpango wa kuyafanya.
Imetolewa na:-
Ridhiwan J. Kikwete
Mbunge wa Jimbo la Chalinze.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269