Breaking News

Your Ad Spot

Jan 17, 2016

TUKUMBUSHANE : KISA CHA RAIS ALIYEKATWA MASIKIO ; NI SAJENTI SAMWELI DOE (2)


Pichani ni Charles Taylor akiwa msituni.
Ndugu zangu,
Ni kisa cha Sajenti Samuel Doe.
Naam, watu wa kabila la Samuel Doe waliogopewa na makabila mengine. Waliweza kufanya lolote lile na hakuna aliyewagusa. Waliua na waliwatisha wengine. Wengi wasio wa kabila la Doe waliishi kwa hofu kubwa.
Na kile ambacho kila mtu, asiye wa kabila la Doe, alikuwa anakisubiri, ni kushuhudia mwisho wa Sajenti Samuel Doe.
Na hapa akatokea Charles Taylor. Huyu alikuwa rafiki wa zamani wa Sajenti Samuel Doe.
Lakini, urafiki wao ulikufa pale Samuel Doe alipodai kuwa Charles Taylor alimtapeli Doe dola milioni moja. Kisha Taylor akatorokea Marekani. Huko akaanza kufanya biashara kwa mtaji wa fedha alizomtapeli Sajenti Samuel Doe.
Charles Taylor nae akaishia gerezani nchini Marekani kwa mashtaka ya utapeli. Lakini, akatoroka jela na kukimbilia Ivory Coast. Na akiwa Ivory Coast, Charles Taylor akaanza kujipanga kwenda kuuangusha utawala wa Sajenti Samuel Doe.Charles Taylor akiwa Ivory Coast alikiandaa kikosi cha wapiganaji 60. Kikosi kilikuwa tayari kwa kuingia Monrovia kumwondoa Samuel Doe madarakani.
Ilikuwa ni mwaka 1989. Wakati huo, wajuzi wa masuala ya kijeshi waliamini kabisa, kuwa Sajenti Samuel Doe angeweza , kirahisi kabisa, kumteketeza kijeshi, Charles Taylor na kikosi chake cha watu 60. Sajenti Samuel Doe angeweza kufanya hivyo hata kabla Charles Taylor hajavikaribia viunga vya Monrovia.
Badala yake, ‘ Master Sergeant’ Samuel Doe aliwatuma mstari wa mbele, wanajeshi kutoka kabila lake la Krahn. Ni wanajeshi wa kuokoteza ambao wengine hawakuwa hata na viatu. Wanajeshi wale mabayaye wa Samuel Samuel Doe, njiani wakitokea Monrovia wakielekea uwanja wa mapambano wakaanza kufanya wizi wa ngawila. Kuiba mali za watu.
Habari za askari ' vibaka' wa Samuel Doe zikasambaa haraka kwenye vijiji vya msituni. Huko watu wakajitolea kujiunga na vikosi vya Charles Taylor kukabiliana na askari bayaye wa Samuel Doe.
Jeshi la Taylor likakua kwa haraka.Baada ya miezi sita tu likaingia kwenye viunga vya mji mkuu wa Liberia, Monrovia.
Ndipo hapo kwenye kambi ya Taylor ugomvi ukazuka. Nani atakuwa Rais? Nani atakuwa na mamlaka ya hazina kuu. Ni ugomvi uliowatenganisha Charles Taylor na Prince Johnsson aliyeamua kuachana na Taylor na yeye kuanzisha kikosi chake.
Wote wawili walikuwa na tamaa ya Ikulu. Vita sasa ikawa ya vikosi vitatu kugombania kuingia Ikulu ya Monrovia; Kikosi cha Sajenti Samuel Doe kinachojihami, kikosi cha Charles Taylor na kikosi cha Prince Johnsson. Wote wakaanza kupigana wenyewe kwa wenyewe kugombania Ikulu ya Monrovia. Nini kilitokea?
Kisa hiki kitaendelea...
Maggid,
Iringa.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages