Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (katikati), akiongozwa
na baadhi ya viongozi wa Machimbo ya Dhahabu ya Matinje yaliyopo katika
Kijiji cha Matinje Kata ya Mwashiku wilayani Igunga. Naibu Waziri
alitembelea Machimbo hayo hivi karibuni akiwa katika ziara ya kikazi
mkoani Tabora.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Medard Kalemani (Mwenye Suti-katikati)
akipokea maelezo kutoka kwa Meneja wa Machimbo ya Matinje yaliyopo Kata
ya Mwashiku wilayani Igunga, Charles Nogu, wakati alipotembelea Machimbo
hayo akiwa katika ziara ya kazi hivi karibuni.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini (katikati) akikagua machimbo ya Matinje
yaliyopo Kata ya Mwashiku wilayani Igunga, alipotembelea Machimbo hayo
hivi karibuni. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Mbunge wa Manonga, wilaya ya
Igunga, Seif Gulamali. Wengine pichani ni baadhi ya viongozi wa Machimbo
hayo, wataalamu kutoka Wizarani, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na
Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Na Veronica Simba - Nzega
SERIKALI
imetoa siku tano kwa mwekezaji wa madini ambaye ni Kampuni ya NMDC
Limited kutoka India, kushughulikia utaratibu wa kuwalipa fidia wananchi
wa Kata ya Ntobo iliyopo wilayani Igunga, mkoa wa Tabora, walioachia
ardhi yao kumpisha mwekezaji huyo.
Agizo
hilo lilitolewa juzi, Februari 17 na Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Dkt Medard Kalemani, wilayani Nzega alipokutana na viongozi wa Kampuni
hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tabora kukagua miradi
mbalimbali inayotekelezwa chini ya wizara yake.
Akiwa
wilayani Igunga, Naibu Waziri alipokea taarifa kuwa mwekezaji huyo
alipewa leseni nne za uchimbaji madini wa kati mwaka 2012 lakini mpaka
sasa hajaanza shughuli za uzalishaji kutokana na kutolipa fidia za
maeneo ya wakazi wa eneo hilo.
Kutokana
na taarifa hiyo, Naibu Waziri aliagiza kukutana na Mwekezaji huyo
ambapo walikutana naye juzi akiwa wilayani Nzega akiendelea na ziara
yake.
Katika
kikao hicho, ilibainika kuwa, kiasi cha shilingi za Tanzania bilioni
20.7 zinadaiwa kama fidia kwa wananchi waliopisha eneo husika.
Ilielezwa
kuwa, ulipaji huo wa fidia umekwama kutokana na mwekezaji huyo kutotaka
kulipa fidia yote kwa wakati mmoja bali anataka alipe fidia kidogo kwa
kuanzia na eneo dogo kati ya lile analomiliki ambalo anadai ndilo
atakaloanza kufanyia kazi.
Aidha, alidai kwamba atakuwa analipa fidia kwa eneo lililobaki kulingana na atakavyokuwa akilitumia.
Akizungumza
katika kikao hicho, Kamishna Msaidizi wa Madini wa Kanda ya
Kati-Magharibi, Humphrey Mmbando alimweleza Naibu Waziri kuwa, wananchi
wa eneo husika wanalalamika kuwa tangia eneo lao lichukuliwe na
mwekezaji huyo, shughuli zao zilizokuwa zikifanyika katika eneo hilo
zimesimama na hivyo wanahitaji kulipwa fidia stahiki.
Kamishna
Mmbando aliongeza kuwa, kufuatia malalamiko ya wananchi, Ofisi yake
ilimtaka mwekezaji huyo awe ametoa majibu ya namna atakavyoshughulikia
madai ya wananchi ndani ya siku 10 ambayo ilikuwa ni juzi, Februari 17,
wakati kikao hicho kikikaa.
Kutokana
na maelezo hayo, Naibu Waziri alitoa siku tano zaidi kwa mwekezaji huyo
ili ashughulikie mambo kadhaa katika kutatua mgogoro huo.
Ndani
ya siku hizo tano, Naibu Waziri alimtaka mwekezaji huyo, atoe taarifa
rasmi ya kimaandishi kwa Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya
Kati Magharibi kuwa anakusudia kufanya uzalishaji kwa kuanzia na eneo
dogo ndani ya leseni yake.
Pia,
alimtaka mwekezaji huyo kumwomba Mthaminishaji wa Serikali kufanya
uthamini kwa kujikita katika eneo lile tu ambalo anakusudia kuanza
kulifanyia kazi.
Vilevile,
Naibu Waziri alimtaka mwekezaji huyo kuzungumza na wananchi husika ili
wakubaliane kiasi cha fidia atakachotoa kwao kwa kuzuia shughuli zao za
kujipatia kipato katika eneo hilo kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.
Mbali
na maagizo hayo, Naibu Waziri alimtaka mwekezaji huyo awaruhusu
wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji katika eneo ambalo atakuwa
hajaanza kulifanyia kazi.
“Nimewapa
siku tano zaidi, mfanyie kazi maagizo niliyoyatoa vinginevyo,
tutachukua hatua nyingine stahiki za kisheria dhidi yenu.”
Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri Kalemani ameagiza kufutwa kwa leseni zote
za madini ambazo hazifanyiwi kazi na maeneo hayo kugawiwa kwa wachimbaji
wadogowadogo ili wayafanyie kazi na kulipa mrabaha kwa Serikali.
“Kwa
kuanzia, katika eneo hili, nimeagiza leseni za utafutaji wa madini za
kampuni za Kilimanjaro Mine na Mabangu Resources ziandikiwe taarifa ya
kufutwa na tutaendelea na maeneo mengine,” alisema.
Alisema
kuwa kuna wawekezaji wengi ambao wamekuwa wakishikilia maeneo kwa muda
mrefu pasipo kuyafanyia kazi na hivyo kuikosesha Serikali mapato
yatokanayo na kodi, pia kuwakosesha wananchi maeneo ya kufanyia kazi.
Awali,
Naibu Waziri alitembelea Machimbo ya Madini katika Kijiji cha Matinje
B, Kata ya Mwashiku wilayani Nzega ambapo mbali na kumpongeza mmiliki wa
machimbo hayo, Jason Shinyanga, kwa kulipa mrabaha wa Serikali,
alimtaka kuboresha mazingira ya uchimbaji katika eneo hilo.
Meneo
aliyoagizwa kuboresha ni pamoja na kujenga nyumba za kulala watumishi
wake pamoja na vyoo bora. “Tunakupa taarifa ya siku 60 urekebishe dosari
hiyo, usiporekebisha, tutasahau kama umelipa mrabaha au la,”
alisisitiza Naibu Waziri.
Aidha,
Naibu Waziri aliwashauri wananchi wanaojishughulisha na uchimbaji
kuhakikisha wanapata ushauri wa kitaalamu kutoka ofisi za madini katika
maeneo yao kabla hawajaanza shughuli hizo.
Pia,
aliwataka kuhakikisha wanakuwa na leseni halali za kuendeshea shughuli
hizo za uchimbaji ili pamoja na mambo mengine kuongeza thamani ya maeneo
yao pindi wanapotaka kuyauza au kuingia ubia na wawekezaji wa kati na
wakubwa.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269