Rais
Yoweri Museveni wa Uganda alisisitiza siku ya Jumamosi juu ya umuhimu
wa nchi yake kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ambayo
makao makuu yake yako The Hague nchini Uholanzi.
Kwa
mujibu wa Museveni, mahakama hiyo imebadilika kuwa chombo kinachotumiwa
na madola ya Magharibi kwa lengo la kufanya njama dhidi ya nchi za bara
la Afrika.
Mahakama
hiyo ya kimataifa imekuwa ikikosolewa kwa muda sasa na nchi mbalimbali
za dunia na hasa za Kiafrika. Akizungumza katika kikao kilichofanyika
mwishoni mwa mwezi Januari uliopita huko mjini Addis Ababa Ethiopia,
Rais Idriss Deby wa Chad ambaye pia ni mwenyekiti wa hivi sasa wa Umoja
wa Afrika AU, alisema kuwa mahakama ya ICC imekuwa ikiwaandama viongozi
wa bara la Afrika tu.
Deby
amesema ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu umekuwa ukifanyika katika
nchi nyingi za Magharibi lakini mahakama hiyo imeufumbia macho na
kuwaandama viongozi wa Kiafrika tu. Katika kikao chao cha hivi karibuni
pia viongozi wa Umoja wa Afrika waliunga mkono pendekezo lililotolewa na
Kenya kutaka nchi wanachama wa umoja huo zijiondoe kwa pamoja katika
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
Mahakama
hiyo ilianzishwa mwaka 2002 kwa lengo la kuwapandisha kizimbani watenda
jinai za kivita na wahusika wa mauaji ya kimbari ambao wameshindwa
kushtakiwa na kuhukumiwa katika nchi zao.(VICTOR)
Hadi sasa
sehemu kubwa ya kesi ambazo zimefuatiliwa na kuchunguzwa na mahakama ya
ICC zinahusiana na nchi za Kiafrika zikiwemo Kenya, Ivory Coast, Libya,
Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati,
Uganda na Mali.
Malalamiko dhidi ya mahakama hiyo yameongezeka tokea mwaka 2009 ambapo
ilitoa waranti wa kimataifa wa kutiwa nguvuni Rais Omar al Bashir wa
Sudan kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita huko Darfur, magharibi
mwa nchi hiyo. Wakati huo Umoja wa Afrika ulikataa kushirikiana na
mahakama hiyo kwa hoja kuwa haikuwa na mamlaka ya kumtia nguvuni rais wa
nchi yoyote barani humo.
Mvutano
kati ya mahakama ya ICC na nchi za Kiafrika uliongezeka tena na kufikia
kilele wakati wa kufikishwa mbele ya mahakama hiyo Laurent Gbagbo,
aliyekuwa rais wa Ivory Coast na pia kufuatia hatua ya mahakama hiyo ya
kukataa pendekezo la Umoja wa Afrika la kufutiliwa mbali takwa la
kufikishwa mahakamani hapo Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya pamoja na makamu
wake William Ruto kujibu mashtaka ya jinai za kivita.
Ni kwa
msingi huo ndipo viongozi wa Kiafrika wakaamini kwamba mahakama hiyo
inawalenga kwa njia isiyo ya kiuadilifu. Lakini pamoja na hayo msimamo
huo wa viongozi wa Afrika unakosolewa na wengi. Wapinzani wao wanasema
kuwa viongozi hao wanataka kujiondoa katika mahakama ya The Hague ili
waendelee kutenda jinai na kuwakandamiza watu wao bila ya kuwajibishwa
kisheria.
Tukiachilia
mbali mvutano huo wa nchi za Kiafrika na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai
ICC, uzoefu wa huko nyuma unaonyesha wazi kuwa kuna haja ya kuwepo kwa
chombo kama hicho cha kimataifa kwa ajili ya kushughulikia jinai
zinazotendwa na wahalifu.
Wakati
vyombo vya mahakama vya nchi yoyote ile vinaposhindwa kushughulikia kesi
za wahalifu ndani ya nchi, vyombo vya kimataifa vinapaswa kuingilia
kati na kutetea haki na maslahi ya wahanga wa jinai za wahalifu hao.
Mahakama
ya Kimataifa ya Jinai ICC ilibuniwa kwa madhumuni ya kuondoa kinga ya
kisheria dhidi ya watenda jinai wakuu wanaoitia wasiwasi jamii ya
kimataifa. Pamoja na hayo inaonekana kuwa kama zilivyo taasisi nyingine
muhimu za kimataifa, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imepoteza
muelekeo na kugeuka kuwa chombo kinachotumiwa na madola ya Magharibi
kutoa mashinikizo ya kisiasa dhidi ya makundi fulani.
Muelekeo
wa upande mmoja wa mahakama hiyo umezua shaka kubwa katika jamii ya
kimataifa na bila shaka unahitaji kurekebishwa haraka iwezekanavyo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269