Akizungumza na Rais John Dramani Mahama wa Ghana hapo jana Jumapili
hapa mjini Tehran, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu amesema kuwa maslahi ya madola ya kiistikbari duniani ndicho
chanzo cha ghasia na vita vinavyoendelea katika pembe mbalimbali za
dunia.
Huku akiashiria kuongezeka kusiko kwa kawaida kwa makundi ya
kigaidi Mashariki ya Kati na vilevile barani Afrika, Kiongozi Muadhamu
wa Mapinduzi ya Kiislamu amehoji ni vipi kiwango kikubwa cha silaha za
kisasa na fedha zinayafikia makundi hayo. Akibainisha chanzo cha suala
hilo, Kiongozi Muadhamu amesema kuwa makundi hayo ya kigaidi yamebuniwa
na kudhaminiwa na mashirika ya kijasusi, na kwamba kiini cha matatizo
yaliyopo ni madola makubwa ya kiistikbari yanayoongozwa na Marekani, na
pia utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unatumia fursa hiyo kuwa
dhihirisho la shari katika eneo. Ukweli wa mambo ni kuwa nchi nyingi
duniani zinakabiliwa na tishio la pamoja ambalo ni ugaidi. Suala hilo
linaonyesha wazi kuwa ugaidi hutambui mipaka na kwamba umeeneza mizizi
katika nchi za Asia, Afrika Ulaya na hata katika jamii ya Marekani.
Ugaidi na misimamo ya kupindukia mipaka unachochewa na mambo kadhaa,
muhimu zaidi zikiwa ni siasa za kindumakuwili za nchi za Magharibi
katika suala zima la kupambana na ugaidi na kutumiwa makundi ya kigaidi
kama Daesh kuwa chombo cha kufikia malengo yao haramu. Kama
ilivyoashiriwa katika matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu alipomkaribisha ofisini kwake Rais Dramani Mahama wa Ghana,
njia pekee ya kupambana na ugaidi ni kukabiliana na kila jambo
lilanochochea ugaidi pamoja na kung'oa mizizi yake yote. Ili kufikia
lengo hilo uwanja unaofaa unapasa kuandaliwa ili kuruhusu pande zote
husika kushirikiana katika kupambana na tishio hilo la pamoja . Mtazamo
wa Iran katika ushirikiano wake na nchi tofauti za dunia umejengeka
katika msingi huo. Uhusiano wa Iran na nchi za Kiafrika ikiwemo Ghana
pia unatekelezwa kwa mtazamo huo. Masuala yaliyojadiliwa katika
mazungumzo ya Rais wa Ghana na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
yanathibitisha kiwango cha uhusiano huo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
inaamini kuwa kama hakutakuwepo na ushirikiano wa aina hiyo basi nchi
zote zitadhurika kutokana na ugaidi na wala hakuna yeyote atakayeshinda
katika uwanja huo. Kwa hakika usalama ni suala la kimataifa na wala
halihusiani tu na mipaka ya nchi za Asia na Afrika. Kwa hivyo njia pekee
ya kupambana na ugaidi ni kushirikiana nchi zote za dunia. Ghana pia
ambayo ina uzoefu mkubwa katika mapambano dhidi ya ukoloni imeazimia
kukabiliana vilivyo na makundi ya kigaidi. Pamoja na hayo tunapasa
kusema kuwa ili kukabiliana vilivyo na vitisho na changamoto za pamoja
kuna haja ya kubadilishwa mitazamo hasi na kufutiliwa mbali siasa za
kundumakuwili za baadhi ya nchi zinazodai kuambana na ugaidi.
Ukweli wa mambo ni kuwa baadhi ya nchi za eneo ikiwemo Saudi Arabia
zinachochea ugaidi na kuutumia katika kujaribu kuiangusha serikali
halali ya Syria. Bila shaka siasa hizo mbovu zitaimarisha tu malengo ya
uingiliaji na kujipanua Marekani na wakati huohuo kuupa utawala haramu
wa Israel fursa ya kutumia vibaya migogoro ya eneo kwa ajili ya
kudhamini maslahi yake.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269