Breaking News

Your Ad Spot

Feb 16, 2016

SHAMBULIZI LA BOMU SOMALIA LAUA WAZIRI WA ZAMANI


Shambulizi la bomu Somalia laua waziri wa zamani
Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Somalia ameuawa katika shambulizi la bomu lililofanywa na kundi la wanamgambo wa al-Shabaab. Shirika la habari la Reuters limemnukuu Sheikh Abdiaziz Abu Musab, msemaji wa kundi hilo la kigaidi ambaye amekiri kuwa wao ndio waliomuua Muhyiddin Muhammed katika shambulizi la bomu la kutegwa garini.
Aidha polisi ya Somalia imethibitisha kuuawa Muhammed, ambaye pia alikuwa mshauri wa Spika wa Bunge la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Habari zaidi zinasema kuwa, aliyekuwa na Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Somalia kwenye gari hilo wakati wa shambulizi hilo la jana Jumatatu alinusurika kifo ingawa amepata majeraha madogo. Mauaji hayo yanajiri siku chache baada ya Rais Hassan Sheikh Mohamoud wa Somalia kusema kuwa, ili kulishinda kundi la kigaidi la al-Shabaab kuna haja kwa vijana wa nchi hiyo kushiriki katika vita na mapambano dhidi ya wanamgambo hao. Rais wa Somalia amesema kuwa, vikosi vya nchi yake vimepata mafanikio ya kuzingatiwa katika vita dhidi ya kundi la al-Shabab; lakini ili ushindi kamili upatikane dhidi ya wanamgambo hao kuna haja ya vijana kuwa na ushiriki katika hilo. Akizungumza mjini Munich Ujerumani na maafisa wa usalama na wanadiplomasia wa Somalia, Rais Hassan Sheikh Mohamoud alisema kuwa, kuna watu wengi wamejitolea na kusimama nchini Somalia kwa ajili ya kupambana na wanamgambo wa al-Shabab, lakini ili kupatikane ushindi kamili dhidi ya wanamgambo hao wanaohatarisha usalama wa nchi ushiriki wa vijana unahitajika

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages