Kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO kikishirikiana na jeshi la nchi hiyo
kimesema kimefanikiwa kuangamiza idadi kubwa ya waasi wa Uganda
mashariki mwa nchi.
Jean Baillaud, Naibu Msemaji wa MONUSCA amesema waasi hao waliuawa
katika operesheni ya jana dhidi ya kundi la ADF-Nalu wa Uganda katika
kijiji cha Semuliki, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Uganda.
Naye Mak Hazukay, Msemaji wa Jeshi la Kongo DR amesema kikosi cha
MONUSCO kimeshambulia kwa mahelikopta ngome ya waasi hao mashariki wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hata hivyo idadi ya waasi waliouawa
katika shambulizi hilo haijabainika lakini imearifiwa kuwa raia mmoja
aliuawa na wengine watatu kujeruhiwa na waasi wa ADF.
Kundi la waasi la ADF-Nalu lilianzisha uasi na kupanga kuipindua
serikali ya Uganda zaidi ya miaka 20 iliyopita, lakini wakalazimika
kutorokea DRC. Itakumbukwa kuwa, kwa akali watu 39 waliuawa nchini DRC
kufuatia mapigano makali yaliyotokea kati ya jeshi la nchi hiyo na waasi
wa ADF-Nalu wa Uganda Disemba mwaka jana 2015.
Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limekuwa
likishuhudia machafuko kwa zaidi ya miaka 20 sasa kutokana na kuwa ngome
ya makundi kadhaa ya waasi kutoka nchi jirani za Rwanda na Uganda.
Baadhi ya vijiji mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
vinadhibitiwa na makundi ya waasi hali ambayo imewafanya wakazi wake
kuyaacha makazi yao na kuwa wakimbizi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269