Jumamosi ya jana tarehe 26 Machi ilisadifiana na kutimia mwaka mmoja
tangu Saudi Arabia ilipochukua uamuzi wa kuivamia na kuishambulia
kijeshi nchi ya Yemen.
Abdul Malik al-Houthi, Kiongozi wa Harakati ya Wananchi ya
Ansarullah ya Yemen amesema kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja wa
uvamizi wa Saudia dhidi ya Yemen kwamba, vita na uvamizi huo ulianza na
unaendelea kwa ridhaa ya Marekani na uungaji mkono wa utawala wa
Kizayuni wa Israel.
Sambamba na kutimia mwaka mmoja wa uvamizi wa kijeshi wa utawala wa
ukoo wa Aal-Saud na washirika wake, Abdul Malik al-Houthi amesisitiza
kuwa, Saudia haikuheshimu haki ya ujirani mwema na Yemen na kumshambulia
bila haki jirani yake huyo. Aidha al-Houthi amesema, Saudia ikiwa na
uungaji mkono kamili wa Marekani, Uingereza, Israel na mamluki wake
iliishambulia Yemen ili kuurejesha madarakani utawala wa kidiktea,
lakini kuwa macho wananchi wa Yemen na vikosi vya Yemen kumesambaratisha
njama hiyo. Hii ni katika hali ambayo, katika mashambulio hayo ya mwaka
mmoja ya Saudia dhidi ya Yemen, wavamizi wakitumia silaha zilizopigwa
marufuku wamefanya mauaji ya kinyama dhidi ya raia. Katika mashambulio
ya anga ya majeshi ya Saudia na mamluki wake dhidi ya makazi ya raia,
wahusika wamekuwa wakilenga hospitali, shule, bandari, barabara,
taasisi, vyombo vya usafiri na uchukuzi, majengo ya serikali, vituo vya
umeme na hata makaburi na hivyo kufanya uharibifu mkubwa. Ripoti kutoka
Yemen zinasema kuwa, miundo mbinu ya nchi hiyo imeharibiwa vibaya na
kuyafanya maisha ya wananchi kuwa magumu kila siku iendayo kwa Mungu.
Hivi karibuni Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch
na asasi nyingine saba zilitoa ripoti ya pamoja ambayo mbali na
kuashiria jinai za kivita huko Yemen ilitaka Saudia iwekewe vikwazo vya
silaha. Aidha mtandao wa Intaneti wa Foreign Policy umeashiria kutimia
mwaka mmoja wa vita vya Saudia huko nchini Yemen na kuandika: Vipi
Marekani, Uingereza na Ufaransa zinaendelea kuitumia silaha Saudia
katika hali ambayo marubani wa ndege za kijeshi za Riyadh wamekuwa
wakiwadondoshea mabomu raia wasio na hatia wa nchi hiyo? Mwaka mmoja wa
mashambulio ya Saudia dhidi ya Yemen unatimia katika hali ambayo,
asilimia 83 a wananchi wa nchi hiyo wanategemea misaada ya kibinadamu.
Hii ni katika hali ambayo, mazungumzo ya amani ya Yemen yanatarajiwa
kufanyika tarehe 18 ya mwezi ujao huko Kuwait. Baada ya mwaka mmoja wa
vita huko Yemen, Wasaudia wanatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na
Harakati ya Ansarullah na kujadili namna ya kuhitimisha vita hivyo.
Tangazo la utayarifu wa Saudia la kushiriki mazungumzo ni sawa na
kuikubali Harakati ya Wananchi ya Ansarullah kuwa ni upande wenye
taathira katika matukio ya Yemen. Aidha hatua hiyo ni ithbati ya kukiri
Wasaudia kushindwa katika vita huko Yemen na kusimama kidete muqawama wa
wananchi dhidi ya wavamizi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269