Breaking News

Your Ad Spot

Mar 25, 2016

MKUTANO WA NANE WA NCHI MAJIRANI WA LIBYA ULIOFANYIKA JIJINI TUNIS, TUNISIA NA KUHUDHURIWA NA RAIS MSTAAFU JAKAYA KIKWETE

 Rais Mstaafu na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika katika  Usuluhishi wa Mgogoro Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwasilisha salamu za Umoja wa Afrika kwa nchi majirani za Libya
------------------------------------------------------
Mkutano wa 8 wa Nchi Jirani wa Libya chini ya Uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia Mheshimiwa Khemales Jhinaoui umefanyika jijini Tunis Tarehe 22 Machi, 2016. Mkutano huo uliotanguliwa na Mkutano wa Ngazi ya Wataalamu uliofanyika tarehe 21 Machi, 2016 uliohusisha nchi jirani za Algeria, Chad, Misri, Niger, Sudan na Tunisia. Waalikwa wengine katika Mkutano huo walikuwa ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Martin Kobler, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika kwa Libya Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) Mheshimiwa Nabeer Al-Arabi na Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kigeni wa Umoja wa Ulaya Mheshimiwa Helga Schmidt.

Mkutano huo wa siku moja ambao ulihudhuriwa kwa mara ya kwanza na Mwenyekiti wa Baraza la Utawala na Waziri Mkuu wa Libya Mheshimiwa Fayez Al-Sarraj umepitisha tamko la pamoja kuunga mkono juhudi za kuleta amani nchini Libya chini ya Mkataba wa Makubaliano (Libya Political Agreement) uliotiwa saini huko Skhirat Morocco Desemba 17, 2015. Wamewataka wale wote ambao hawakusaini Mkataba huo kufanya hivyo mapema iwezekanavyo.

Kupitia Tamko hilo, nchi jirani za Libya zimeelezea wasiwasi wao juu ya kuzorota kwa hali ya usalama na kushamiri kwa ugaidi kunakotokana na ombwe la kisiasa nchini Libya, hali inayoathiri usalama wa nchi jirani. Kwa ajili hiyo, nchi hizo zimeunga mkono jitihada za Mwenyekiti wa Baraza la Utawala na Kiongozi wa Libya Fayez Sarraj za kuunda Serikali na kuanza kazi Shughuli zake katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli.  Wamewataka Wabunge wa Bunge wote kuungana na kupitisha pendekezo la Baraza la Mawaziri ili Serikali iweze kuanza kazi zake.

Kuhusu kupambana na ugaidi ndani ya Libya, nchi hizo zimepinga kwa kauli moja shambulio lolote la kijeshi kutoka nje ya Libya na kusema kuwa athari zake zitakuwa kubwa kwa wananchi na nchi jirani na Libya. Wametaka shambulio lolote la kijeshi kutoka nje litokane na ombi la Serikali ya Libya na kwa kuzingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa.


Akizungumza katika mikutano huo, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameunga mkono jitihada za nchi jirani na Libya kuungana kwa pamoja kusaidia kutatua mgogoro huo. Amesisitiza kuwa Umoja wa Afrika unaunga mkono Mkataba wa Amani wa Libya na hauna dhamira ya kuanzisha mchakato mwingine bali kuongeza msukumo katika mchakato uliopo. Hivyo, ameungana nao kuwataka wale wote ambao hawajasaini mkataba huo kufanya hivyo. Amesisitiza pia umuhimu wa Bunge la Libya kukamilisha wajibu wake wa kuidhinisha Baraza la Mawaziri ili Serikali mpya iweze kufanya kazi.  Amewakumbusha nchi jirani za Libya juu ya wajibu wao wa kipekee katika kusaidia kumaliza mgogoro huo na amewaahidi ushirikiano wa Umoja wa Afrika katika kufikia azma hiyo.
Pichani Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia na Mwenyekiti wa Mkutano wa 8 wa Marafiki wa Libya Mheshimiwa Khemales Jhinaoui akifungua Mkutano jijini Tunis.
PICHA ZAIDI ZA JK TAFADHALI>BOFYA HAPA

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages