Breaking News

Your Ad Spot

Apr 11, 2016

AU: UCHAGUZI WA DJIBOUTI ULIKUWA HURU NA WA HAKI

AU: Uchaguzi wa Djibouti ulikuwa  huru na wa haki
Licha ya lalama kutoka vyama vya upinzani, lakini Umoja wa Afrika AU umesema uchaguzi mkuu wa Djibouti wa Ijumaa iliyopita ulikuwa huru na wa haki.
Mkuu wa timu ya waangalizi wa AU katika uchaguzi huo, Soumana Sako amesema licha ya uchaguzi huo kukabiliwa na kasoro za hapa na pale, lakini ulikuwa huru na wa haki. Amesema vyombo husika vilionyesha uwazi wa hali ya juu, jambo ambalo linaufanya uchaguzi huo kuhesabiwa kuwa huru. Viongozi wa upinzani nchini Djibouti wametangaza kutotambua ushindi wa Rais Ismail Omar Guelleh katika uchaguzi mkuu uliofanyika Ijumaa iliyopita. Muhammed Tourtour, mmoja wa wagombea watano wa upinzani katika uchaguzi huo ametaja kama kichekesho na ndoto tangazo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi kwamba Rais Guelleh alishinda kiti hicho kwa asilimia 86 na kusisitiza kuwa, uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu na kasoro nyingi. Licha ya vyama vingi vya upinzani kususia uchaguzi huo, lakini Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi imesema kuwa asilimia 68 ya watu laki 1 na 87 elfu waliotimiza masharti ya kupiga kura walijitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo, madai ambayo upinzani unasema kuwa hayaingii akilini. Rais Guelleh mwenye umri wa miaka 68, amekuwa madarakani tokea mwaka 1999.
Djibouti ambayo ni nchi ndogo ya Pembe ya Afrika yenye idadi ya watu wasiofikia hata milioni moja, mwaka 2011 ilishuhudia wimbi la maandamano ya kupinga kuchaguliwa tena Rais Guelleh ambaye ilisemakana kuwa alipata asilimia 80 ya kura zilizopigwa. Maandamano hayo yalijiri baada ya Rais Guelleh kuifanyia marekebisho katiba ya nchi, ili kumruhusu kugombea kiti hicho kwa mara ya tatu mfululizo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages